1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuondosha wanajeshi wake Mali

Mohammed Khelef
14 Aprili 2023

Ujerumani inajitayarisha kuwaondosha wanajeshi wake kwenye kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, ingawa itaendeleza ushirikiano wa maendeleo na mataifa ya Sahel kama njia ya kukabiliana na kitisho cha usalama.

https://p.dw.com/p/4Q3sd
Mali Verteidigungsminister Pistorius im Camp Castor
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Hatua za kiusalama zinaimarishwa wakati mawaziri hao wawili kutoka Ujerumani wakiwasili kwenye Kambi ya Castor. Hapa ndipo yalipo makaazi rasmi ya kikosi cha jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, kwenye mji wa Gao ulio kwenye eneo tete la kaskazini mwa Mali. 

Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius na mwenzake wa maendeleo, Svenja Schulze, wanasafiri kwa mara ya kwanza pamoja wakitaka kujifunza hali ya hatari wanayokabiliana nayo wanajeshi wa Kijerumani waliotumwa huko.

Soma zaidi: Wanajeshi 10 wauawa Niger na wanaoshukiwa kuwa magaidi

Ujumbe wao ni mmoja: kwamba maendeleo hayawezekani pasipo usalama na bila maendeleo usalama hauna maana.

"Tupo hapa kwa muda mrefu kutoa msaada wa kijeshi, lakini hata kama uhusiano huo wa kijeshi utakapomalizika, bado ushirikiano wa kimaendeleo utaendelea. Tutaendelea kuwapo kwa ajili hiyo." Anasema Waziri Svenja Schulze.

Hata hivyo, ikiwa kila jambo litakwenda kama lilivyopangwa na serikali ya Ujerumani, basi mwisho wa kikosi hiki cha Bundeswehr nchini Mali utakuwa mwezi Mei 2025. Kufikia hapo, Kambi ya Castor yenye vifaa na majengo mengi itakuwa imeshavunjwavunjwa kabisa.

Kiini cha uasi wa makundi ya itikadi kali

Mali ni  kiini cha uasi wa makundi yenye itikadi kali kwenye Ukanda wa Sahel. Kutoka hapa, ndipo matawi ya makundi ya Al-Qaida na lile lijiitalo Dola la Kiislamu yanapochipukia na kusambaa kwengine.

Mali Svenja Schulze im Minusma Camp in Gao
Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Svenja Schulze (kushoto) akiwa kwenye kambi ya MINUSMA mjini Gao, kaskazini mwa Mali.Picha: Mey Dudin/epd

Wapiganaji hao wanasababisha machafuko yasiyo mfano na khofu isiyo mipaka kwa watu wa hapa.

Soma zaidi: Waasi wenye mafungamano na IS wachukua udhibiti wa mji wa Tidermene, Mali

Matokeo yake, ni mamia kwa maelfu ya wakimbizi, njaa na mateso, ndani ya Mali kwenyewe na kwenye ukanda mzima.

Katikati ya haya, wanajeshi 1,100 wa Ujerumani wana wajibu wa kuwalinda raia, kurejesha utulivu kwenye nchi hiyo na kuhakikisha usalama, maana wao ni sehemu ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo, MINUSMA.

Ujerumani inaondoka, Urusi inajiimarisha

Lakini Bundeswehr haijawahi kuwa na uwezo wa kutimiza jukumu lake hili kwa miezi kadhaa sasa.

Mali Verteidigungsminister Pistorius im Camp Castor
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Boris Pistorius, (kushoto) akizungumza na wanajeshi wa nchi yake wanaohudumu kwenye Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali. Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius anasema ni "bahati mbaya kwamba jeshi la nchi yake linapaswa kuondoka katika hali hiyo ya mazingira ya kushindwa kwa lengo lao," kwani ukweli ni kuwa usalama haujaimarika nchini Mali.

Miaka 10 iliyopita, serikali ya Mali iliyaomba mataifa ya Magharibi kuingia nchini humo na kurejesha amani, lakini baada ya mapinduzi ya kijeshi mara mbili ndani ya kipindi cha miaka miwili, kuna mambo mengi yamebadilika.

Mtawala mpya, Rais Assimi Goita mwenye umri wa miaka 40, anamtegemea mshirika mpya kwenye kuusaidia utawala wake wa kijeshi, yaani Urusi ambayo uwepo wake unaonekana kila mahala.