Boris Johnson aenda Ufaransa baada ya kukutana na Merkel | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.08.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Boris Johnson aenda Ufaransa baada ya kukutana na Merkel

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anaizuru Ufaransa Alhamisi, siku moja baada ya Kansela Angela Merkel kumpa matumaini ya kufikia muafaka kuhusu mchakato wa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

Katika mkutano wake na Merkel siku ya Jumatano, viongozi hao walisema wanataka kuepusha Brexit bila makubaliano, ingawa wanatofautiana juu ya namna ya kufanikisha suala hilo. Lakini Johnson huenda akakumbana na hadhira ngumu zaidi mjini Paris kuliko ilivyokuwa Berlin.

Siku ya Jumatano rais Macron alitupilia mbalia mapendekezo ya Johnson kuutaka Umoja wa Ulaya kufungua tena majadiliano kuhusu mpaka wa Ireland, akisema kanda hiyo imeweka wazi wakati wote kwamba haitakubali hilo, na aliwaambia waandishi habari mjini Paris kwamba mapendekezo ya Uingereza kujadili upya vipengele vya mkataba ni suala lisilokuwepo.

Mwishoni mwa wiki viongozi hao watatu wa Ulaya watakutana na Rais wa Marekani Donald Trump, muungaji mkono mkubwa wa Brexit na Johnson, pamoja na viongozi wa Canada, Italia na Japan kwenye mkutano wa kilele wa mataifa saba yalioendelea zaidi duniani G7, katika mji wa mapumziko wa Biarritz nchini Ufaransa.

Berlin, Angela Merkel trifft Boris Johnson (Reuters/A. Hilse)

Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson wakikutana katika ofisi ya kansela mjini Berlin, Agosti 21, 2019.

Mazungumzo hayo yanakuja baada ya Merkel kumuambia Johnson siku ya Jumatano kwamba makubaliano yanaweza kufikiwa ndani ya siku 30, ikiwa suluhisho litapatikana kuhusu suala gumu la mpaka wa Ireland.

"Kuna masuala mawili ambayo yote ni muhimu: Moja ni, Uingereza inataka kuondoka Umoja wa Ulaya. Lingine ni kwamba makubaliano ya Good Friday laazima yazingatiwe. Hii halitoki Uingereza pekee, bali pia mwanachama wa Umoja wa Ulaya Ireland," alisema Merkel na kuongeza kuwa, "hilo ni sehemu ya msimamo wetu wa Umoja wa Ulaya, na sasa tunapaswa kuileta misimamo hiyo pamoja."

Mkwamo kuhusu suala la mpaka wa Ireland
 

Waziri mkuu huyo wa Uingereza amekuwa akisitiza kwamba hatokubali mpango wa mpaka uliokubaliwa na mtangulizi wake Theresa May na ameonya kuwa Uingereza itandoka Umoja wa Ulaya Oktoba 31, hata ikiwa hilo litasababisha machafuko ya kiuchumi.

"Sisi nchini Uingereza tunataka makubaliano, tunatafuta makubaliano, na naamini tunaweza kuyapata. Lakini hatuwezi kuyakubali makubaliano ya sasa ya kujiondoa," alisema Johnson katika mkutano na Merkel mjini Berlin.

Frankreich Präsident Emmanuel Macron speaks at the residence of French Defense Minister on the eve of Bastille Day in Paris (Reuters/K. Zihnioglu)

Rais Emmanul Macron tayari ameonyesha kupinga mapendekezo ya Uingereza kujadili upya makubaliano ya Brexit.

Mjini Berlin, Johnson alisisitiza mtazamo wake kwamba mpango huo wa mpaka wa Ireland una madhara makubwa kwa nchi huru na ya kidemokrasia kama Uingereza, na kusisitiza kwamba kipengele hicho laazima kiondolewe.

Merkel alisema mpango huo ndiyo njia pekee ya kulinda soko la pamoja katika kipindi ambamo mataifa mengine 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya na London watakuwa wanajadili uhusiano wao wa baadae.

Katika kutafuta suluhisho, alisema yumkini watalipata katika kipindi cha miaka mwili ijayo, lakini akaongeza kuwa inawezekana pia likapatikana ndani ya siku 30.

Johnson katika kile kinachoweza kuelezwa kama kamari ya kufa na kupona, amesisitiza kuwa Uingereza itaondoka Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31, bila kujali imesuluhisha tofauti zinazobakia na kanda hiyo au la.

Vyanzo: Mashirika

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com