Waasi mashariki mwa Ukraine wafanya uchaguzi | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Uchaguzi mashariki mwa Ukraine

Waasi mashariki mwa Ukraine wafanya uchaguzi

Wapiga kura wanachagua viongozi wa majimbo mawili yaliyojitenga na Ukraine ya Lugansk na Donetsk katika uchaguzi unaoungwa mkono na Urusi na kupingwa na nchi za Magharibi

Waasi waliojitenga Mashariki mwa Ukraine wanaoungwa mkono na Urusi wamefanya uchaguzi baada ya kuuliwa kiongozi wa juu wa waasi,licha ya nchi za Magharibi kuitolea mwito Urusi kutoyahujumu mazungumzo ya amani. Marekani na Umoja wa Ulaya mjini Brussels zinasema uchaguzi huo katika majimbo mawili ya Donetsk na Lugansk yaliyoko Mashariki mwa Ukraine utazidi kuzikwamisha juhudi za kuumaliza mgogoro ambao umeshawauwa zaidi ya watu 10,000 tangu mwaka 2014.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogheini amesema siku ya Jumamosi kwamba kwa jicho la Umoja wa Ulaya uchaguzi huo sio halali na hautambuliwi. Mjumbe maalum wa Marekani nchini Ukraine,Kurt Volker amesema uchaguzi huo ni kichekesho  na wanaitolea mwito Urusi kuuzuia usiendelee. Mjumbe huyo wa Marekani ameongeza pia kusema kwamba uchaguzi huo unakwenda kinume na makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na nchi za Magharibi.

Serikali ya Urusi mjini Moscow imeipuuza miito iliyotolewa ikisema uchaguzi huo hauhusiki chochote na makubaliano ya amani.Urusi inasema uchaguzi huo ni muhimu ili kujaza pengo la madaraka baada ya kuuwawa kiongozi wa Jamhuri ya jimbo la Donestk Alexander Zakharchenko. Kiongozi huyo aliuwawa katika shambulizi la bomu kwenye mgahawa mnamo mwezi Agosti.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi  Maria Zakharova amesema na hapa tunanukuu,'' Watu wanahitaji kuishi,kuendelea na shughuli zao za maisha na kuhakikisha kuna sheria katika jimbo ambalo linakabiliwa na vizuizi pamoja na vitisho  vya matumizi ya nguvu ya watawala wa Ukraine.

Mwaka 2014 Urusi ililichukua kwa nguvu jimbo la Crimea  na kuunga mkono uasi uliozuka Mashariki mwa Ukraine katika kile ambacho serikali ya Ukraine mjini Kiev inakiona kama hatua ya kuiadhibu kutokana na msimamo wake wa kuelemea nchi za Magharibi.

Licha ya vita vikali kumalizika migogoro inayoendelea  mara kwa mara kwenye eneo hilo imegharimu maisha ya wanajeshi na raia. Hata hivyo mazungumzo ya kutafuta amani yamekwama ma mikataba ya amani iliyosimamiwa na nchi za Magharibi na kufikiwa mwaka 2015  imeshindwa kwa kiasi kikubwa.

Baada ya kuuliwa Zakharchenko,Denis Pushilin mwenye umri wa miaka 37 aliyekuwa msimamizi wa mradi mchafu wa Urusi  wa wizi wa wawekezaji ndiye aliyekaimu wadhifa wa uongozi wa Jamhuri ya watu wa Donetsk na anatarajiwa kushinda katika uchaguzi unaofanyika. Leonid Pasechnik mkuu wa zamani wa idara ya usalama ya Ukraine na kaimu kiongozi wa jimbo la Lugansk mwenye umri wa miaka 48 naye anatarajiwa kupata ushindi kwenye uchaguzi wa jimbo hilo. Wote wawili wameshaahidi kuwa na ushirikianp mkubwa na Urusi.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com