Iran yaonya kuhusu jitihada ya kuongezewa vikwazo | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Iran yaonya kuhusu jitihada ya kuongezewa vikwazo

Iran yaonya kuhusu jitihada ya kuongezewa vikwazo

Balozi wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa amesema anaamini kuwa azimio la Marekani kuongeza muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya nchi yake litashindwa.

Huku balozi huyo akionya kuwa litakuwa kosa kubwa sana ikiwa utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani utajaribu kurejesha vikwazo hivyo vya Umoja wa Mataifa kwa taifa lake.

Balozi Majid Ravanchi alisema hapo jana kwamba kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa vitaumalizika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa makubwa na kuiondowa nchi yake kwenye wajibu wa kutekeleza ahadi zake katika mkataba huo. Kuiondolea Iran vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa ni moja ya vipengele vya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilioidhinisha makubaliano hayo.

Ravanchi alizungumza siku moja baaa ya Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo, kutishia kuwa ataomba kurejeshwa upya kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa Iran ikiwa baraza hilo la usalama halitaidhinisha azimio jengine la kuongeza vikwazo kwa muda usiojulikana, muda ambao ulikuwa unamalizika Oktoba mwaka huu.

Pompeo atahadharisha kuhusu hatari ya Iran kuweza kununua silaha

USA PK Mike Pompeo in Washington

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo

Pompeo alidai endapo muda wa sasa ukimalizika, Iran itaweza kununuwa mifumo ya silaha zenye kiwango cha juu na itaweza kuwauzia magaidi na tawala za kikatili duniani kote, jambo ambalo alisema halikubaliki. Ravanchi alisema kukomesha vikwazo vya silaha mwezi Oktoba ni sehemu muhimu sana ya makubaliano kati ya Iran na washirika wake. "Tunaamini hakuna mwenye uthubutu wa kuzungumzia azimio kama hilo linalowasilishwa na Marekani kwenye Baraza la Usalama. Kwa hivyo, tunaamini kuwa litashindwa. Hatutokubali chochote chengine zaidi ya utekelezwaji wa kipengele cha kuondowa kabisa vikwazo vya silaha.” Alisema Balozi huyo wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa, akionesha barua za mawaziri wa kigeni wa Urusi na China, wote wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, ambazo zinapinga kuongezwa kwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya nchi yake.

Juzi Jumatano, Mwakilishi Maalum wa Marekani kwa ajili ya Iran, Brian Hook, na Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Kelly Craft, walitoa taarifa mbele ya Baraza la Usalama juu ya rasimu ya azimio la nchi yao ambalo linataka vikwazo vya silaha dhidi ya Iran viendelee kwa muda usiojulikana.

Soma zaidi:Ulaya yaanza biashara ya mabadilishano na Iran

Hali ya wasiwasi baina ya Marekani na Iran imeongezeka tangu mwaka 2018, pale utawala wa Trump ulipojiondowa kwenye mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani na kurejesha upya vikwazo vyake kwa taifa hilo la Kiislamu.

Mkataba huo wa mwaka 2015, maarufu kama JCPOA, una kipengele ndani yake ambacho kinaupa Umoja wa Mataifa nguvu za kurejesha vikwazo vyote dhidi ya Iran ambavyo vilishaondoshwa au kusitishwa, endapo makubaliano hayo yamekiukwa. Kipengele hiki ndicho ambacho Marekani inataka kitumike kuirejeshea vikwazo Iran.

Hata hivyo, mataifa mengine matano yenye nguvu ambayo yalisaini mkataba huo - Urusi, China, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani - yameendelea kuuheshimu mkataba huo, yakisema kusalia kwao ni muhimu ili kulipa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani, IAEA, nafasi ya kuendelea kuikaguwa na kuizuwia Iran isiwe na silaha za nyuklia.