Waziri mkuu wa Urusi Putin atazamiwa kuwasili Ujerumani hii leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri mkuu wa Urusi Putin atazamiwa kuwasili Ujerumani hii leo

Majadiliano makali yanatarajiwa kati ya waziri mkuu Putin na kansela Angela Merkel

Kansela Angela Merkel

Kansela Angela MerkelWaziri mkuu wa Urusi Vladimir Putin anasubiriwa kwa hamu kubwa hii leo mjini Berlin kwa mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel yatakayogubikwa na mzozo wa gesi. Hata hivyo waziri mkuu huyo wa Urusi anatazamiwa kutunukiwa nishani ya jimbo la Sachsen alikowahi kufanya kazi kama mtumishi wa idara ya upelelezi ya Urusi KGB.


Mkutano wa viongozi hao wawili wa serikali unasadif baada ya kansela Angela Merkel kulalamika jana wakati wa mkutano wa waandishi habari mwishoni mwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown alipotamka:


"Nnaamini kuna hatari kwamba Urusi inaweza kupoteza imani kutokana na kuzuiliwa kwa muda mrefu gesi inayosafirishwa hadi katika nchi za Ulaya,na nitamuarifu waziri mkuu Vladimir Putin tutakapokutana,kwamba tunabidi kurejesha hali ya kuaminiana".


Msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani Thomas Steg amezungumzia juu ya "hali isiyokubalika hata kidogo kwamba nchi za Ulaya ziangukie mhanga wa mzozo kati ya Urusi na Ukraine. Bwana Thomas Steg amesisitiza wakati huo huo kwamba pande zote mbili; Moscow na Kiev zinabeba dhamana.''Pande zote mbili hazitekelezi dhamana zao. Pande zote mbili zinashindwa kulipatia ufumbuzi wa maana tatizo lililopo," amesema msemaji wa serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin.


Ujerumani ndio mteja mkubwa wa gesi ya Urusi, ikiagizia mita za ujazo bilioni 36 za gesi kwa mwaka 2007-hata kama kiwango hicho hakipindukii kwa mfano kile cha Bulgaria inayoagizia asilimia 40 ya gesi yake kutoka Urusi.


Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times Deutschland, akiba ya gesi ya Ujerumani imepungua na kufikia asili mia 59 na huenda ikafikia asili mia 50 hadi wiki ijayo ikiwa gesi inayopitia Ukraine haitaanza upya kufunguliwa.


Ujerumani inashikilia nafasi muhimu katika mzozo huu hasa kwa kuwa ina maingiliano mazuri na Urusi ikilinganishwa na nchi nyengine za Umoja wa ulaya. Wadadisi wanaamini ikiwa Vladimir atamsikiliza mtu, basi ni Angela Merkel.


Mtaalam wa uhusiano kati ya Urusi na Ujerumani Stefan Meister anaamini,kansela Angela Merkel atafanya kila awezalo kumtanabahisha Vladimir Putin,katika wakati ambapo Umoja wa Ulaya umezitishia pande zote mbili Moscow na Kiev kupitisha "hatua kali za kiuchumi na kisiasa."


Kabla ya mazungumzo yake pamoja na kansela Angela Merkel,waziri mkuu wa Urusi, Vladimir Putin atayatembelea maonyesho ya kilimo (Wiki ya kijani) mjini Berlin na anatazamiwa pia kushiriki katika hafla ya burudani ya Dresden leo usiku ambako Vladimir Putin atatunukiwa nishani ya heshima na serikali ya jimbo la Sachsen kwa mchango wake katika kuimarisha uhusiano wa kitamaduni kati ya Ujerumani na Urusi.
 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ga0l
 • Tarehe 16.01.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ga0l
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com