1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yafikia makubaliano kuhusu bei ya nishati

Tatu Karema
21 Oktoba 2022

Viongozi wa EU wamefikia makubaliano ya hatua za kuwalinda raia kutokana na ongezeko la bei ya nishati. Makubaliano hayo yameafikiwa baada ya masaa 11 ya mvutano kuhusu mapendekezo ya kupunguza gharama ya nishati

https://p.dw.com/p/4IVqG
EU-Kommissionspräsidentin von der Leyen
Picha: Jean-Francois Badias/AP/dpa/picture alliance

Jumuiya hiyo ya nchi wanachama 27 imekuwa ikivutana kwa muda wa miezi kadhaa kuhusu mipango ya pamoja ya kukabiliana na ongezeko hilo la bei ya nishati kutokana na ukweli kwamba matumizi ya nishati katika mataifa ya Jumuiya hiyo yanatofautiana pakubwa. Huku tangazo hilo la makubaliano likionesha mshikamano kwa umma, ni wazi kwamba mazungumzo yatakayofuata yatabaki kuwa magumu.

Akizungumza na waandishi wa habari, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema makubaliano ya mkutano huo wa kilele yameweka utaratibu mwafaka wa kuendelea kufanyia kazi suala la bei ya nishati. von der Leyen ameongeza kuwa wanalenga  kutoa hadi euro bilioni 40 ya fedha ambazo bado zinapatikana kwenye mfuko wa bajeti wa mwaka uliopita . Kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya amesema kutokana na hatua hiyo, nchi wanachama zitaweza kusaidia walioathiriwa zaidi na mgogoro wa nishati iwe ni familia  zilizo hatarini, au biashara ndogondogo.

Makubaliano hayo yanaitaka Halmashauri kuu ya Ulaya na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya kutafuta njia katika wiki zijazo kuwalinda raia dhidi ya bei za juu huku yakidumisha ushindani wa Kimataifa wa Ulaya na uadilifu wa soko la pamoja.

Ukraine | Präsident Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine- Volodymyr ZelenskyPicha: Ukrainian President'S Office/APA Images/ZUMA/picture alliance

Huku hayo yakijiri, Rais wa baraza la Ulaya Charle Michel amesema kwamba mzozo wa nishati unawakilisha tishio kwa soko la ndani la Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa uratibu wa hali ya juu unahitajika kulilinda. Takriban mataifa 15 ya Umoja wa Ulaya hii ikiwa zaidi ya nusu ya mataifa wanachama, yanashinikiza kupunguzwa kwa bei na yanatatizwa na migomo na maandamano yanayotokana na kupanda kwa gharama ya maisha kutoka Ufaransa, Ubelgiji na mataifa mengine ya Umoja huo.

Wakati huo huo, akiwa njiani kwa mkutano wa siku ya pili ya kongamano hilo, waziri mkuu wa Latvia Krisjanis Karins, amesema kuwa Umoja wa Ulaya lazima udumishe umoja katika msaada wake kwa Ukraine na kuanza kuchukuwa hatua za kuiwajibisha Urusi kisheria kwa shughuli zake za kivita.

Siku ya Alhamisi, akilihutubia kongamano hilo kwa njia ya video , rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alionya kuwa Urusi inapanga kulipua mtambo wa kuzalisha umeme wa maji wa Kakhovka katika eneo la Kherson ambapo wanajeshi wa Ukraine wanasonga mbele. Zelensky ameongeza kuwa Urusi inapanga kwa makusudi kusababisha maafa makubwa Kusini mwa Ukraine . Zelensky ameonya kuwa iwapo mtambo huo utalipuliwa , huenda kukawa na mafuriko makubwa ambayo yataathiri Kherson na maelfu ya watu kuathirika .