Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani zaafikiana | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani zaafikiana

Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani zimefikia makubaliano muhimu jana jioni ambayo ni hatua kubwa katika kuelekea makubaliano kamili kuhusu kuizuia Iran kutengeza silaha za kinyuklia.

Baada ya miaka kumi na miwili ya vuta nikuvute kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China na Marekani pamoja na Ujerumani ambayo sio mwanachama wa kudumu, pande hizo mbili hapo jana zimekubaliana kuhusu masuala muhimu yaliyokuwa yakizua utata kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran.

Makubaliano hayo muhimu lakini yasio kamili yalifikiwa mjini Lausanne, Uswisi baada ya mazungumzo ya kina ya usiku na mchana yaliyodumu kwa siku nane mfululizo.

Obama: Ni makubaliano ya kihistoria

Rais wa Marekani Barack Obama amesema nchi yake na washirika wake wamefikia makubaliano ya kihistoria na Iran ambayo iwapo yatatekelezwa kikamilifu basi yataizuia Iran kutengeneza silaha za kinyuklia. Hata hivyo ametahadharisha kuwa ufanisi wa makubaliano hayo hauwezi kuhakikishwa hivi sasa.

Rais wa Marekani Barack Obama akizungumzia makubaliano na Iran

Rais wa Marekani Barack Obama akizungumzia makubaliano na Iran

Iran kwa upande wake italegezewa vikwazo vya kiuchumi lakini kwasasa baadhi ya vikwazo hivyo vinasalia hadi makubaliano kamili yatakapofikiwa tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu.

Raia wa Iran wamejitokeza katika mji mkuu wa nchi hiyo Tehran, hii leo kusherehekea kufikiwa kwa makubaliano hayo muhimu na video zilizowekwa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha makundi ya watu wakiimba kumsifu Rais wa Iran Hassan Rouhani.

Kuna masuala kadha wa kadha ambayo yanahitaji kupigwa msasa kuhusiana na makubaliano hayo. Wanadiplomasia wanasema makubaliano hayo ni tete na huenda yasitekelezwe kama inavyotarajiwa kati ya sasa na hadi tarehe 30 mwezi Juni kama ilivyopangwa.

Iran sasa itaanza kuondolewa vikwazo hatua kwa hatua na kupewa misaada kutoka kwa Marekani na Umoja wa Ulaya na kuondolewa baadhi ya vikwazo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa iwapo itayaheshimu makubaliano hayo.

Chini ya makubaliano hayo, Iran itapunguza urutubishaji wa madini ya Urani kwa thuluthi mbili ili kuihakikishia Jumuiya ya kimataifa kuwa haitakuwa na uwezo wa kuunda zana za kinyuklia, kukivunja kinu chake kinachozalisha Plutonium na kukubali kufanyiwa uchunguzi huru na wataalamu wa masuala ya atomiki wakati wowote.

Iran yasema safari bado ni ndefu

Israel imepinga vikali makubaliano hayo ya jana na kusema Iran inasalia kuwa kitisho kwake na ulimwengu hasa kutokana na kupewa muda wa miaka kumi kupunguza kabisa uwezo wake wa kinyuklia. Wabunge wa upinzani nchini Marekani wa chama cha Republican pia wameyashutumu makubaliano hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarid amesema bado wana safari ndefu kufikia kule wanakotaka kufika. Naye mwenzake wa Marekani John Kerry amesema kuna masuala mengi ya kiufundi ambayo yanahitaji kushughulikiwa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Fedrica Mogherini amesema Marekani na Umoja huo zitaanza kuiondolea vikwazo Iran punde tu baada ya shirika la umoja wa Mataifa la kudhibiti silaha za atomiki likapothibitisha kuwa Iran imeheshimu yaliyofikiwa.

Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema Jumuiya ya Kimataifa haijawahi kuwa karibu kuafikiana na Iran kuhusu mpango wa kinykulia kama sasa.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com