1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dadaab: Nini Ujerumani inajifunza kwa Kenya?

11 Septemba 2015

Ujerumani inakabiliwa na changamoto kubwa ya wakimbizi, lakini kambi kubwa zaidi ya wakimbizi Afrika iko nchini Kenya. Mwandishi wetu Antje Passenheim, anaeleza uzoefu wa Kenya wa kushughulikia idadi kubwa ya wakimbizi.

https://p.dw.com/p/1GUvu
Flüchtlingslager Dadaab Kenia
Picha: AP

Ujerumani iko katika hekeheka za kuwashughulikia maelfu ya wakimbizi. Wakaazi wa mji mkuu wa Kenya Nairobi wanafuatilia kwa shauku kubwa, namna Wajerumani wanavyoushughulikia mmiminiko huo mkubwa wa watu wanaotafuta msaada. Waandishi wa Kijerumani wamekuwa wakienda nchini Kenya kuripoti juu ya kambi kubwa zaidi ya wakimbizi Afrika mashariki. Na sasa Ujerumani imo katika mazingira sawa, hata mwanafunzi Mike amelibaini hilo.

"Nimesikia katika taarifa za habari, kwamba Kansela Merkel amelipigia kelele suala hilo, akisema yatupasa kuwasaidia wakimbizi,hatupaswi kuwafukuza na tunahitaji kuwa wavumilivu", anasema mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17.

Mike ameguswa na ukweli kwamba Ujerumani imeamua kuwasaidia mamia ya maelfu ya watu walioko njipanda, na kuwataka majirani za Ujerumani kuiga mfano pia. "Tunafahamu vizuri ni namna gani Wajerumani wanahisi kwa sababu hata sisi tunaishi na idadi kubwa ya wakimbizi."

Kansela Angela Merkel akipiga picha na mkimbizi kutoka Syria.
Kansela Angela Merkel akipiga "selfie" na mkimbizi kutoka Syria.Picha: Reuters/F. Bensch


Muhimu ni kuvumiliana

Shule ya bweni ya Mike iko katika eneo la Eastleigh la mjini Nairobi - ambalo linafahamika pia kama "Mogadishu ndogo." Eastleigh ni kitongoji kinachokumbwa na ghasia za mara kwa mara. Wakenya wengi huingia Eastleigh kwa kusita sita.

Kitongoji hicho ndiyo eneo kuu la biashara kwa raia wa Somalia walioko uhamishoni nchini Kenya. Kuanzia nyama ya ngamia hadi kwenye silaha aina ya Kalashanikov, karibu kila kitu kinapatikana katika eneo hilo. Maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wameifanya Eastleigh kuwa nyumbani kwao.

Mike anasema jambo muhimu ni kuvumiliana. "Jirani yangu wa nyumbani ni mkimbizi na mimi na yeye tunaishi kama ndugu na simuangalii vibaya na wala simshushi hadhi kwa sababu yeye ni mkimbizi na wala halikuwa kosa lake kwamba waliondoka nchini kwao. kwa hivyo muhimu ni kuvumiliana."

Hata Victor Ithiongo, dereva wa studio za shirika la utangazaji la umma la Ujerumani ARD mjini Nairbi, anashangazwa inakuwaje kuna mataifa barani Ulaya yanayokataa kuwapokea wakimbizi.

"Sidhani kama wanawatendea vyema kwa sababu wameanza kujenga kuta ambazo wakimbizi hawaezi kuzipenya," anasema.

Ikiwa Kenya, nchi maskini sana inaweza kuchukuwa wakimbizi karibu laki sita na nusu kutoka mataifa jirani yanayokabiliwa na migogoro ya kivita kwa msaada wa kimataifa, kwa nini basi mataifa yalisostawi vizuri zaidi barani Ulaya yashindwe? anauliza Ithiongo.

Anafahamu kwamba ipo hofu kwa watu wanaotokea mataifa yenye uhasama, lakini anasema suala la muhimu ni kuwafamisha sheria za kuzingatia wanapokuwa katika mazingira ya ukimbizi. "Kambi ya wakimbizi ni kama shule, hivyo lazima kuwepo na sheria."

Wakimbizi wa Kisoamali wakiwa katika kambi ya Dadaab.
Wakimbizi wa Kisoamali wakiwa katika kambi ya Dadaab.Picha: Oli Scarff/Getty Images


Siyo yote yafaa kuingwa

Lakini mtalaamu wa uchumi wa Kenya Kwame Owino kutoka taasisi ya ushauri ya masuala ya kiuchumi, anasema Ujerumani lipo suala muhimu ambalo Ujerumani haipaswi kuiga mfano wa Kenya. "Hata ukiruhusu wakimbizi wengi zaidi kuingia, kuwaweka watu katika makambi siyo njia nzuri ya kuwashirikisha katika jamii."

Afrika kama ilivyo kwa Ulaya, ukiwawezesha wakimbizi kuingia katika soko la ajira, wanaweza kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi. Katika makala ya maoni aliyoiandikia gazeti kubwa la kila siku la Nation, Owino aliisifu hatua ya Ujerumani kukubali kuchukuwa maelfu ya wakimbizi kuwa ndiyo ya kishujaa zaidi tangu kuungana tena kwa Ujerumani mbili miaka 25 iliyopita.

Hatua hiyo imepandisha taswira ya Ujerumani barani Afrika, anasema Owino, kwa sababu ilikuwa imepata madoa kutokana na malumbano yaliyofuatia mgogoro wa madeni wa Ugiriki. Nchini Kenya watu wana taswira ya Ujerumani kama nchi inayochukia sana wageni.

"Mgogoro huu wa wakimbizi umetoa fursa kwa Ujerumani na Wajerumani kujisafisha machoni pa watu, tunajua haya ni maamuzi magumu kisiasa lakini tunapotafakari vizuri na kuchanganua zipi chaguo za kimaadili bila shaka tutafanya maamuzi sahihi," aliadika mtaalamu huyo wa masuala ya kiuchumi.

Mwandishi: Antje Passenheim

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Josephat Charo