1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Mamilioni waamriwa kusalia nyumbani

Angela Mdungu
21 Machi 2020

Mamilioni ya watu duniani wameuanza mwisho wa juma wakiwa wameamriwa kusalia majumbani mwao kutokana na janga la virusi vya Corona wakati idadi ya vifo ikiendelea kupanda

https://p.dw.com/p/3Zpnw
Mitaa mitupu jimboni Carlifonia baada ya agizo la kutotoka nje
Picha: Getty Images/AFP/J. Edelson

Hatua za kuwataka raia kubaki kwenye makazi yao zinachukuliwa na mataifa malimbali huku idadi ya vifo vinavyotokana na virusi vya Corona duniani kote ikiwa imefikia 11,000. Italia inaongoza kwa vifo vingi zaidi ikiwa na takribani vifo 4,000. Idadi ya vifo nchini humo kwa siku imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika wiki moja iliyopita. Wengi wa wanaoripotiwa kufa kutokana na maambukizi ni wazee na watu wenye matatizo ya kiafya.

Licha ya makundi hayo kuwa hatarini zaidi, shirika la afya duniani WHO, limetoa onyo kwa vijana kuwa virusi hivyo vinaweza pia kuwapata. Kauli hiyo ya WHO imetolewa na mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Tedros Adhanom Ghebreyesus ambapo amewaambia vijana kuwa virusi vya Corona vinaweza kuwadhuru na kuwaweka hospitalini kwa muda mrefu na hata kusababisha kifo. 

Mlipuko wa virusi hivyo umeyabadilisha maisha ya watu kote ulimwenguni kwa haraka kutokana na kudhibitiwa kwa mienendo ya makundi makubwa, shule na biashara kufungwa na kuwalazimu mamilioni ya watu kufanya kazi kutokea majumbani wakati wengine wakipoteza njia za kujipatia riziki zao.

Huko Marekani wakati Rais wa Marekani Donald Trump akitangaza kushinda vita dhidi ya virusi vya Corona, baadhi ya majimbo nchini humo yakiwemo New York na illinois yameungana na jimbo la California kuwaamuru wakaazi wake kusalia nyumbani.

Katika hatua nyingine, China hii leo, haijaripoti kisa chochote cha maambukizi mapya ikiwa ni siku ya tatu mfululizo. Shirika la Afya duniani WHO limesema pia kuwa mji wa Wuhan ambao ni chimbuko la virusi hivyo, umeonesha matumaini kwa nchi nyingine ulimwenguni. Hata hivyo kuna wasiwasi mkubwa  juu ya wimbi jipya la virusi hivyo katika mji wa Hong Kong ambapo hadi jana Ijumaa kulikuwa kunakadiriwa kuwa na visa 48. Hiyo ni idadi kubwa zaidi iliyorekodiwa ndani ya siku moja tangu kuanza kwa janga hilo. Wengi wa watu waliogunduliwa kuwa na maambukizi hayo mjini humo walikuwa wakitokea safarini barani Ulaya.

Roma- Italia
Moja ya maeneo maarufu yanayofurika watu mjini Rome yanavyoonekana sasa aada ya amri ya kusalia nyumbani Picha: Reuters/R. Casilli

Kwingineko barani Ulaya serikali zimeendelea kuchukua hatua za kuwataka watu kusalia majumbani. Mbali na Italia kutoa agizo la watu kubaki nyumbani, Ufaransa, Uhispania na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya yamewaambia pia raia wake kusalia nyumbani huku watakaokiuka maagizo hayo wakiamriwa kulipa faini. Kwa upande wa Ujerumani, jimbo la Bavaria limekuwa la kwanza kuwaamuru watu wake kusalia majumbani.  Uingereza, yenyewe ilitangaza hatua kali kwa kufunga migahawa na baa huku ikiahidi kusaidia kuwalipa mishahara wafanyakazi walioathiriwa.

Nalo bara la Afika limerekodi takribani visa 1000 vya maambukizi ya virusi vya corona. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la kimataifa la AP. Hadi sasa idadi ya vifo imefikia 17 barani humo. Kuna hofu kwamba mifumo duni ya afya ya katika mataifa barani humo italemewa kwa haraka na mlipuko wa virusi hivyo.