Bunge la Afrika lakabiliwa na changamoto kubwa. | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Bunge la Afrika lakabiliwa na changamoto kubwa.

Ukosefu wa fedha ni moja ya vikwazo vya utendaji .

Makamu wa rais wa Ghana John Mahama ameuambia mkutano wa wabunge wa bunge la Afrika mjini Midrand Afrika kusini kwamba itakua bado ni vigumu kwa Afrika kukabiliana na athari za msukosuko wa kiuchumi duniani au kuyatatua matatizo mengine barani humo, ikiwa nchi za bara hilo zitataka kuchukua hatua peke yao.

Akihutubia kikao cha 11 cha bunge hilo la Afrika, Bw Mahama alisema maendeleo ya miradi ya pamoja ya bara hilo yamekua ni ya taratibu mno. Makamu huyo wa rais wa Ghana alisema nchi za kiafrika zimekuwa zikinga´ngania bendera na nyimbo zao za taifa, bila ya kuona umuhimu wa kuwa na Afrika ilioungana zaidi. Akasisitiza kwamba kile ambacho Afrika inataka ni heshima na utu kama waafrika.

Bunge la Afrika liliundwa 2004 kama chombo kimoja wapo cha Umoja wa Afrika, lakini shughuli zake tangu wakati huo zimekua hazionekani kuwa na uzito wowote. Serikali zimeshindwa kuliunga mkono bunge hilo kwa sababu ya wasi wasi linaweza kuweka utaratibu imara kuhusu suala la kuwajibika , kuliko yalivyo mabunge ya kitaifa.

Viongozi wa taasisi hiyo wanasema shughuli zake zimeathirika kutokana na ukosefu wa nyenzo. Miongoni mwa changamoto kubwa zilizotajwa na spika wa bunge hilo bibi Getrude Mongella wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho ni fedha pamoja na uwezo wa watumishi na wa kiufundi.

Changamoto upande wa fedha inayolikabili bunge la Afrika, iligeuka kuwa kubwa pale umoja wa Afrika ulipopunguza nusu ya bajeti yake.Kutokana na hayo bunge la Afrika likashindwa hata kutuma watazamaji katika uchaguzi wa karibuni nchini Afrika kusini na Algeria.

Kikubwa katika ajenda ya kikao hicho kitakachoendelea hadi tarehe 29 ya mwezi huu wa Mei ni mjadala kuhusu itifaki ya kuundwa bunge hilo la Afrika pamoja na msukosuko wa kiuchumi duniani ambao unaendelea kuziathiri sana nchi zinazoendelea duniani. Kupitishwa kwa itifaki hiyo kunatarajiwa kukipa sura zaidi chombo hicho machoni mwa wakaazi wa bara hilo.

Aidha wabunge watajadiliana pia jinsi kuimarishwa ushirikiano barani humo kunavyoweza kuzipa nguvu juhudi za kukabiliana na matatizo kama vile uchaguzi huru na wa haki au kuhama kwa watu wenye ujuzi na vijana kujitafuitia maisha bora nchi za nje.Spika Mongella amesema kuna haja ya kubadilishana fikra na kushirikiana ili bara hilo liweze kupiga hatua mbele.

Akaongeza ," Wakati tunayajadili masuala haya muhimu, tunafahamu kwamba halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika imo katika jitihada za kuleta mabadiliko, na kwa kuwa chombo hiki kinaratibu shughuli za vyombo vyengine vya Umoja wa Afrika, tunafikiri mabadiliko yake yatakua na ushawishi mkubwa kwa mabadiliko katika nyanja nyengine."

Makamu wa Rais wa Ghana Bw Mahama alisema kwa upande mwengine kuwa kilimo ni uwezekano mmoja wapo wa kulikwamua bara la Afrika katika wakati dunia ikikabiliwa na msukosuko wa fedha. Alisema mabilioni ya dola yanatumiwa kuagiza chakula kutoka nje kila mwaka, wakati fedha hizo zingeweza kuwekwa akiba kama nchi hizo zingeimarisha shughuli za kilimo.

Akasema kuna haja kubwa ya kuwasaidia wakulima kuingia katika kilimo cha kisasa ili waweze kuongeza mavuno na kuwa na uwezo wa kulilisha bara hilo.

Mwandishi: Mohamed Abdul-Rahman/IPS

Mhariri:Abdul Mtullya

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com