Iran yakiri kituo cha Natanz kimeharibiwa kwa moto | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iran yakiri kituo cha Natanz kimeharibiwa kwa moto

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, AEOI, limesema kuwa kituo chake cha kurutubisha madini ya urani cha Natanz kimeharibiwa vibaya kwa moto.

Msemaji wa shirika hilo, Behrus Kamalvandi ameliambia jana shirika la habari la Iran, IRNA kwamba hakuna mtu yeyote aliyekufa katika tukio hilo, lakini kituo hicho kilichojengwa miaka saba iliyopita kimeharibiwa vibaya na moto huo uliozuka Alhamisi iliyopita.

''Tukio kwenye kituo cha Natanz halijasababisha uharibifu kwenye kinu kikubwa cha kurutubisha madini ya urani, ingawa moja ya kituo kinachoendelea kujengwa kwenye eneo la wazi cha Natanz kimeharibiwa vibaya kwa moto huo ambao chanzo chake kinachunguzwa. Ni kweli kuna uharibifu mkubwa wa vifaa na kwa sasa tunatathmini uharibifu huo,'' alifafanua Kamalvandi.

Chanzo cha moto kuwa siri

Kamalvandi amesema kutokana na sababu za kiusalama, uongozi wa Iran hautatoa maelezo zaidi kuhusu chanzo cha moto huo. Hata hivyo, Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limesema hakukuwa na vifaa vyovyote vya nyuklia katika kituo cha Natanz ambacho sehemu yake kubwa iko chini ya ardhi. 

Kamalvandi amesema tukio hilo huenda likachelewesha maendeleo ya urutubishaji wa madini ya urani kwa muda, lakini serikali ya Iran itakikarabati kituo hicho kwa kujenga jengo kubwa lenye vifaa vya kisasa zaidi. Mara baada ya moto kuzuka, maafisa wa Iran walikanusha kuhusu tukio hilo, wakidai kwamba moto huo uliunguza tu eneo la kiwanda.

Iran Kamalwandi

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, AEOI, Behrus Kamalvandi

Baadhi ya maafisa wanahofia kwamba huenda mataifa adui wa Iran kama vile Marekani na Israel yanahusika na tukio hilo, lakini hakuna ushahidi au uthibitisho ambao umetolewa. Katika siku za nyuma, kirusi cha kwenye komyputa cha Stuxnet kilitumika kukivamia kituo cha nyuklia cha Natanz. Iliaminika kwa kiasi kikubwa kwamba Marekani na Israel ndiyo walikitengeza kirusi hicho.

Hivi karibuni, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Nishati ya Nyuklia, IAEA liliishinikiza Iran kuruhusu ukaguzi wa nyuklia kwenye vinu vyake vya nyuklia vyenye utata. Kituo cha Natanz kimekuwa kikifuatiliwa na IAEA.

Iran yakanusha kuwa na silaha za nyuklia

Shirika hilo na washirika wake wa Magharibi waliamini kuwa kituo hicho kilikuwa kitovu cha mpango wa silaha za nyuklia wa Iran hadi mwaka 2003. Hata hivyo, Iran imekanusha kutengeneza silaha za nyuklia.

Iran iliachana na mpango wake wa nyuklia baada ya kufikia makubaliano na mataifa sita yenye nguvu duniani mwaka 2015. Vikwazo muhimu vilivyowekwa dhidi yake viliondolewa chini ya makubaliano hayo. Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump alijiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018, na kuiwekea Iran vikwazo vipya. Iran nayo ilisema itaacha kuheshimu ukomo wa kurutubisha madini ya urani uliowekwa katika makubaliano hayo.

Katika tukio tofauti, jeshi la Iran limesema kile kinachoitwa ''miji ya makombora'' imejengwa kwenye vituo vya chini ya ardhi katika pwani ya Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman. Vyombo vya habari vya Iran jana vilimnukuu kamanda wa jeshi la majini, Ali Reza Tangsiri, ambaye amesema wako tayari kuwatisha maadui wa Iran ambao wanataka kuanzisha uchokozi wa kijeshi.

(AP, DPA, Reuters, DW https://bit.ly/2Z4l8eq)

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com