1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaendeleza mashambulzi dhidi ya meli za mafuta Hormuz

12 Machi 2026

Boti za Iran zimezishambulia meli mbili za mafuta katika Mlango Bahari wa Hormuz, upande wa Iraq. Milipuko iliyotokana na mashambulizi hayo imesababisha kifo cha mfanyakazi mmoja wa meli.

https://p.dw.com/p/5AFrI
Maji ya Iraq 2026 | Meli ya mafuta inayowaka moto baada ya shambulio linalodhaniwa kufanywa na Iran kwa kutumia boti zenye vilipuz
Meli ya mafuta ikiwaka moto baada ya shambulio linalodhaniwa kufanywa na Iran kwa kutumia boti zenye vilipuzPicha: Media Office of Iraqi Ports/REUTERS

Iraq imesema kuwa imefunga kwa muda operesheni zote katika bandari zake za mafuta kutokana na mashambulizi ya Iran yaliyozilipua meli mbili za mafuta kwenye Mlango Bahari wa Hormuzupande wa Iraq. 

Meli zilizoshambuliwa Safesea Vishnu, iliyokuwa na bendera ya Kisiwa cha Marshall na Zeyfros, iliyopeperusha bendera ya Malta zilikuwa zikiendelea na shughuli zake karibu na bandari ya Al Faw wakati wa tukio.

Kando ya mfanyakazi mmoja wa meli aliyeuwawa, watu wengine 38 waliokolewa kutoka kwenye meli kulingana na televisheni ya taifa ya Iraq.

Wakati huohuo, Oman nayo imeziondoa meli zake zote kutoka katika bandari kuu ya Mina Al Fahal kama hatua ya tahadhari ili kukwepa mashambulizi, kwa mujibu wa shirika la habari la Bloomberg.

Oman, Muscat 2026
Meli zikiwa zimetia nanga Muscat, OmanPicha: Benoit Tessier/REUTERS

Bandari hiyo iko katika eneo la kimkakati la ghuba ya Oman nje kidogo ya mlango bahari wa Hormuz uliozuiwa na Iran. Hilo linaifanya kuwa moja ya bandari chache zinazotoa njia mbadala kwa meli za mafuta kutoka Mashariki ya Kati.

Masoko ya dunia ya mafuta yako kwenye hali mbaya

Aidha kutokana na mzozo huo wa Mashariki ya kati unaovuruga upatikanaji wa mafuta, Mkurugenzi wa Shirika la IEA Fatih Birol mara baada ya kutangaza kutoa kiasi hicho cha mapipa ya mafuta amesema kwa sasa masoko ya dunia ya nishati yako katika hali mbaya.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni IEA ilisema kuwa uzalishaji wa mafuta ulikuwa wa kiwango cha chini kwa karibu mapipa milioni 8.0 kwa siku na mapipa mengine milioni 2.0 ya bidhaa zinazotokana na petroli.

Shirika hilo linaloundwa na mataifa 32 yanayotumia mafuta zaidi duniani. Mapema Jumatano, ilitangaza kutoa mapipa milioni 400 ya mafuta kutoka katika hifadhi zake za kimkakati ili kukabiliana na changamoto kubwa zaidi ya upatikanaji wa bidhaa hiyo kuwahi kutokea katika historia.