Baraza la Uchumi baina ya Ujerumani na Syria laanzishwa | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 25.02.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

IDHAA YA KISWAHILI

Baraza la Uchumi baina ya Ujerumani na Syria laanzishwa

Mwanzoni mwa wiki hii, mjini Damascus, nchini Syria, kuliasisiwa baraza la kiuchumi baina ya wafanya biashara wa nchi hiyo na wa Ujerumani.

Picha ya barabara ya Damascus nchini Syria

Picha ya barabara ya Damascus nchini Syria

Hivyo kumaanisha kuweko ushirikiano mwingi zaidi wa watu binafsi na mchache zaidi baina ya serekali na serekali. Lakini umuhimu wa baraza hilo unavuka mipaka ya uchumi. Syria inataka kuchanganyika tena na mataifa ya dunia, na ni lazima iboreshe kwa haraka hali ya maisha ya wananchi wake, ambao kwamba asilimia 30 kati yao ni maskini. Nchi za Magharibi, zikiuangalia mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati, zina hamu ya kumaliza hali ya kutengwa Syria.

Ni eneo la ujenzi mjini Damascus. Hapa zaidi yanakuja makampuni ya kigeni. Uchumi wa Syria unafungua milango yake, pia kwa Wajerumani.

"Ujerumani inafaa ifahamu kwamba nchini Syria, uchumi wa kibinafsi unazidi kuwa na umuhimu; ni kinyume na vile ilivokuwa kabla. Hivi sasa serekali inatupa mara nyingi kandarasi kubwa muhimu."

Omar Karkour ni mmoja kati ya wafanya biashara wanaoongoza nchini Syria. Yeye anaagizia magari kutoka nchi za ng'ambo, aina ya Volkswagen, Audi, Skoda na pia anafanya biashara ya vyakula. Tangu jumatatu hii anaongoza baraza la kiuchumi baina ya Ujerumani na Syria, na ambalo lina lengo la kuengeza biashara baina ya nchi hizo mbili. Kwa Karkour, Ujerumani ni mfano wa mafanikio ya kupigiwa mfano, mfano ambao unaweza kuigwa. Pia hivyo ndivyo anavosema mshauri wa kibiashara kutokea Syria, Samir Saifan:

"Tujiegemeze katika uchumi wa masoko unaotilia maanani maslahi ya kijamii, lakini tutilie umuhimu suala la misaada ya kijamii, sio tu kuzalisha bidhaa ili kupata fedha, fedha ambazo mwishowe ni chache zinazobakia mikononi. Isiwe usawa na haki zikabakia pembeni kwa maslaha ya uzalishaji mkubwa wa bidhaa. Kwa maneno mengine, isiwe kwamba sehemu kubwa ya jamii ibakie kuwa maskini, ili sehemu ndogo iwe tajiri."

Syria inatafuta njia ya kujikwamua kutoka mfumo wa uchumi wa mpangilio na ulio wa kimangimeza. Vikwazo vilivowekwa na Marekani tangu miaka mitano iliopita bado vingaliko na vimeitenga nchi hiyo, kimataifa. Lakini Rais Obama wa Marekani anajitahidi kuijongelea nchi hiyo na amempeleka balozi wa nchi yake hadi Damascus. Pia baraza hili la uchumi baina ya Ujerumani na Syria litazileta nchi hizo mbili zikikaribiana zaidi. Hivyo ndivyo anavotaraji katibu wa nchi wa Ujerumani, Bernd Pfaffenbach, na alisema hivi huko Syria:

"Naamini , maisha ni muhimu kwa wafanya biashara kujuana, kuzungumza pamoja, na jambo hilo ni zuri kwa upande wa serekali. Baraza hili la biashara baina ya Ujerumani na Syria limetokana na takwa la upande wa Syria. Mimi nachukulia jambo hili kuwa ni ishara nzuri, na tusingekuwa watu wa busara ingekuwa hatujalikamata jambo hili. Sio nadra kwamba mwenendo mzuri katika upande wa uchumi ukaigizwa na jamii, kwamba jambo hilo litashawishi siasa ya kila nchi, ni jambo linalotamaniwa."

Bado mambo yameduwaa kutokana na umangi meza wa serekali, ulaji rushwa na kutoaminiana. Mara nyingi makampuni ya Syria hayawezi kushindana, kimataifa. Kwa hivyo, Umoja wa Ulaya unawasaidia wafanya biashara wadogo na wa wastani. Mkataba wa kuifungamanisha Syria kibiashara na Umoja wa Ulaya uko tayari kutiwa saini, lakini haujaanza kufanya kazi kutokana na vile Syria imeorodheshwa kuwa ni nchi yenye serekali korofi. Kwa mfanya biashara Karkour, Syria haina mbadala wa kujifungua, kiuchumi. Syria inazihitaji nchi za Magharibi kama vile nchi za Magharibi zinavoihitaji Syria kwa ajili ya mwenendo wa amani wa Mashariki ya Kati. Maendeleo ya uchumi yanaweza kuifanya njia iwe pana zaidi.

"Uchumi na siasa ni pande mbili za sarafu. Biashara nzuri inashawishi vizuri siasa. Kwa hivyo, tunataraji kwamba harakati zetu zitaboresha, kwa ujumla, uhusiano baina ya Ujerumani na Syria."

Mwandishi: Leidholdt, Ulrich/Othman, Miraji/ ZR

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com