1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama UN kuamua kuhusu marufuku ya silaha Iran

Rashid Chilumba14 Agosti 2020

Marekani imewasilisha pendekezo mbele ya baraza la usalama Usalama la Umoja wa Mataifa la kurefusha bila kikomo vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ikisema hatua hiyo itakomesha ufedhuli wa Jamhuri hiyo ya Kiislam.

https://p.dw.com/p/3gzLc
UN-Sicherheitsrat New York 2016 | Waffenembargo Libyen
Picha: Imago Images/Xinhua

Duru kutoka makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York zimearifu kuwa Marekani imewasilisha pendekezo hilo ili kurefusha muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran ambao unakaribia kumalizika.

Wajumbe wengine wa baraza hilo la usalama lenye wanachama 15 watakuwa na muda wa hadi mwisho wa siku ya leo kuwasilisha maoni yao kuhusu pendekezo la Marekani.

Soma zaidi Urusi yatetea uzinduzi wa satelaiti wa Iran

Hata hivyo kulingana na wanadiplomasia hatua hiyo ya Marekani inatarajiwa kushindwa na huenda ikauweka rehani mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu ambao tayari utekelezaji wake unasuasua.

Marufuku iliyowekwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015 ya kuingiza au kuuza silaha zote za kivita kwa Iran inatarajiwa kufikia mwisho Oktoba 18 mwaka huu.

US-Präsident Trump
Rais Donald Trump akiwa na wasaidzi wake katika ikulu ya White House, akiwemo mjumbe maalumu kwa Iran Brian Hook.Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Harnik

Pendekezo jipya lililowasilishwa na Marekani linataka vikwazo hivyo kurefushwa bila ya kikomo ikisema iwapo vitaondolewa, Iran itakuwa msambazaji wa silaha bila kuzingatia maadili ya kimataifa.

Iran yaonya kuchukuwa hatua

Rais wa Iran Hassan Rouhani ameonya kuwa nchi yake itajibu iwapo Baraza la Usalama litarefusha vikwazo hivyo vya silaha lakini hakuainisha hatua watakazochukua.

Soma zaidi Iran yaonya kuhusu jitihada ya kuongezewa vikwazo

Kwa upande wake waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amesema Baraza la Usalama linapaswa kuiwajibisha Iran kwa kurefusha marufuku ya silaha.

Tayari China na Urusi, wanachama wawili wa Baraza la Usalama wenye kura ya turufu wameshatangaza kupinga jitihada hiyo ya Marekani dhidi ya Iran.

Soma pia Iran yakiri kituo cha Natanz kimeharibiwa kwa moto

Iwapo pendekezo hilo litashindwa, Marekani imetishia kutengua kipengele cha mkataba wa nyuklia kinachoruhusu washirika wa mkataba huo kuutuhumu upande mwingine kwa kutotekeleza masharti ya mkataba.

Iran Militärübung Revolutionsgarden mit Raketen
Mazoezi ya kijeshi ya Iran.Picha: picture-alliance/dpa/AP/Sepahnews

Pindi hilo litatokea, vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vitarejeshwa.

Kuna wasiwasi juhudi hizo mpya za Marekani huenda zitauvuruga mkataba wa Vienna uliolenga kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia kwa ahadi ya kuondolewa vikwazo vikali vya kiuchumi.

Soma pia Iran yazindua makombora ya chini ya ardhini

Hata hivyo wafuatiliaji wa suala hilo wamesema Marekani haina haki ya kutumia kipengele hicho kwa sababu rais Donald Trump aliiondoa nchi yake kutoka mkataba wa nyuklia na Iran mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo la kiislamu.

Makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran, Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani yalianza kuyumbayumba baada ya Marekani kujitoa na Tehran kuanza kukiuka vipengele vya mkataba.

Chanzo: Mashirika