Virusi vya Corona vyaua watu 197 Italia | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Virusi vya Corona vyaua watu 197 Italia

Idadi ya waliokufa kutokana na virusi vya Corona nchini Italia imepanda na kufikia watu 197 huku bara la Ulaya likishuhudia kuongezeka maambukizi baada ya Serbia na Vatican kurekodi visa vya kwanza vya Corona.

Idara ya Usalama wa Umma nchini Italia imesema idadi ya watu waliogundulika kuwa na virusi hivyo imepanda hadi 4,636 ikilinganishwa na visa 3,800 vya siku ya Alhamisi.

Idadi ya wagonjwa walio mahututi imefikia watu 426 na ongezeko hilo limeleta wasiwasi wa kukosekana vitanda zaidi vya kuwalaza wagonjwa wanaohitaji  msaada wa dharura.

Mripuko wa virusi vya Corona nchini Italia ndiyo mbaya zaidi barani Ulaya na kwa sehemu kubwa umeyakumba maeneo ya kaskizini ya taifa hilo.

Maambukizi zaidi yameripotiwa pia nchini Uingereza, Ufaransa, Uswisi, Ujerumani pamoja na Croatia

Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha  Johns Hopkins University nchini Marekani pamoja na tarakimu kutoka vyanzo vingine zinasema idadi ya maambukizi ya virusi vya Corona imepindukia watu 100,000 kote duniani.

WHO ina wasiwasi na kusambaa kwa virusi vya Corona 

Mjini Geneva, Shirika la Afya Duniani WHO limesema takwimu zake zinaonesha mamabukizi yamefikia watu 98,023 huku Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo akisema ulimwengu " uko kwenye ukingo wa kufikia maambukizi 100,000"

Schweiz WHO Coronavirus Covid-19

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus

Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema ana wasiwasi mkubwa kwamba ugonjwa Covid-19 unasambaa kwenye mataifa yaliyo na mifumo dhaifu ya afya yanayoweza kushindwa kudhibiti mripuko wake.

China bara ambako ndiyo chimbuko la virusi vya Corona  pamoja na Korea Kusini, Iran na Italia ndiyo mataifa yenye visa vingi vya maambukizi lakini maambukizi yameshuhudiwa pia katika mataifa mengine zaidi ya 40 duniani.

Hapo jana Croatia ilithibitisha kuwa na wagonjwa 11 wa virusi vya Corona. Taifa hilo liko jirani na Italia na kuna muingiliano mkubwa kutokana na shughuli za Utalii, biashara na uchukuzi.

G20 yatoa ahadi ya kusaidia uchumi wa ulimwengu 

Wakati huo huo mawaziri wa Fedha na magavana wa benki kuu za kundi la mataifa yaliyostawi na yale yanayoinukia, G20, wamekubaliana kuchukua hatua madhubiti za kisera na kifedha katika kukabiliana na mripuko wa virusi vya Corona na kunusuru mtikiso kwenye ukuaji wa uchumi duniani.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa leo viongozi hao waliokutana mjini Riyadh, Saudi Arabia mwezi uliopita wamezikaribisha hatua na mipango ambayo tayari imewekwa na mataifa ya kundi hilo katika kuchochea shughuli za uchumi.

Taarifa hiyo imesema kundi la G20 liko tayari kuchukua hatua za ziada kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya Corona na kusimamia uthabiti wa masoko na mfumo wa kimataifa wa kifedha.

Kusambaa kwa virusi vya Corona nje ya China kumeleta mtikisiko kwenye masoko ya mitaji duniani na kulazimisha hatua za uokozi ikiwemo benki kuu ya Marekani kupunguza kiwango cha riba kwa mabenki ya biashara.