Ghasia za Kisiasa nchini Thailand. | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 13.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Ghasia za Kisiasa nchini Thailand.

Ghasia zimeendelea leo nchini Thailand, wakati Jeshi la nchi hiyo likiwachukulia hatua kali Waandamanaji wanaopinga serikali. Wanajeshi walifyatua risasi kuwaonya waandamanaji waliojibu kwa kurusha mabomu ya petroli.

default

Wanajeshi wa Thailand katika juhudi za kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok.

Milio ya risasi ilisikika leo katika mji mkuu wa Thailand Bangkok huku wanajeshi wakfyatua maji ya mizinga kwa waandamanaji wanaoipinga serikali ya nchi hiyo wakati ghasia zikiongezeka katika mji huo.


Mapigano hayo yameongezeka leo baada ya wanajeshi kujaribu kuzima ghasia hizo za waandamanaji hao wanaoipinga serikali ya nchi hiyo, ambao wanazidi kutaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo kujiuzulu.


Mapema leo, katika maeneo tofauti ya mji huo, Wanajeshi walifyatua risasi angani na kurusha mabomu ya gesi kuwatawanya waandamanaji hao ambao walikuwa wameziba barabara na makutano mengine ya barabara.


Katika ghasia hizo waandamanaji hao wanaomtii, Waziri Mkuuu wa zamani wa nchi hiyo Thaksin Shinawatra pia walichoma moto Mabasi kadhaa.

Madaktari nchini humo wanasema watu kadhaa wametibiwa majeraha waliyoyapata, baada ya polisi wakitumia mabomba ya maji kujaribu kuwatawanya waandamanaji wanaopinga serikali ya nchi hiyo.


Takriban watu 77, wamejeruhiwa katika ghasia hizo, ikiwemo 19 waliolazwa hospitali, ambapo wanne kati ya hao wamejeruhiwa kwa risasi, wakiwemo raia wawili na askari wawili.Msemaji wa jeshi la nchi hiyo amesema waandamanaji kadhaa wamekamatwa.


Aidha amesema ghasia hizo ilianza wakati wanajeshi waliokuwa ndani ya magari yao walipokuwa wakiwataka waandamanaji hao waliovaa fulana nyekundu kuondoka katika eneo walilolizingira la makutano ya njia ya Din Daeng.


Hata hivyo waandamanaji hao wametishia kutoondoka katika eneo hilo kwa madai ya kuwa wanataka demokrasia kamili.


Ghasia nchini humo, zimesababisha kuvunjwa kwa mkutano wa Viongozi wa Jumuia ya Nchi za Kusini -Mashariki mwa Asia -ASEAN.

Wakati ghasia hizo zikionekana kuzidi kuendelea serikali ya Thailand imesema itahakikisha usalama katika viwanja vya ndege na Bandari.


Awali akizungumza kwa njia ya Televisheni, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abhisit Vejajjiva alitishia kutumia nguvu kuzima ghasia hizo zinazofanywa na waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok. Katika taarifa yake aliwataka waandamaji kuelewa kwamba kitendo chao si cha kisheria.

Aliwataka kuheshimu sheria na kusitisha hatua yao mara moja.


Aidha aliwataka wananchi kutulia, wakati serikali ikirejesha hali ya kawaida.

Ghasia hizo zinatokea wakati nchi hiyo ikiadhimisha sherehe za mwaka mpya, zinazojulikana kama Songkran.


Wanajeshi wa nchi hiyo yamekua wakikabiliwa na shinikizo kubwa la serikali, kuhakikisha wanawaondoa waandamanaji wote, ambao walikuwa katika majengo mbalimbali ya serikali pamoja na eneo la uwanja wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje.


Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Mohamed Abdul-rahman

 • Tarehe 13.04.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HVbd
 • Tarehe 13.04.2009
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/HVbd
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com