Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje Mashariki ya kati | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje Mashariki ya kati

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani atilia mkazo haki ya Israel kuishi kwa amani na haki ya Palastina kuwa na taifa lao

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani (kushoto) na rais Shimon Peres wa Israel

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani (kushoto) na rais Shimon Peres wa Israel

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle leo amekataa kufuta uwezekano kwa Iran kuwekewa vikwazo vikali zaidi kutokana na tamaa yake ya kuwa na silaha za nuklea.

_________________________

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Jerusalem waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema kwao wao kuwepo kwa Iran yenye kumiliki silaha za nuklea kwa njia yoyote ile ni jambo lisilokubalika.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman, Westerwelle amesema usalama wa Israel ni jambo lisilokuwa na mjadala kwa kila mtu na hususan kwa Wajerumani.

Amesema hilo ni suala linalohusu jumuiya nzima ya kimataifa na sio tu Israel.

Lieberamn kwa uwpande wake amesema wakati umefika kwa kuliweka wazi suala hilo na kufanya maamuzi yasiotetereka.

Rais Shimon Peres wa Israel pia ameitaka Ujerumani kuendelea kuishinikiza Iran.

Peres amesema vitisho vya maangamizi, kukanusha kutokea kwa maangamizi ya Wayahudi wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia yaliofanywa na Manazi wa Ujerumani,kugharamia kwa kiasi kikubwa cha fedha na kuunga mkono makundi ya kigaidi ikiwa ni pamoja na Hezbollah nchii Lebanon na Hamas huko Gaza ni mambo mazito ambayo hayapaswi kupuuzwa.

Ujerumani ni mojawapo ya mataifa sita makubwa yenye nguvu duniani yanayozungumza na Iran juu ya mpango wake wa nuklea ambao mataifa ya magharibi yanautilia mashaka kuwa ni kwa ajili ya kutengeneza silaha za nuklea.

Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani amesisitiza msimamo wa nchi yake kuiunga mkono Israel laki pia kuwepo kwa ufumbuzi wa mataifa mawili kwa mzozo kati ya nchi hiyo na Wapalestina.

Westerwelle pia amesema kwamba lengo lao ni kuwepo kwa ufumbuzi wa kweli wa mataifa mawili ambapo taifa la Israel liheshimiwe na mataifa yote jirani na kuwepo kwa taifa la Palestina lenye kufanya kazi.

Ameepuka kuikosoa Israel kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina.

Mapema akiwa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi Westerwelle amewataka Waisrael na Wapalestina kurudi katika meza ya mazungumzo ya amani kwa haraka iwezekanavyo.

Kaimu Waziri Mkuu wa Wapalestina Salama Fayyad amesema baada ya kukutana na Westerwelle mjini Ramallah kwamba waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani anaunga mkono madai ya Wapalestina ya kusitishwa kabisa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu na Israel ikiwa ni pamoja na Jerusalem ya Mashariki.

Fayyad ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wamezungumzia matakwa ya mpango wa ramani ya amani ambapo Israel inapaswa kusitisha harakati zote za ujenzi wa makaazi katika maeneo yote na kwamba kulikuwa na makubaliano na waziri huyo wa Ujerumani juu ya jambo hilo.

Serikali ya Ujerumani ilielezea kusikitishwa kwake sana na uamuzi wa Israel kujenga makaazi katika ardhi ilioinyakua na kuikalia kwa mabavu katika vita vya mwaka 1967 na kuijumuisha kwenye mipaka ya manispaa ya Jerusalem.

Ujerumani inaona ujenzi wa makaazi hayo kuwa kikwazo kikubwa katika njia ya kusonga mbele na mchakato wa amani.

Waziri huyo mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani alifanya safari hiyo fupi huko Ramallah akitokea Jerusalem ambapo baada ya kuwasili kwake hapo jana alitembelea kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi ya Yad Vashem kabla ya kuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Israel Avigdor Lieberman hapo jioni.

Akitembelea eneo la kumbukumbu ya Maangamizi ya Wayahudi ya Yad Vashem ya Wayahudi milioni sita waliouwawa na Manazi wa Ujerumani wakati wa Vita Vikuu vya Pili Westerwelle amesema Ujerumani ina wajibu maalum kwa Israel.

Ziara ya Westerwelle Mashariki ya Kati inakuja wiki moja kabla ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukutana mjini Berlin na Kansela Angela Merkel na mawaziri wa Israel na Ujerumani kuwa na kikao cha pamoja.

Ziara yake inafanyika wakati kukiwa na repoti za juhudi mpya na hata uwezekano wa kufikiwa makubaliano katika mazungumzo yanayosuluhishwa na Ujerumani ya kumuachilia huru askari wa Israel anayeshikiliwa na kundi la Hamas la Wapalestina kwa zaidi ya miaka mitatu katika Ukanda wa Gaza.

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Lieberman akikutana na Westerwelle hapo jana alimshukuru waziri mwenzake kwa juhudi za serikali ya Ujerumani kufanikisha makubaliano hayo akisema kwamba bado haiko wazi iwapo kutafikiwa kwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Israel na kundi hilo la Hamas.


Mwandishi:Mohamed Dahman /DPA

Mhariri:M.Abdul-Rahman • Tarehe 24.11.2009
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KeS8
 • Tarehe 24.11.2009
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KeS8
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com