Dhima mpya ya Uturuki Mashariki ya Kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Dhima mpya ya Uturuki Mashariki ya Kati

Miaka michache iliopita Uturuki imeibuka kuwa taifa lenye ushawishi Mashariki ya Kati.Imeimarisha sera zake za kigeni na imechukua dhima ya usuluhishi.

Der tuerkische Aussenminister Ahmet Davutoglu informiert am Dienstag, 16. Juni 2009, in Berlin auf einer Pressekonferenz mit seinem deutschem Amtskollegen Frank-Walter Steinmeier die Medien. (AP Photo/Markus Schreiber) ---Turkish Foreign Minister Ahmet Davutoglu briefs the media during a news conference with his German Frank-Walter Steinmeier in Berlin, Germany, Tuesday, June 16, 2009. (AP Photo/Markus Schreiber)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Ahmet Davutoglu.

Serikali ya Uturuki imeanzisha uhusiano madhubuti wa kisiasa, kiuchumi na kitamaduni sio tu na Iran, bali pia na Syria,Jordan na mataifa mengine ya Kiarabu katika kanda hiyo. Deger Akal wa Deutsche Welle alizungumza na wataalamu wakuu nchini Uturuki, kupata ufafanuzi wa kina, juu ya sera hiyo mpya ya Uturuki.

Sera hiyo mpya ya kigeni ya chama tawala cha AKP chenye mizizi ya Kiislam imepokewa kwa shauku na mashaka na serikali za mataifa ya Magharibi. Je, Uturuki inaziba pengo lililoachwa wazi na mataifa ya Magharibi, hatua ambayo itasaidia sana kuleta usalama na utulivu katika kanda hiyo? Au Uturuki inataka kuchukua hatua za mbadala, wakati uwezekano wa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya unaonekana kuzidi kuzorota?

Mmojawapo wa waandishi habari wa Kituruki mwenye uzoefu mkubwa katika kanda hiyo,Cengiz Candar, ni muungaji mkono mkubwa wa dhima mpya ya Uturuki katika Mashariki ya Kati. Anaamini kwamba serikali ya Uturuki haiendi kinyume na maslahi ya mataifa ya Magharibi.

"Kile inachofanya Uturuki nchini Iraq na Syria, ni kuwasiliana na makundi ambayo sio ya serikali kama vile, Hamas na Hizbollah. Kwa kweli, ni kukatiza ushawishi wa Iran ili isieneze ushawishi wake katika eneo hilo, ambao inataka kuutumia vibaya kwa malumbano na mataifa ya magharibi."

Mwandishi huyo anatumai kwamba kile inachofanya Uturuki, ni kile kiilichoyashinda mataifa ya Magharibi na inafanya hivyo kwa maslahi yao wenyewe.

Ikiwa ni nchi yenye Waislamu wengi na iliyo mwanachama wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO, Uturuki kwa muda mrefu, imekuwa rafiki mtiifu wa Marekani na imetimiza dhima kubwa katika usalama wa mataifa ya Magharibi. Kwa zaidi ya miaka 50 ilijiepusha na kujihusisha sana na masuala ya Mashariki ya Kati na badala yake kuwa na msimamo wa hadhari ambao uliifungamanisha nchi hiyo na marafiki zake wa Magharibi.

Hata hivyo, miaka michache iliopita kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sera ya Uturuki kwa Mashariki ya Kati kwa kuwa huru na kujishughulisha zaidi. Kutokana na uchumi wake kukua kwa haraka na kuzidi kujiamini, Uturuki inapigania kuongoza harakati za kidiplomasia.Sio tu inataka kutokomeza kabisa matatizo na majirani zake, bali pia kuungana nao kama alivyosisitiza Waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Profesa Ahmet Davutoglu .

Sera mpya ya Uturuki kwa Mashariki ya Kati imebuniwa na chama tawala cha AKP na mmojawapo wa wakuu wa itikadi hiyo Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki. Chama cha AKP kina mizizi yake katika siasa za Uislamu lakini kinakanusha madai kwamba ni chama cha itikadi kali za Kiislam. Kinajieleza kuwa ni chama cha kidemeokrasi ya kihafidhina. Hata hivyo, mtaalamu wa sera za kigeni Semih Idiz, anaelezea pengo lilioko katika harakati hizo kubwa za kidiplomasia za Uturuki na hali halisi ya mambo.

"Katika suala la Iran, tulitengwa kwenye Umoja wa Mataifa. Kuhusu suala la Iran na Israel, uhusiano wetu na mshirika wetu mkuu, umekuwa ukiyumba. Hivi sasa inahitajika kazi kubwa, kurekebisha hali hiyo."

Kuzidi kujihusisha kwa serikali ya Uturuki kwa masuala ya Mashariki ya Kati,kuunga mkono kundi la Hamas na kupinga kwake vikwazo dhidi ya Iran, kumesababisha mvutano kati yake na Marekani, halikadhalika na Israel.

Mwandishi:Akal.Deger/ZPR/P.Martin

Mhariri: M.Dahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com