Wasemavyo walimwengu juu ya mabadiliko katika Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.08.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wasemavyo walimwengu juu ya mabadiliko katika Libya

Ulimwengu wote umeshakubali, kama walivyo wananchi wenyewe wa Libya, kwamba enzi ya kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, iliodumu zaidi ya miaka 40, sasa imekwisha.

default

Mtu afyetua risasi hewani kusheherekea kuingia majeshi ya waasi mjini Tripoli

Ulimwengu wote umeshakubali, kama walivyo wananchi wenyewe wa Libya, kwamba enzi ya kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, iliodumu zaidi ya miaka 40, sasa imekwisha. Ni suala la masaa tu kwa serikali mpya kutangazwa huko Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo. Kwa vyovyote , bila ya kujali namna vita hivyo vilivokwenda na roho nyingi za Walibya zilizopotea, walimwengu sasa watapumua kuona kwamba kuna tamaa ya kukoma kabisa umwagaji wa damu katika nchi hiyo ya Afrika ya Kaskazini.

Kansela Angela wa Ujerumani amemtaka kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, atangaze kuondoka madarakani, hivyo kuepusha kumwagika damu zaidi:

Deutschland Libyen Angela Merkel in Berlin zu Flugverbotszone

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwahutubia waandishi wa habari mjini Berlin

"Bila ya shaka, tuna furaha. Kwa muda mrefu nimesema, kama vile alivosema waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, kwamba Gaddafi amepoteza uhalali wake, na ingekuwa uzuri kwamba kwa haraka kama iwezekanavyo angesalimu amri na kupusha damu kumwagika na roho zaidi za watu kupotea...."

Masaa machache yaliopita, waziri wa mambo ya kigeni wa Italy, Franco Frattini, aiiambia televisheni ya Sky Italia kwamba majeshi ya Gaddafi yanadhibiti tu asilimia 10 hadi 15 ya Tripoli, na akamtaka kiongozi huyo wa Libya asalimu amri ili kuepusha uwezekano wa kumwagika damu nyingi. Italy ni nchi ya Ulaya ilio karibu sana na Libya, kijiografia, na ambayo vituo vyake vilitumiwa na ndege za NATO katika kudhoofisha nguvu za majeshi ya Gaddafi, hivyo kuwawezesha waasi wa Libya kusonga mbele kwa kasi karibuni hadi mji mkuu wa Tripoli. Alisema wakati umekwisha kwa Gaddafi kutaka kufanya mashauriano juu ya uwezekano wa yeye kwenda uhamishoni, na kwamba lazima akabiliane na mashtaka mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu huko The Hague.

Waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron, amefupisha likizo yake ili ahudhurie leo asubuhi mkutano wa London juu ya usalama kuhusu Libya, wakati jeshi la Uingereza limefichua kwamba lilikishambulia kituo cha operesheni za kijeshi kinachotumiwa na utawala wa Gaddafi hukoTripoli, na pia kukipiga kifaru kilichowekwa nje ya mji wa Tripoli. Na serikali hiyohiyo ya Uingereza imeliomba baraza la mpito la taifa huko Libya lilinde usalama nchini humo na kutolipiza visasi. Pia ilimtaka Gaddafi asalimu amri baada ya majeshi yake kuzishambulia sehemu za katikati ya Tripoli hii leo alfajiri. Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Alistair Burt, alisema kwanza kabisa nchi yake inamtaka Gaddafi aondoke sasa na aepushe kumwagika damu zaidi.

Na wizara ya mambo ya kigeni ya China ilisema nchi hiyo inaheshimu uchaguzi wa watu wa Libya, na ikasema inataraji utulivu utarejea kwa haraka Libya wakati mapigano yakihanikiza katika eneo anakoishi Gaddafi. Marekani ilisema utawala wa Gaddafi uko nchani kabisa ya kuanguka.

Kutoka Afrika Kusini, waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Maite Nkoana-Mashabane, amesea nchi yake haisaidii kupanga kuondoka Muammar Gaddafi kutoka Libya, na kwamba yeye anajuwa kwamba mwenyewe Muammar Gaddafi hatotaka kuomba hifadhi nchini Afrika Kusini.

"Tumesema mara kadhaa, kama Umoja wa Afrika, suluhisho la matatizo ya kisiasa ya Libya yanapaswa kushughulikiwa na Walibya wnyewe."

Alizikanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba Afrika Kusini imepeleka ndege hadi Libya kwa Gaddafi kuondoka. Alisema haijulikani wapi aliko Gaddafi. Alisema anashangaa kwamba kuna hata tetesi kwamba Afrika Kusini inapanga kuondoka Libya kwa mtu yeyote. Itakumbukwa kwamba Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini aliongoza juhudi za upatanishi za Umoja wa Afrika, AU, lakini ziara zake mbili za kibinafsi hadi Libya zilishindwa kutoa matunda yeyote.

Na balozi wa baraza la mpito la taifa la Libya nchini Marekani, Ali Suleiman Audschali, amesema kwamba ana habari nzuri kwamba kikosi cha Gaddafi katika mji wa Brega kimepandisha juu bendera nyeupe ya kusalimu amri, hivyo ina maana Libya iko chini ya udhibiti wa baraza hilo la mpito la kitaifa, lenye makao yake hadi sasa mjini Benghazi.

Mwandishi: Othman Miraji /rtr,afp

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com