1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani Thailand watishia kuendeleza mapambano dhidi ya serikali

Kabogo Grace Patricia13 Aprili 2010

Waandamanaji hao wanamtaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abhisit Vejjajiva ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/MvTL
Waandamanaji wanaoipinga serikali ya Thailand, wakiandamana kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Bangkok.Picha: AP

Waandamanaji nchini Thailand wanaoipinga serekali ya nchi hiyo wametishia kuandamana hadi kwenye kambi ya jeshi ambako Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abhisit Vejjajiva ameweka makao yake baada ya tume ya uchaguzi bila kutarajiwa kupendekeza chama cha kiongozi huyo kifutwe kwa kukiuka utaratibu unaohusiana na  ufadhili kwa vyama vya kisiasa.

Waziri Mkuu wa Thailand Abhisit Vejjajiva aliyeingia madarakani mwaka 2008, huenda akaachia madaraka iwapo mahakama ya kikatiba itakikuta chama chake tawala kina hatia ya kutumia vibaya michango ya fedha kwa ajili ya uchaguzi, kutokana na uchunguzi uliofanywa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo. Waandamanaji hao wanaojiita " mashati mekundu'', wameahidi kuendeleza mapambano hadi hapo Bwana Vejjajiva atakapojiuzulu na kuitisha uchaguzi mwingine.

Kiongozi wa waandamanaji hao, Nattawut Saikua amewaambia waandishi habari kuwa wataandamana hadi katika kambi ya 11 ya jeshi kupata majibu ya kiongozi huyo pamoja na jeshi la Thailand kufuatia mauaji ya watu 21 yaliyotokea mwishoni mwa wiki na wengine 800 kujeruhiwa. Maandamano hayo yaliyodumu kwa muda wa mwezi mmoja hapo awali hayakukumbwa na tukio lolote la umwagaji wa damu. Bwana Vejajjiva amekuwa akiendesha shughuli zake kutoka kwenye kambi hiyo tangu maadanamano hayo yalipoanza. Waandamanaji hao wanaoipinga serikali wamesema kuwa wanajeshi waliwaua kwa kuwapiga risasi waandamanaji hao, lakini serikali imesema kuwa kivuli cha ''magaidi'' ndio kinahusika kwa mauaji hayo.

Kiasi watu 300 waliovalia ''mashati ya njano'', walikusanyika katika mnara wa makumbusho ya vita mjini Bangkok wakiwataka waandamanaji wa ''mashati mekundu'' kurudi nyumbani na kuacha kuiharibu nchi hiyo kwa kuwa wao wanataka amani. Kundi hilo la watu hao wanaovalia ''mashati ya njano'' linawajumuisha, wanataaluma, wafanyabiashara, wafuasi wa mfalme na wanaharakati wa tabaka la wastani. Kundi hili linampinga waziri mkuu wa zamani aliyeondolewa madarakani, Thaksin Shinawatra na vyama vya kisiasa anavyoviunga mkono akiwa uhamishoni.

Aidha, mkuu wa majeshi ya Thailand, Anupong Paochinda, jana alisema kuwa kuitishwa uchaguzi wa haraka kutasaidia kutatua mzozo wa kisiasa unaoendela nchini humo. Naibu Waziri Mkuu wa Thailand, Suthep Thuagsuban amesema anataka kumaliza mzozo huo haraka na kwamba muda wa miezi tisa uliowekwa kwa ajili ya kulivunja bunge ni muda muafaka.

Nayo Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia-ASEAN, imesema kuwa mzozo wa kisiasa nchini Thailand unatishia usalama wa eneo hilo kwa jumla na kwamba hali hiyo isipotatuliwa mapema inaweza ikaleta ghazia zaidi na kusababisha mauaji zaidi. Mkuu wa jumuiya hiyo, Surin Pitsuwan amesema kuwa wako tayari kuisaidia Thailand kuleta hali ya usalama bila kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo, iwapo nchi hiyo itaomba msaada.

Wakati huo huo, wananchi wa Thailand leo wameanza siku tatu za maadhimisho ya kuanza kwa mwaka mpya wa kalenda ya nchi hiyo. Maadhimisho hayo yanajumuisha matukio mbalimbali ikiwemo kucheza, kunywa pombe kali na michezo ya kupigana kwa maji.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/APE/RTRE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed