1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMashariki ya Kati

Baerbock apinga kurejesha uhusiano na Assad bila ya masharti

Zainab Aziz
16 Mei 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ametahadharisha juu ya kusawazisha uhusiano na rais wa Syria, Bashar al-Assad bila ya kumpa masharti. Ameyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/4RNyE
Saudi-Arabien | Besuch Außenministerin Baerbock in Dschidda
Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amefanya ziara nchini Saudi Arabia wakati ambapo nchi hiyo inajiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa Umoja wa nchi za Kiarabu unaotarajiwa kufanyika mjini Jeddah, siku ya Ijumaa ambapo Syria pia itashiriki. 

Baerbock amesema kila hatua ya kumsogelea Assad inapaswa kuambatanishwa na masharti. Waziri huyo wa Ujerumani ametoa kauli hiyo baada ya kukutana na waziri mwenza, wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud ambapo mawaziri hao pia walijadili masuala ya eneo la mashariki ya kati na ya kimataifa.

Katikati: Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alipowasili Jeddah.
Katikati: Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alipowasili Jeddah.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Ujerumani na Saudi Arabia walikutana katika mji wa bandari wa Jeddah, kwenye Bahari Nyekundu, ambapo Baerbock alisisitiza kwamba rais wa Syria Bashar al Assad hapaswi kukumbatiwa kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Syria. Hata hivyo nchi kadhaa za kiarabu zimelegeza misimamo yao juu ya rais huyo wa Syria, mnamo miezi ya hivi karibuni.

Soma:Ujerumani haioni sababu ya kurejesha uhusiano na Syria

Baerbock amesema Ujerumani na Saudi Arabia zinataka kuimarisha ushirikiano wao katika mageuzi ya viwanda na uchumi kwa kuzingatia mgogoro wa hali ya hewa. Amesema upo uwezekano mkubwa wa kukuza jitihada za kutafuta nishati mbadala kama nishati ya jua na pia nishati ya upepo.

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani. Nchi hiyo inayafanya marekebisho ya kina katika uchumi wake, ambapo inataka kupunguza utegemezi wake wa mafuta na gesi kulingana na mpango wake wa kufanikisha matarajio na malengo yake hadi kufikia mwaka 2030 ambapo taifa hilo linataka kubadilika na kuwa muuzaji mkuu wa nishati ya haidrojeni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan Al Saud. Picha: Hadi Mizban/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo Rais wa Syria Bashar al-Assad amealikwa na rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan, kuhudhuria mkutano ujao wa hali ya hewa wa COP28 utakaofanyika Dubai tarehe 30 mwezi Novemba.

Soma:Syria yarejea katika Umoja wa kiarabu

Shirika la Habari la serikali ya Syria SANA, limeripoti kwamba Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, COP28 litakuwa mkutano mkuu wa kwanza kwa rais wa Syria Bashar al Assad kuwa pamoja na viongozi wengi wa nchi za magharibi tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini mwake mnamo mwaka 2011.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad.
Rais wa Syria, Bashar al-Assad.Picha: Joseph Eid/AFP/Getty Images

Wakati wa mkutano wa mwisho wa COP27 uliofanyika nchini Misri, Syria iliwakilishwa na wajumbe 14 miongoni mwao Waziri wa Mazingira wa Syria Hussein Makhlouf. Rais wa Marekani Joe Biden, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na raia nwa Ufaransa Emmanuel Macron pia walihudhuria mkutano huo.

Chanzo:/DPA