1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi wanahofiwa watakufa.

Mtullya, Abdu Said13 Mei 2008

Habari kutoka China zinasema watu wapatao 12,000 wameshakufa kutokana na tetemeko kubwa la ardhi nchini humo.

https://p.dw.com/p/Dyxg
Mwanafunzi asaidia kukabiliana na maafa ya tetemeko la ardhi nchini China.Picha: AP

Watu wasiopungua  12,000 wamekufa kutokana  na  tetemeko la ardhi,  katika jimbo  la  Sechuan kusini mashariki mwa China. Na habari   zinasema hali ni mbaya zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.

Siku moja  baada  ya  tetemeko hilo kutokea  idadi ya watu waliokufa imeshafikia 12,000. Na maiti  zaidi zinaendelea kupatikana. Shirika la habari la China Xinhua limesema maalfu wengine  wamejeruhiwa katika jimbo la Sechuan kusini  mashariki mwa China. 

Maafisa wa serikali wamesema wanahofia watu wengi zaidi  watakufa kutokana  na athari  za  tetemeko hilo lililokuja na nguvu ambazo hazijawahi kuonekana katika kipindi cha miaka 30 iliyopita nchini China.

Waziri mkuu wa  China  bwana Wen Jiabao  alielitembela jimbo la maafa la Sechuan  amesema hali ni mbaya zaidi kuliko ilivyohofiwa hapo awali.

Kitovu cha tetemeko hilo lililofikia nguvu ya 7.8  kilikuwa  Chengdu, mji mkuu wa jimbo la Sechuan.

Nguvu  ya tetemeko hilo ilifikia hadi miji ya Beijing na hata nje ya  China  katika mji mkuu wa Thailand, Bhangkok.

Timu  ya waokoaji ya wanajeshia na madaktari imewasili katika mji wa Wenchua  ambao umekatika  kimasiliano na miji mingine,kutokana na  nguvu ya tetemeko.

Lakini habari zinasema juhudi za kuwakoa watu  zaidi  zinakabiliwa na ugumu kutokana na mvua kubwa na kutokana na barabara kuharibika sana.