Wadukuzi wadai dola milioni 70 kurudisha data
5 Julai 2021Madai hayo ya kulipwa yamechapishwa kwenye blogu ambayo hutumiwa na genge la uhalifu wa mitandaoni la REvil, kundi linalohusishwa na Urusi ambalo linazingatiwa kuwa miongoni mwa wanyang'anyi hatari sana katika ulimwengu wa uhalifu wa mitandaoni.
Shambulizi la mtandaoni la REvil, ambalo lilifanywa Ijumaa iliyopita, ni miongoni mwa mashambulizi makali katika msururu wa matukio yanayoongezeka ya udukuzi wa kutaka kuonekana na kusikika.
Kampuni ya Kaseya yahujumiwa
Kundi hilo la wahuni lilivamia kampuni ya Kaseya ambayo ni ya teknolojia ya habari yenye makao yake mjini Miami, nchini Marekani, na kuingia katika baadhi ya data za wateja wa wateja wao, na kuzusha mfululizo wa matukio yaliyoharibu kompyuta za mamia ya kampuni kote duniani. Fred Voccola ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Kaseya "Kile ambacho maafisa wa serikali wana uhakika nacho, ni kuwa ni kundi la REvil, ambalo halihusiani na serikali ya Urusi, kwa hiyo hawaamini kama ni shambulizi la serikali ya Urusi au vyombo vya ujasusi. Ni udukuzi unaohusishwa na mtandao wa kimataifa ambao una watu kote duniani na ndio ambao wanaamini sana wamehusika na hili." Amesema Voccola. Voccola amesema kampuni hiyo inafahamu kuhusu masharti ya kikomboleo lakini hakusema kama watatoa au la.
Mapema jana, Ikulu ya White House ilisema inawatafuta waathirika wa shambulizi hilo "ili kuwapa msaada kwa kuzingatia tathmini ya kitisho cha kitaifa”. Athari za shambulizi hilo bado zinajitokeza. Walioshambuliwa ni pamoja na shule, mashirika madogo madogo ya sekta ya umma, mashirika ya kusafiri na starehe na vyama vya mikopo na wahasibu.
Biden aahidi kuchukua hatua
Rais wa Marekani Joe Biden amesema hatua itachukuliwa kama uchunguzi utaonyesha kuwa Ikulu ya Urusi ilihusika kwa njia yoyote. Nchini Ujerumani, kampuni moja ya huduma za teknolojia ya habari – IT ambayo haijatajwa jina inaamini kuwa maelfu kadhaa ya wateja wake wameathirika na shambulizi hilo. Kampuni mbili kubwa za Kiholanzi za IT, VelzArt na Hoppenbrouwer Techniek pia zimeripoti matatizo.
Shirika la Upelelezi la Marekani – FBI limesema katika taarifa kuwa linachunguza, lakini kiwango cha shambulizi hilo la mtandaoni huenda kikafanya kuwa ngumu kumshughulikia kila muwathirika kivyake.
Naibu mshauri wa Usalama wa Taifa nchini Marekani Anne Neuberger amesema Biden ameamuru kutumika raslimali zote za serikali kuchunguza tukio hilo na kumhimiza yeyote anayeamini mifumo yao ya kompyuta iliingiliwa awasiliane na FBI.
Mtalaamu wa usalama wa mitandano Dmitri Alperovitch anasema haamini kuna uwezekano wa Kremlin kuhusika, lakini shambulizi hilo linaashiria kuwa mamlaka za Urusi hazijaweza kuyadhibiti magenge ya udukuzi wa mitandaoni yanayoendesha harakati zake nchini Urusi.
AFP, Reuters, AP, DPA