Clinton akutana na viongozi wa Israel na Palestina mjini Washington | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Clinton akutana na viongozi wa Israel na Palestina mjini Washington

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amekutana na viongozi wa Israel na wa Palestina mjini Washington, Marekani. Mkutano umegubikwa na mauaji ya Waisraeli wanne katika eneo la Ukingo wa Magahribi

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Hillary Clinton

Kuwasili kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu mjini Washington kulifuatiwa na taarifa za kupigwa risasi na kuuwawa Waisraeli wanne, wanaume wawili na wanawake wawili, mmoja mjamzito, katika makaazi ya walowezi ya Kiyahudi ya Kiryat Arba karibu na mji wa Hebron. Waisraeli hao walipigwa risasi walipokuwa ndani ya gari katika shambulio ambalo kitengo cha kundi la Hamas cha wapiganaji wa Ezzedine al Qassam, kimedai kuhusika.

Msemaji wa jeshi la Israel Leibovitch, Avital, amesema,"Tunafahamu motokaa hiyo ni ya Israel na ilikuwa na watu wanne ndani. Ilifyetuliwa risasi ilipokuwa barabarani na raia hao wakauwawa. Naweza kuthibitisha kuwa mmoja wao alikuwa mama mjamzito. Tunaliona shambulio hili kuwa hatari na baya kabisa."

Jeshi la Israel limeyafunga baadhi ya maeneo ya Ukingo wa magharibi, huku maafisa wa usalama wa Palestina wakisema wamewatia mbaroni watu 50 kufuatia kuuliwa kwa Waisraeli hao. Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa mjini Jerusalem,Robert Serry, amesema ameshtushwa na mauaji hayo na kuhimiza yasiruhusiwe kuwatatiza viongozi wa Israel na Palestina wanaotaka kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake rais Abbas amelilaani shambulio hilo akisema lilinuiwa kuvuruga mchakato wa amani.

Mahmoud Abbas, Mahmud Abbas PLO Treffen

Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas

Ikulu ya Marekani imetoa taarifa kulaani mauaji ya walowezi hao wanne wa Kiyahudi na kutoa mwito yasitumike kuvuruga mazungumzo ya amani.

Akizungumza kabla kuanza mashauriano na waziri mkuu Netanyahu, Bi Clinton amesema ukatili wa aina hiyo hauna nafasi katika taifa lolote chini ya mazingira yoyote yale. "Nguvu za ugaidi na uharibifu haziwezi kuruhusiwa kuendelea. Hii ni mojawapo ya sababu kwa nini waziri mkuu amekuja hapa leo, kushiriki mazungumzo ya ana kwa ana na Wapalestina ambao wamekataa njia ya machafuko na badala yake kuchagua njia ya amani," ameongeza kusema waziri Clinton.

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema atasisitiza kwenye mazungumzo ya ana kwa ana na rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas kwamba mipango kuhusu usalama katika makubaliano yoyote ya mwisho ya amani itaisaidia Israel kupambana na ugaidi wa aina hiyo na vitisho vyengine. "Hatutaruhusu ugaidi kuamua ni wapi Waisraeli wanakotakiwa kuishi wala mipaka ya mwisho ya taifa letu. Masuala haya pamoja na mengine yatatathminiwa kwenye mashauriano ya amani tunayoyafanya," amesema waziri mkuu Netanyahu.

Benjamin Netanjahu wird Außenminister Israels

Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu

Rais wa Marekani Barack Obama anapanga kufanya mikutano na kuwaalika kwa chakula cha jioni waziri mkuu Netanyahu na rais Abbas, pamoja na mfalme Abdullah wa Jordan na rais wa Misri, Hosni Mubarak, hivyo kupanua mdahalo kuhusu amani ya Mashariki ya Kati kuwajumulisha majirani wawili wa Kiarabu wenye ushawishi mkubwa na ambao tayari walisaini mikataba ya amani na Israel. Mauaji ya Waisraeli wanne huenda yakatawala ajenda ya mkutano huo.

Waziri mkuu Netanyahu pamoja na rais Abbas wanatarajiwa kuanza rasmi mazungumzo ya ana kwa ana hapo kesho katika wizara ya mambo ya ndani ya Marekani, hivyo kuuanzisha tena mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati huku kukiwa na wasiwasi kama kweli juhudi za sasa zitafua dafu kuweza kufikia amani ya kudumu baina ya Israel na Wapalestina.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/AFPE

Mhariri: Mwadzaya, Thelma

 • Tarehe 01.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P1Qt
 • Tarehe 01.09.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/P1Qt
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com