Ethiopia: Waasi wa Tigray wathibitisha kurusha makombora Eritrea | Matukio ya Afrika | DW | 15.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Ethiopia

Ethiopia: Waasi wa Tigray wathibitisha kurusha makombora Eritrea

Kiongozi wa waasi katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia amethibitisha kwamba wamerusha makombora kuulenga mji mkuu wa Asmara katika nchi jirani ya Eritrea.

Kundi hilo la waasi wa Tigray pia limetishia kufanya mashamulio zaidi hali inayoashiria kuongezeka kwa mivutano katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia kati ya vikosi vya Tigray na vile vya serikali ya mjini Addis Ababa. Vita hivyo vimesogea hadi kwenye sehemu za mipaka ya kimataifa.

Rais wa mkoa wa Tigray Debretsion Gebremichael, alipozungumza kwa njia ya simu mnamo siku ya Jumapili na shirika la habari la Associated Press, hakutaja idadi ya makombora yaliyorushwa katika mji wa Asmara ingawa alitaja kuwa mji huo kuwa ndio wa pekee uliolengwa.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa waonya kuhusu 'uhalifu wa kivita' Tigray

Vita vya wenyewe kwa wenyewe

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia kati ya serikali ya mkoa wa Tigray ambayo wakati mmoja ilitawala kwenye serikali ya muungano na serikali ya sasa ya waziri mkuu Abbiy Ahmed mshindi wa tuzo Amani ya Nobel ambaye mageuzi yake makubwa yameutenga na kuupunguzia nguvu mkoa wa Tigray, vinaweza kusababisha kumpoteza mshirika muhimu wa masuala ya usalama ambaye ni Marekani na hatua hiyo italidhoofisha eneo la Pembe ya Afrika, na kusababisha maelfu ya wakimbizi kuingia nchini Sudan.

Baadhi ya raia wa Ethiopia wanaokimbia mapigano katika jimbo la Tigray na kuingia nchini Sudan

Baadhi ya raia wa Ethiopia wanaokimbia mapigano katika jimbo la Tigray na kuingia nchini Sudan

Hali ya tahadhari

Katika taarifa ya tahadhari ya usalama iliyotolewa na ubalozi wa Marekani nchini Eritrea umetaja mfululizo wa kelele kubwa zilizosikika katika mji mkuu, Asmara mnamo siku ya Jumamosi usiku. Hata hivyo Eritrea haijatoa tamko lolote.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika taarifa fupi ametangaza kwamba nchi yake ina uwezo wa kuyafikia malengo ya operesheni yake. Amesema '' Haki itatawala na Ethiopia itaondokana na kadhia hiyo!."

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR

Raia wa Ethiopia wapatao 25,000 wanaokimbia mzozo katika eneo la Tigray wamevuka na kuingia nchi jirani ya Sudan, shirika la habari la serikali SUNA limeripoti. Wakati huo huo shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, nchini Sudan limesema linafanya jitihada kuwapatia makazi watu hao. Wakimbizi hao wamewasili katika majimbo ya Gadaref na Kassala tangu siku ya Jumamosi.

Kamishna wa wakimbizi wa Sudan Abdullah Suleiman alizuru eneo la mpakani siku ya Jumamosi pamoja na mwakilishi msaidizi wa shirika hilo la wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Jan Hansmann kuzungumzia hali ya wakimbizi wanaomiminika nchini Sudan.

Hansmann, aliyenukuliwa na shirika la habari la Sudan SUNA, amesema kipaumbele cha UNHCR ni kuwapa wakimbizi makazi, chakula na maji na kisha kuwahamishia katika mikoa iliyo mbali na mpaka kwa sababu za kiusalama. Amesema shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linapanga kuanzisha kambi mpya nchini Sudan kwa ajili ya wakimbizi wanaotoka Ethiopia.

Soma zaidi:Mvutano wa nchini Ethiopia

Kulaumiana

​​Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

​​Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy amesema chama cha TPLF kilifanya uhaini kwa kuwashambulia wanajeshi wa serikali siku kumi zilizopita, lakini kwa upande wake Rais wa jimbo la Tigray Debretsion Gebremichael amesema hatua ya serikali ni kulipiza kisasi kwa mkoa huo kutokana na kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mnamo mwezi Septemba. Serikali ya shirikisho ilitaka kuchelewesha uchaguzi huo, kwa sababu ya Covid-19, lakini jimbo la Tigray liliendelea na uchaguzi wake ambapo chama cha TPLF kilipata ushindi mkubwa.

Vyanzo: AP/AFP