Erdogan: Tunatekeleza mkataba wa kupunguza ghasia Idlib | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.10.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Erdogan: Tunatekeleza mkataba wa kupunguza ghasia Idlib

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema nchi yake inatekeleza mkataba uliokubaliwa na Urusi na Iran ili kupunguza ghasia katika jimbo la Idlib lililoko kaskazini mwa Syria.

Akizungumza leo na wanachama wa chama tawala cha Uturuki cha AK katika jimbo la magharibi la Afyon, Erdogan amesema kwa sasa wanayatekeleza makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita katika mazungumzo ya Astana, Kazakhstan.

Amesema kama Uturuki isingechukua hatua, mashambulizi ya mabomu yangefanyika katika miji yao. Amesema juhudi zinazofanywa na Uturuki katika jimbo la Idlib zinaendelea kwa ushirikiano na wapiganaji wa kundi la waasi wa Jeshi Huru la Syria, bila ya kuwepo matatizo yoyote kwa sasa.

Erdogan ameitoa kauli hiyo wakati ambapo tayari vikosi vya Uturuki vimeanzisha mapambano na wapiganaji wa jihadi wa kundi la muungano la Hayat Tahrir al-Sham, HTS katika jimbo la Idlib katika eneo la mpaka wa Uturuki na Syria.

Syrien Soldaten (picture alliance/abaca/E. Sansar)

Wapiganaji wa Jeshi Huru la Syria

Msemaji wa kundi lenye silaha la Syria linaloungwa mkono na Uturuki, Mustafa Sejari, amesema kuwa mizinga ya kijeshi ya Uturuki ilijibu mashambulizi ya makombora baada ya kushambuliwa na wapiganaji wenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda katika eneo la mpaka.

Shirika la habari la Uturuki, Dogan limeripoti kuwa Uturuki leo ilifyatua makombora saba katika jimbo la Idlib. Sejari amesema operesheni hiyo ina lengo la kupeleka wapiganaji wa upinzani wanaoungwa mkono na Uturuki katika jimbo hilo linalodhibitiwa na wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda. ''Hadi sasa vikosi vyetu havijaingia Idlib,'' alisema Sejari wakati akizungumza na shirika la habari la Associated Press, AP.

Nalo shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London, Uingereza limesema kuwa makombora ya Uturuki yaliangukia karibu na kambi ya watu wasio na makaazi pembezoni mwa eneo la mpaka, na kusababisha taharuki ingawa hakuna watu walioathirika.

Mashambulizi yalifuatiwa na mapigano

Kwa mujibu wa shirika hilo, mashambulizi hayo ya makombora yalifuatiwa na mapigano yaliyodumu kwa muda mfupi na urushwaji wa makombora huku mvutano ukiendelea. Wakati huo huo, Shirika hilo pamoja na taasisi nyingine ya wanaharakati ya Thiqa, zimeripoti kuhusu kile kinachoonekana kuwa majeshi ya Uturuki yamesonga mbele kuingia Syria katika idadi kubwa ya magari yanayoelekea katika eneo kati ya Idlib na jimbo la Aleppo.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria limesema kuwa wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda pia wamepeleka wapiganaji wapya katika eneo ambako mapigano yalitokea kwa muda mfupi kwenye kijiji cha Kafr Lusin, pembezoni mwa mpaka.


Türkische Panzerfahrzeuge an der Reyhanli-Grenze im türkischen Hatay (picture alliance/dpa/abaca/C. Genco)

Gari la kijeshi la Uturuki katika mpaka wa Reyhanli likielekea Idlib

Sejari amesema mpango wa kuzuia kuenea kwa ghasia katika jimbo la Idlib, unahusisha kupeleka vikosi maalum vya Uturuki pamoja na kuifuta miradi yote ya kigeni ambayo ina lengo la kudhibiti kaskazini mwa Syria kwa kisingizio ca kupambana na ugaidi, kwa kuvitaja dhahiri vikosi vya Kikurdi vinavyoungwa mkono na Marekani.

Ama kwa upande mwingine, kiasi ya raia 11 wakiwemo watoto wawili wameuawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanyika leo katika soko lililoko kaskazini magharibi mwa Syria.

Shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria limesema huenda mashambulizi hayo katika eneo la Maaret al-Numan kwenye jimbo la Idlib yamefanywa na vikosi vya serikali.

Eneo kubwa la Idlib, ikiwemo Maaret al-Numan linadhibitiwa na Hayat Tahrir al-Sham. Watu wengine 20 wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo na idadi ya wahanga inaweza ikaongezeka.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters, http://bit.ly/2hWllgw
Mhariri: Yusra Buwayhid

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com