1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatetea uzinduzi wa satelaiti wa Iran

Tatu Karema
5 Juni 2020

Urusi inatetea haki ya Iran ya kuzindua setilaiti na kupuuza madai ya Marekani kwamba Iran inakiuka maazimio ya UN yanayoridhia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yenye ushawishi mkubwa

https://p.dw.com/p/3dHiC
USA Vassily Nebenzia
Picha: DW/A. Cama

Mjumbe wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia, amesema kuwa juhudi zinazoendelea za Marekani kuinyima Iran haki ya kufurahia manufaa ya teknologia ya amani ya angani chini ya kisingizio cha uongo ni hatua zinazoibua wasiwasi na kusikitisha. Katika barua iliyowasilishwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres na baraza la usalama la Umoja huo, Nebenzia amesema kuwa Iran haijawahi kumiliki silaha za nyuklia, wala haimiliki silaha hizo kwa sasa ama kutarajiwa kuzimiliki katika siku za usoni.

Nebenziaamepuuzilia mbali na kuzitaja kuwa '' za kupotosha'' shtuma za Marekani kwamba uzinduzi wa setilaiti wa Aprili 22 uliofanywa na jeshi la mapinduzi la Iran ulikiuka maazimio ya mwaka 2015 yalioitaka Iran kutojihusisha na shughuli zozote za makombora ambazo zingewezesha kupatikana kwa silaha za nyuklia. Nebenzia ameongeza kuwa tangu mkataba wa nyuklia wa Iran ulipopitishwa mwaka 2015 Iran limekuwa taifa lililothibitishwa zaidi na Taasisi ya kimataifa ya kawi ya atomiki na kwamba imebainishwa kuwa haimiliki wala kutengeneza  ama kutumia makombora yaliotengenezwa kuwa na uwezo wa kutengezea silaha za nyuklia.

Botschafterin Kelly Craft
Kelly Kraft- Mjumbe wa Marekani katika Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/S. Acar

Mjumbe huyo wa Urusi alikuwa akijibu barua ya mjumbe wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Kelly Craft kwa rais wa baraza la usalama la Umoja huo mwezi uliopita iliyosema kuwa mifumo ya uzinduzi wa angani inashirikisha teknologia zinazofanana na zinazoweza kubadilishwa na zile zinazotumika katika makombora yanayoweza kutengeneza silaha za nyuklia.

Craft aliongeza kusema kuwa kwa mara nyingine tena wanaihimiza jumuiya ya kimataifa kuichukulia hatua Iran kwa vitendo vyake na kwamba kuendelea kwa Iran kutengeneza teknologia yake ya makombora kunachangia kwa mvutano wa kikanda na tishio kwa amani na usalama wa kimataifa. Mvutano kati ya Iran na Marekani umeongezeka tangu serikali ya Trump ilipojiondoa katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 mnamo mwaka 2018 na kuweka tena vikwazo vyake dhidi ya Iran.

Vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba na Marekani imesambaza rasimu ya maamzimio ya Umoja wa Mataifa ambayo itaongeza kwa muda usiojulikana vikwazo hivyo kwa idadi ndogo ya wanachama wa baraza hilo mwishoni mwa mwezi Aprili.

Nebenzia amesema kuwa Urusi itapinga juhudi zozote za Marekani za kuongeza marufuku hiyo ya silaha  na kuwekwa tena kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Nebenzia ameongeza kuwa Marekani ilijiondoa katika mkataba huo na kwamba haina haki ya kutumia vifungu vyake vyovyote.