1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaonyesha makombora yake ya masafa marefu mjini Tehran

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
7 Januari 2022

Iran imeadhimisha miaka miwili tangu jeshi lake lilipoitungua ndege ya abiria ya Ukraine kwa kuonesha hadharani makombora matatu ya masafa marefu huku mazungumzo ya nyuklia ya mjini Vienna yakiwa yanaendelea.

https://p.dw.com/p/45GNs
Iran Tehran | Trauernde | Qassem Soleimani
Picha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Shambulio hilo lilizua machafuko nchini Iran kote na wakati huo huo kuuharibu zaidi uhusiano wake na nchi za Magharibi. Iran ilikubali mnamo Januari 2020 kwamba walinzi wake wa kijeshi wa Mapinduzi ya Iran waliiangusha ndege hiyo kimakosa na mahakama ya kijeshi ilianza kusikiliza kesi ya watu 10 wanaoshukiwa kuhusika katika kuiangusha ndege ya hiyo ya Ukraine mnamo Novemba mwaka jana.

Ndege hiyo ya Ukraine iliangushwa siku hiyo hiyo ambapo Iran ilishambulia kambi za Marekani nchini Iraq ili kulipiza kisasi shambulio la ndege isiyo na rubani ya Marekani iliyomuua jenerali mkuu Qassem Soleimani mjini Baghdad mnamo mwaka 2020. Abiria wote 176 waliokuwamo kwenye ndege hiyo ya Ukraine waliuawa.

Kikosi cha jeshi la walinzi wa mapinduzi ya Iran kimesema makombora hayo yenye nguvu yana uwezo wa kufika umbali wa hadi kilomita 1000.

Wajumbe wa nchi sita zenye nguvu duniani wanaofanya mazungumzo na Iran mjini Vienna Austria.
Wajumbe wa nchi sita zenye nguvu duniani wanaofanya mazungumzo na Iran mjini Vienna Austria.Picha: EU Delegation in Vienna/Handout/AFP

Wanadiplomasia kutoka nchi ambazo zimesalia katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 ambazo ni Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na China zinashirikiana na Iran katika juhudi za kuyafufua makubaliano, ambayo kwa upande wake Iran inatakiwa kusimamisha mpango wake nyuklia na kwa nchi hizo zenye nguvu kuifungulia Iran biashara.

Duru ya nane ya mazungumzo ilianza tena siku ya Jumatatu baada ya mataifa makubwa kuyaongeza madai mapya ya Iran kwenye ajenda. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa amesema hatua za maendeleo zimepigwa kwenye mazungumzo hayo.

Wanadiplomasia wa nchi za magharibi wameonyesha kuwa na matumaini kwamba mafanikio yanaweza kupatikana mwishoni mwa mwezi huu wa Januari au mapema mwezi ujao, ingawa tofauti bado zipo na masuala magumu zaidi bado hayajatatuliwa. Iran imekataa mashinikizo yoyote kuhusu muda wa mazungumzo hayo yaliyowekwa na mataifa ya Magharibi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-AbdollahianPicha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Press Wire/picture alliance

Waziri wa mabo ya nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian pia amependekeza hali ya mazungumzo hayo inaridhisha lakini amesisitiza msimamo wa nchi yake kwamba vikwazo vyote lazima viondolewe na Marekani inapaswa kutoa dhamana kwamba haitajitoa tena kutoka kwenye makubaliano.

Vyanzo: AP/RTRE