Abbas: Hakuna matarajio ya mapatano ya amani na Israel ifikapo mwisho wa mwaka huu | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Abbas: Hakuna matarajio ya mapatano ya amani na Israel ifikapo mwisho wa mwaka huu

Hakuna matumaini ya mapatano baina ya Israel na Wapalastina mwaka huu

Rais wa Wapalastina, Mahmoud Abbas( kushoto), na waziri mkuu was Israel, Ehud Olmert.

Rais wa Wapalastina, Mahmoud Abbas( kushoto), na waziri mkuu was Israel, Ehud Olmert.

Rais wa Wapalastina, Mahmoud Abbas amesema ana wasiwasi kama mapatano ya amani na Israel yataweza kufikiwa ifikapo mwisho wa mwaka huu. Aliongeza kusema kwamba hamna hata moja kati ya masuala sita muhimu yanayohusiana na mzozo baina ya Wapalastina na Israel yaliotanzuliwa. Wakati huo huo, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema atajiuzulu mara pale chama chake cha Kadima kitakapochaguwa kiongozi mpya katika uchaguzi unaopangwa kufanywa wiki ijayo. Hata hivyo, alisema yeye anataraji mapatano makubwa yanaweza kufikiwa ifikapo mwisho wa mwaka huu.


Rais Mahmoud Abbas aliapa kwamba ataendelea kufanya mazungumzo ya amani pamoja na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, hadi siku ya mwisho ya kuweko madarakani waziri mkuu huyo aliyozongwa na kashfa. Pia atafanya mazungumzo na mtu yeyote atakayechukuwa nafasi ya Ehud Olmert. Lakini aliliambia gazeti la Haaretz la huko Israel kwamba ana wasiwasi kama pande mbili hizo zitayafikia matarajio ya Marekani ya kufikia hata mapatano fulani ya amani kabla ya Rais George Bush wa Marekani kuondoka madarakani Januari mwakani.


Mahmoud Abbas alisema upande wa Wapalastina umewasilisha fikra na matakwa yao kuhusu masuala sita, lakini hawajapokea jibu lolote kutoka upande wa Israel. Aliyasema hayo leo ikiwa imetimia miaka 15 tangu kutiwa saini mapatano ya muda ya amani huko Oslo na viongozi wa Israel na Palastina, marehemu Yitzhak Rabin na Yasser Arafat. Mapatano hayo yalitoa utawala wa ndani kwa Wapalastina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza, hivyo kuwezesha kuundwa utawala wa ndani wa Wapalastina. Pia ilitakiwe kuweko dola mbili, ile ya Israel na ya Wapalastina.


Bwana Abbas alisema Marekani inachangia kwa sehemu kubwa katika mwenendo huo wa amani, na japokuwa maafisa wa Kimarekani wana hamu mapatano yafikiwe ifikapo mwisho wa mwaka huu, na wana hakika jambo hilo linawezekana, lakini tafauti baina ya pande mbili ni kubwa mno. Alitaja kwamba mizozo ya kisiasa ndani ya Israel ni sababu ya kutokweko maendeleo katika mwenendo wa amani. Masuala yanayoleta utata baina ya pande hizo mbili katika mashauriano ya amani ni vipi mipaka mipya itakavyokuwa, tatizo la wakimbizi wa Kipalastina, usalama, na suala gumu kabisa juu hali ya baadae ya mji wa Jerusalem.


Mahmoud Abbas aliongeza kusema kwamba Israel lazima izungumziwe juu ya dhamana yake kwa wakimbizi wa Kipalastina na haki yao ya kurejea makwao, akitaja kwamba Wapalastina wasiorejea Israel wataweza kurejea Palastina. Kiongozi huyo wa Wapalastina alikariri kwamba hatakubali kutia saini mapatano ya muda yanayotaja juu ya mipaka ya muda. Anachotaka ni kwamba mapatano yeyote lazima yazungumzie masuala yote ya mzozo huo, likiwemo suala la Jerusalem.


Lakini leo Israel iliyakataa matakwa ya Wapalastina ya kuliingiza suala la mji wa Israel katika mashauriano ya sasa ya amani, na ikasema imelalamika kutokana na matamshi yaliotolewa na balozi mdogo wa Marekani kwamba Israel imekubali suala hilo lizungumziwe.


Pia waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alisema jana kwamba punde baada ya Chama cha Kadima kuchaguwa kiongozi, anapanga kujiuzulu wadhifa wake na atamwambia rais wa nchi kwamba mtu atakayechaguliwa anafaa aunde serekali mpya.


Olmert, ambaye amezongwa na mlolongo wa kashfa za rushwa, ataweza kubakia kama waziri mkuu wa kujishikiza kwa wiki au miezi kadhaa baada ya kujiuzulu rasmi hadi pale serekali mpya itakapoundwa au kufanyika uchaguzi mkuu. • Tarehe 12.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGwL
 • Tarehe 12.09.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FGwL
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com