Hospitali mbili zapigwa mabomu nchini Syria | NRS-Import | DW | 05.02.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Syria

Hospitali mbili zapigwa mabomu nchini Syria

Majeshi ya serikali ya Syria na Mshirika wake Urusi yamezipiga hospitali mbili, jengo moja la ghorofa na sehemu zingine ambazo zililengwa na majeshi hayo katika jimbo la waasi la Idlib.

Wanaharakati leo hii Jumatatu, wameelezea kuwa mashambulio hayo yanafanyika hasa baada ya wapiganaji wa kundi la Al Qaida kuidungua ndege ya kijeshi ya Urusi mnamo siku ya Jumamosi iliyopita karibu na mji wa Saraqeb na kumuua rubani wa ndege hiyo. Na kutokea hapo mashambulio dhidi ya maeneo ya waasi yameongezeka.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu, takriban watu 23 wameuawa kutokana na mashambulizi hayo ya majeshi ya serikali ya Syria baada ya kuushambulia ngome za waasi katika vitongoji vya Ghouta Mashariki, karibu na mji mkuu wa Damascus.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa watoto wanne ni miongoni mwa wale waliouawa, Shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza limesema watu wengine tisa wameuwawa baada ya soko lililo katika mji wa Beit-Sawa kushambuliwa.

wanajeshi wa Uturuki (Getty Images/AFP/B. Kilic)

Wanajeshi wa Uturuki

Wakati huo huo jeshi la Uturuki limesema msafara wa askari wake umeingia katika jimbo la Idlib kaskazini magharibi mwa Syria kwa ajili ya kuanzisha kituo kipya cha uchunguzi kwa lengo la kudhibiti vurugu chini ya makubaliano na Urusi. Jeshi hilo limesema kuwa kituo hicho ni cha nne kufunguliwa katika jimbo la Idlib kulingana na mazungumzo ya amani ya mjini Astana, Kazakhstan.

Idlib, ambayo kwa kiasi kikubwa inadhibitiwa na vikosi vya waasi wa Kiislamu, ipo upande wa magharibi mwa eneo la Afrin ambalo linadhibitiwa na Wakurdi ambalo linalengwa zaidi katika operesheni kubwa ya kijeshi inayofanywa na jeshi la Uturuki.

Jamii ya kimataifa imeelezea wasiwasi wake kuhusu hatima Ghouta Mashariki wakati ambapo majeshi ya serikali ya Syria na washirika wake Urusi wanaendelea kuushambulia mji huo na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula pamoja na madawa hali ambayo imesababisha utapiamlo.

Rais wa Syria Bashar al Assad na rais wa Urusi Vladimir Putin (picture alliance/ dpa/TASS/M. Klimentyev)

Marais wa Syria Bashar al Assad na wa Urusi Vladimir Putin

Assad na washirika wake wameongeza kasi katika vita hivyo vya miaka saba, na wameweza kuyateka maeneo kadhaa na kuwafurusha waasi kutoka kwenye maeneo mengi na miji mikubwa, hali iliyoyalazimisha baadhi ya makundi kujisalimisha mnamo mwaka jana.

Wakati hayo yakijiri Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alikutana leo hii na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis katika mji wa Vatican. Polisi walikuwa na kibarua kigumu cha kuwadhibiti  waandamanaji wakati ambapo hisia zinaendelea kuwa kali kutokana na operesheni ya Uturuki dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi ndani ya Syria. Papa Francis alimpa Erdogan kisanamu kilichokuwa na picha ya malaika anayemkaba shetani  - ikiwa ni ishara ya kukumbushia amani na haki.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Gakuba Daniel

 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com