Eneo la mataifa ya maghreb laingia katika hali ya wasi wasi. | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Eneo la mataifa ya maghreb laingia katika hali ya wasi wasi.

Mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga nchini Algeria yanaamsha hali ya wasi wasi juu ya usalama wa muda mrefu wa eneo la Afrika ya kaskazini, eneo ambalo hali ya kudumaa kwa ukuaji wa uchumi na kisiasa inatoa kwa kundi la kigaidi la Al-Qaeda nafasi ya kuchochea hali ya machafuko karibu na bara la Ulaya.

Wachunguzi wachache wa masuala ya kisiasa wanaona kitisho katika muda mfupi ujao kwa watawala ambao wanaudhibiti mkubwa katika eneo hilo ambalo bara la Ulaya linapata asilimia 20 ya mahitaji yake ya gesi na wakaazi wake kwa mamilioni wanatembelea huko wakati wa likizo zao kila mwaka.

Na pia hauonikani uwezekano wa uasi wa kiwango kikubwa kama ule ulioitikisa nchi mwanachama wa OPEC Algeria katika miaka ya 90.

Hata hivyo , kutengwa kwa kiasi kikubwa kutoka siasa rasmi pamoja na kiwango cha chini cha ujenzi wa nafasi za kazi huenda ukatoa kwa makundi ya waasi wa Kiislamu, wataalamu wanasema , ambao licha ya kupungua idadi yao lakini wanazidi kuwa jasiri nchini Algeria , nafasi ya kujiongezea ushawishi katika mataifa jirani ya Tunisia, Morocco na Libya.

Kitisho ni kwamba kuongezeka kwa unyonge wa kijamii kunaweza kusaidia makundi yenye silaha kuwaandikisha vijana wengi zaidi ili kufanya mashambulizi haya ya kujitoa muhanga ya aina ambayo imesababisha vifo vya watu kadha nchini Algeria mwaka huu.

Mtindo kama huu utaathiri hali ya kujiamini katika eneo hilo ya kujaribu kuwavutia wawekezaji, kuimarisha bishara katika eneo hilo na kuwapa watu matumaini.

Kwa kijana aliyemaliza chuo kikuu na ambaye hana kazi Abdeslam Selmane , na pia kwa mamia kwa maelfu ya vijana wa eneo hilo la maghreb, suluhisho linaweza kuwa ni uhamiaji haramu katika maboti kwenda Ulaya kuliko kujiunga na ugaidi. Nahitaji kazi, nyumba , vitu muhimu kwa ajili ya maisha bora, amesema kijana huyo mwenye umri wa miaka 23. Kuondoka nchini kwa njia yoyote ile ndio suluhisho langu.

Mtengano katika eneo hilo , baina ya watawala na watawaliwa limekuwa linaonekana kuwa hatari. Katika waraka uliotolewa mwaka 2005, mtaalamu wa Marekani katika masuala ya eneo la maghreb John Pierre Entelis ameandika , kuwa ugaidi ni matokeo ya kushindwa kwa mageuzi muhimu na kufanyia mageuzi utaratibu wa kisiasa wa eneo la maghreb. Mwaka huu umeshuhudia shambulio la kwanza la kujitoa muhanga pamoja na kujitokeza kwa kiwango kidogo sana kwa asilimia 35 na 37 katika uchaguzi wa bunge nchini Algeria na Morocco, na kuongeza wasi wasi uliopo juu ya matokeo ya ubanaji mkubwa wa ushiriki wa kisiasa.

Tunisia na Libya zimeongeza uchunguzi wao dhidi ya Waislamu wenye imani kali. Watu katika eneo hilo wanaamini kuwa kupiga kura ni kupoteza wakati. Kwa nini nipige kura, wanasema, iwapo haitasaidia chochote kubadilisha maisha yetu, amesema mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Algeria Mahmoud Belhimer. Kitu muhimu hapa ni uthabiti wa eneo lote. Na haiwezekani kuwa na uhakika wa kuwa na uthabiti bila ya kufungua milango ya demokrasia. Wasi wasi juu ya eneo hilo, umesaidia kutia msukumo katika pendekezo la Ufaransa kwamba la kutaka kile kinachoitwa umoja wa nchi zinazopakana na bahari ya Mediterranean ambao utaratibu masuala ya uhamiaji, ugaidi na maendeleo ya kiuchumi.

 • Tarehe 27.09.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7Y
 • Tarehe 27.09.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7Y

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com