1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kutowanyonga watuhumiwa wa vurugu za maandamano

15 Januari 2026

Iran imelifunguwa tena anga lake huku ikisema haina nia ya kuwanyonga watuhumiwa waliotiwa nguvuni kwa vurugu na mauaji kwenye maandamano makubwa kabisa ya umma kuwahi kushuhudiwa tangu mapinduzi ya 1979.

https://p.dw.com/p/56qnB
Iran Teheran 2026 | maandamano ya umma
Muandamanaji anayeiunga mkono serikali akipeperusha bendera jijini Tehran.Picha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Kwa mujibu wa shirika la Flightradar24 linalofuatilia safari za anga, Iran iliiondosha marufuku hiyo majira ya saa nne usiku wa kuamkia leo, baada ya kulifunga anga lake kwa takribani masaa matano, isipokuwa kwa ndege za kimataifa zenye ruhusa maalum, kuanzia saa 11 na robo jioni ya jana, Jumatano.  

Kufungwa na kufunguliwa huko kwa anga la Iran kunakuja wakati Rais Trump wa Marekani akisema amejulishwa kuwa mauaji dhidi ya waandamanaji yamekoma na kwamba hakutakuwa na hukumu ya kifo kwa wale waliokamatwa kwenye maandamano hayo. 

Hata hivyo, tayari Washington ilishawaamuru baadhi ya maafisa wake kuondosha kwenye vituo vya kijeshi na balozi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake, Iran imesema iko tayari kwa chochote kitakachotokea, huku ikiionya Marekani dhidi ya uamuzi unaoweza kuhatarisha maisha na maslahi ya kila mmoja, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi.

"Iran imeshathibitisha mara zote kwamba iko tayari kwa majadiliano, kwa diplomasia. Tumethibitisha ndani ya kipindi cha miaka 20, mwaka 2015, mwaka 2025, kila mara. Lakini ni Marekani ambayo daima inaikimbia diplomasia na kuchagua vita. Ujumbe wangu ni kuwa baina ya vita na diplomasia, diplomasia ni njia bora zaidi, ingawa hatuna uzoefu mzuri kutoka Marekani, ila bado diplomasia ni bora zaidi kuliko vita. Isipokuwa hilo ni juu ya rais wa Marekani kuamua." Alisema Arraghchi.

Waandamanaji kutonyongwa

Shirika la habari la Iran limeripoti hivi leo kwamba kijana wa miaka 26 aliyekamatwa wakati wa maandamano katika mji wa Karaj, Essam Soltani, hajanyongwa, likikanusha ripoti za mashirika ya haki za binaadamu kwamba kijana huyo angenyongwa jana. 

Iran Teheran 2026 | maandamano ya waungaji mkono wa serikali
Waandamanaji wanaoiunga mkono serikali ya Iran wakipinga kile wanachosema ni uingiliaji kati wa Marekani na Israel.Picha: Fatemeh Bahrami/Anadolu/picture alliance

Soltani alitiwa nguvuni tarehe 10 Januari na ameshitakiwa kwa "kula njama dhidi ya usalama wa ndani na kuendesha propaganda dhidi ya dola."

Hata hivyo, chanzo kimoja cha mahakama kimethibitisha kwamba makosa hayo hayana adhabu ya kifo hata kama atatiwa hatiani, kinyume na uvumi uliokuwa ukisambazwa. 

Kwa ujumla, hali ya usalama imeaanza kurejea kuwa ya kawaida ndani ya Iran, kufuatia wiki kadhaa za maandamano na ghasia kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu mapinduzi ya mwaka 1979, ambazo zinadaiwa kupoteza maisha ya malefu ya watu. 

Serikali ya Iran inatuhumu mauaji hayo kufanywa na makundi yaliyopandikizwa kutoka nje, huku wanaharakati wakilituhumu jeshi maalum la Walinzi wa Mapinduzi kuwauwa waandamanaji.

Huduma ya intaneti imefungiwa kwa siku ya saba mfululizo na bado haijawa wazi lini zitafunguliwa rasmi.