1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Angela Mdungu
30 Aprili 2021

Kati ya masuala yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na matumaini ya shirika la Afya duniani WHO kwa chanjo, katika mapambano dhidi ya Malaria

https://p.dw.com/p/3so5e
Somalia Präsident Mohamed Abdullahi Mohamed
Picha: Vladimir Smirnov/TASS/imago images

Kati ya masuala yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani wiki hii ni pamoja na matumaini ya shirika la Afya duniani katika chanjo dhidi ya Malaria, hatari inayoikabili Chad baada ya kifo cha Rais Idris Deby pamoja na hatua ya Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed kuachana na mpango wake wa kutaka kuongeza muhula mwigine  wa uongozi

Frankfuter Allgemeine

Gazeti la Frankfuter Allgemeine wiki kii liliandika kuhusu matumaini ya shirika la afya duniani kwa chanjo dhidi ya Malaria. Limeandika, kwa karibu miaka mitano iliyopita, kumekuwa na mafanikio  makubwa katika vita dhidi ya Malaria,hasa barani Afrika. Sababu ya mafanikio haya ni kuwa hadi kufikia mwaka 2016, takribani nusu ya idadi ya watu barani Afrika walikuwa wakilala kwenye neti zenye dawa ya kuuwa mbu.

Frankfuter Allgemeine limeongeza kuwa, kwa mujibu wa shirika la afya duniani, kwa mwaka 2019 watu milioni 229 ulimwenguni walikadiriwa kuwa na Malaria na 409,000 walifariki dunia kutokana na maradhi hayo. Afrika imeathiriwa zaidi. Mara nyingi ni watoto wa umri wa chini ya miaka mitano wanaopatwa na Malaria, na kila baada ya dakika mbili, mtoto mmoja hufariki kwa ugonjwa huo.

Sasa, shirika hilo la afya duniani linalenga kuwafikia kwanza watoto katika kutoa chanjo ya kwanza dhidi ya Malaria. Ni chanjo iliyoidhinishwa mwaka 2015 na ilianza kutumika mwaka 2019 katika majaribio ya awali, ambako maeneo yaliyochaguliwa kupokea chanjo hizo ni pamoja na Ghana, Kenya na Malawi. Kwa upande wa Kenya, chanjo hizo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikitolewa kwenye eneo la Ziwa Victoria.

Der Freitag

Gazeti la der freitag limeandika kuhusu namna kifo cha rais wa Tschad Idris Deby kinavyoweza kusababisha ukanda wa Sahel kubadilika kuwa janga. Gazeti hilo lina maelezo kuwa, upande wa upinzani nchini Chad ulitangaza haraka kupinga uliposikia Rais Deby aliyekuwa madarakani kwa miaka 30, alitaka kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa April 11. Kwa kuwa taifa hilo la ukanda wa SAHEL lilikuwa katika amri ya kutokutoka nje, maandamano ya umma yalipigwa marufuku. Yeyote aliyekiuka amri hiyo alikumbana na ukatili wa kutisha uliofanywa na polisi.

Makundi ya waasi nchini humo likiwemo Boko Haram, hayakutaka kukubali muhula wa sita wa uongozi wa Rais Deby aliyeuwawa katika mapambano na waasi.Kwa sasa taifa hilo linaongozwa na utawala wa kijeshi chini ya mtoto wa Deby Jenerali Mahmat Idris Deby aliyetangaza uchaguzi ujao kuwa Oktoba 2022 ingawa katiba inataka kipindi cha mpito cha siku 45 hadi 90 kunapotokea mapinduzi nchini humo.

Jenerali Mahmat Deby ametambuliwa na Umoja wa Ulaya licha ya ukiukwaji wa  demokrasia ambao kwa kawaida huwekewa vikwazo vikali. Hata Rais Emmanuel Macron alihudhuria maziko ya Rais Derby na kumhakikishia mtawala huyo mpya wa kijeshi ushirikiano wa Ufaransa kama ilivyokuwa kwa baba yake.

Frankfuter Allgemeine

Frankfuter Allgemeine liliandika kuhusu hatua ya kampuni ya  mafuta ya Total ya kufunga miradi yake ya gesi barani Afrika. Kwa dola bilioni 20, Total, ilitaka kuzalisha gesi asilia kwa kushirikiana na kampuni nyingine katika pwani ya Msumbiji, ili iichakate na kuisambaza duniani kote. Kwa sasa Total imetangaza haiwezi kuendelea na mradi huo kutokana na mashambulizi ya kigaidi likiwemo lile lililoelekezwa kwenye mji wa Palma kaskazini mwa Cabo Delgado, wiki tano zilizopita.

Uamuzi wa Total kujiondoa Msumbiji umekosolewa na taasisi ya uwekezaji ya nishati barani Afrika inaysema uamuzi wa kukatisha mkataba wa kampuni hiyo kutokana na mashambulio ya kigaidi umefanywa mapema mno  na ungeweza kuzuilika. Taasisi hiyo imesema, ni kweli Msumbiji  ina matatizo ya kiusalama lakini haipo hata kwenye nchi kumi zinazoshika nafasi ya juu kwa matukio ya kigaidi.

Süddeutsche Zeitung

Süddeutsche Zeitung liliandika habari kuhusu uamuzi wa Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed wa kuachana na mpango wa kutaka kuongeza muhula wake wa uongozi. Gazeti hilo limeeleza kuwa, katika siku chache zilizopita, kumekuwa na maandamano ya kumpinga Rais huyo katika mji mkuu Mogadishu.

Mapigano kati ya makabila hasimu yaliibuka huku Umoja wa Ulaya na Marekani wakitishia kumuwekea vikwazo Rais Mohammed Abdullahi baada ya kufuta uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Februari. Jumanne, wakati wa hotuba yake, Wasomali wengi waliamini kuwa Rais wao mtata angetangaza kujiuzulu, badala yake alihutubia usiku wa manane watu wengi wakiwa wamelala. Hakuonesha kutaka kujiuzulu alitangaza tu kuwa angependekeza kwa bunge kuwa atauweka kando mpango wake wa miaka miwili ya ziada na uchaguzi utafanyika hivi karibuni.

Süddeutsche Zeitung limeandika, hatua hii inatarajiwa kutatua tatizo kwa muda mfupi lakini matatizo mengi yatabaki bila majibu kwa muda mrefu.