Chaguzi katika nyakati za virusi vya corona | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Chaguzi katika nyakati za virusi vya corona

Mripuko wa virusi vya corona ukiwa unazidi kuutikisa ulimwenguni, Ujerumni na Ufaransa zimeendelea na chaguzi huku marufuku za kubakia majumbani zikizidi kutangazwa katika mataifa mbalimbali.

Licha ya kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona kote nchini Ujerumani, uchaguzi wa jimbo la Bavaria kusini mwa nchi hiyo unafanyika kama ulivyopangwa.

Takriban watu milioni kumi wanastahili kushiriki katika uchaguzi huo wa jimbo unaofanyika kwenye vituo 4,000 tofauti kuwania nafasi 40,000 za uongozi katika halmashauri za miji na manispaa

Nafasi za umeya zitachaguliwa katika miji 24 kati ya 25 ya jimbo la Bavaria, ikiwa ni pamoja  na Munich, Nuremberg na Augsburg. Hata hivyo, uamuzi juu ya nafasi za ngazi ya juu hautatolewa hadi kutakapofanyika duru nyingine ya uchaguzi, mnamo Machi 29.

Vituo hivyo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa saa kumi na mbili jioni Jumapili, huku matokeo ya awali yakitarajiwa kutolewa baadae jioni na matokeo kamili siku ya pili Jumatatu.

Hadi Jumamosi jioni, Taasisi ya Ujerumani ya Afya, Robert Koch, imeripoti visa 3,800 vilivyothibitishwa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo, na vifo vinane.

Kommunalwahl in Bayern

Uchaguzi katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria, Munich - 15.03.2020

Bavaria yaathirika zaidi

Bavaria ni moja wapo ya majimbo yaliyoathirika vibaya na maambukizi hayo nchini Ujerumani, ambapo kumeripotiwa visa vya maambukizi vipatavyo 680 na kifo kimoja.

Aidha mipaka kati ya Ujerumani na mataifa ya Uswisi, Austria na Ufaransa itafungwa kuanzia Jumatatu asubuhi, kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kulingana na jarida la habari la Ujerumani la Spiegel pamoja na gazeti la Bild. Hata hivyo, mamlaka za Ujerumani zitaruhusu wale wanaovuka mipaka kwa ajili ya kazi kila siku pamoja na uingizaji wa bidhaa. Hakuna taarifa juu ya iwapo Ujerumani inalenga kuifunga pia mipaka mingine ikiwemo kati yake na Poland, Uholanzi, Denmark na Jamhuri ya Czech.

Shule kote Ujerumani zimefungwa kwa wiki kadhaa zijazo, na hafla za umma zimefutwa kama sehemu ya juhudi za kupunguza kusambaa kwa maambukizi hayo ya maradhi ya COVID-19.

Mamlaka ya mji mkuu wa Ujerumani, Berlin na ya jiji la Cologne katika jimbo la North Rhine Westfalia  zimetangaza kufungwa baa, vilabu vya starehe, majumba ya sinema na kumbi za matamasha wakati ambapo Ujerumani inaongeza juhudi za kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi hivyo vya corona. Kuanzia sasa hafla yoyote inayowahusisha watu 50 au zaidi katika mji wa Berlin imepigwa marufuku.

Ufaransa nayo pia imetangaza kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa utaendelea kama ulivyopangwa kufanyika Jumapili, huku ikiwa imeamrisha kufungwa kwa mikahawa, vilabu, kumbi za cinema na muziki lakini imesema maduka ya chakula, dawa na benki zitasalia wazi.

Watu 196 wameshafariki kwa virusi vya corona Uhispania

Uhispania Jumapili pia imetangaza marufuku kadhaa katika juhudi zake za kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona.

Ikichukua hatua sawa na Italia, Uhispania imeweka marufuku ya karibu nchi nzima inayowazuia watu kuondoka majumbani isipokuwa kwa lengo la kwenda kazini, kutafuta matibabu au kununua chakula.

Maradhi ya COVID-19 tayari yamesababisha vifo vya watu 196 nchini Uhisapania na kulifanya kuwa taifa lililoathiriwa zaidi na virusi hivyo barani Ulaya baada ya Italia.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez na mkewe ni miongoni mwa watu walioambukizwa virusi vya corona.

Spanien | Regierung verhängt Ausgangssperre

Tangazo barabarani mjini Barcelona, Uhispania; 'Kaa nyumbani, upunguze maambukizi ya virusi vya corona.'

Taarifa iliyotolewa Jumapili na Makao Makuu ya Kanisa Katoliki mjini Vatican imesema sherehe za kitamaduni za wiki ya pasaka hazitohudhuriwa na waumini kutokana na kitisho cha virusi vya corona.

Idara katika ofisi ya kiongozi mkuu wa kanisa katoliki imesema kutokana na dharura ya kiafya duniani, sherehe zinazofahamika pia kama "Liturujia ya wiki takatifu" ya pasaka itafanyika bila ya kuwepo makundi ya watu.

Vatican pia imesema mikusanyiko ya watu na sala ya Malaika wa Bwana ambayo huongozwa na papa Francis itafanyika kwa njia ya mtandao hadi April 12.

Kesi ya rushwa dhidi ya Netanyahu yaahirihswa

Kwa upande wa Mashariki ya Kati, kesi ya rushwa inayomkabili waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imeahirishwa Jumapili kwa muda wa miezi miwili kutoka na taharuki ya kusambaa kwa virusi vya corona.

Waziri wa sheria wa Israel amesema kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa Machi 17 kwa kusomwa mashtaka matatu ya rushwa dhidi ya Netanyahu imesogezwa mbele hadi Mei 24.

BdT | Iran Feuerwehmänner desinfizieren die Straße in Teheran

Wazima moto Iran wapuliza dawa kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona katika barabara za mji mkuu Tehran - Machi 13, 2020.

Afisa wa Iran anayeongoza juhudi za kupambana na ugonjwa wa COVID-19 nchini humo amekiri Jumapili kwamba huduma ya afya nchini mwake inaweza kuelemewa kutokana na maradhi hayo.

Iran ni nchi iliyoathiriwa zaidi na virusi vya corona Mashariki ya Kati huku ikiwa chini ya vikwazo vikali vya kiuchumi ilivyowekewa na Marekani.

Iran pia imeripoti vifo vipya 113 kutokana na virusi hivyo, na kuifanya idadi jumla kufika vifo 724.

Barani Asia, Sri Lanka nayo Jumapili imepiga marufuku mikusanyiko ya umma na binafsi na kuweka hatua kadhaa za karantini katika juhudi zake za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Hayo ni kulingana na msemaji wa polisi ya taifa ambaye pia amearifu kuwa erikali ya Sri Lanka imetangaza kesho Jumatatu kuwa likizo ya umma ili kusaidia kutekeleza hatua za karantini.

Hadi sasa visa kumi vya maradhi ya COVID-19 vimethibitshwa nchini humo na zaidi ya watu 100 wameonyesha dalili za kupata maambukizi ya virusi vya corona.

Virusi vya corona tayari vimewakumba watu 158,465 kote ulimwenguni na kusababisha vifo 5,838 kulingana na takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la Reuters.

Vyanzo: (afp, dpa, rtre, ap)