1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kimataifa wajitolea kuleta amani Libya

Tatu Karema
20 Januari 2020

Viongozi wa dunia wamejitolea kusitisha uingiliaji wa kimataifa katika vita nchini Libya na kuzingatia marufuku ya silaha wakati wa mkutano ulioandaliwa mjini Berlin kukomesha mzozo nchini humo.

https://p.dw.com/p/3WSQa
Deutschland Libyen-Konferenz in Berlin
Picha: Reuters/A. Schmidt

Marais wa Urusi, Uturuki na Ufaransa, walikuwa miongoni mwa viongozi wa kimataifa waliotia saini makubaliano hayo ya kusitisha uingiliaji wa vita hivyo aidha kupitia kuepeleka silaha, vikosi vya kijesi ama ufadhili. Lakini mazungumzo hayo yalishindwa kuleta maridhiano kamili kati ya pande zinazozozana za kamanda muasi Khalifa Haftar na mkuu wa serikali inayotambulika na Umoja wa Mataifa Fayez al-Sarraj ama kuzifanya pande hizo mbili kutia saini mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kuwa hali ya Libya ni tete ambapo kuhakikisha usitishaji wa mara moja wa mashambulizi unazingatiwa ni vigumu lakini ana matumaini kwamba kupitia mkutano wa jana, kuna fursa ya mpango huo unaweza kudumishwa. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, amethibitisha kuwa ''bado kuna maswali kuhusu jinsi ya kushughulikia kikamilifu'' na kufuatilia kujitolea huko. Lakini amesema kuwa ana matumaini kwamba kutakuwa na ghasia za kiwango kidogo, fursa ya kuanza mazungumzo ambayo mjumbe maalumu Ghassan Salame amekuwa akijaribu kuendeleza kati ya pande zinazozozana nchini Libya.

Libya imegawika kati ya pande mbili pinzani tangu vuguvugu la mwaka 2011 lililoungwa mkono na jumuiya ya kujihami ya NATO lilipomuuwa aliyekuwa kiongozi wa muda mrefu Muammar Gadhafi. Katika siku za hivi majuzi, vikosi vinavyoongozwa na Sarraj mjini Tripoli, vimekuwa chini ya mashambulizi tangu mwezi Aprili kutoka kwa vikosi vinavoongozwa na Haftar.

Mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 280 na wapiganaji elfu 2 na kusababisha maelfu kupoteza makazi yao hadi pale mkataba hafifu wa kusitisha mapigano unaoungwa mkono na Uturuki na Urusi ulipowekwa tarehe 12 mwezi Januari. Ijapokuwa serikali ya Sarraj inatambuliwa na Umoja wa Mataifa, mataifa yenye ushawishi mkubwa yamejitenga na kumuunga mkono Haftar na kuugeuza mzozo wa taifa hilo kuwa kile ambacho baadhi wamekitaja kuwa vita vikubwa ambapo mataifa ya kigeni yameingilia kulinda maslahi yao.

Wakati huo huo, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya hii leo wanatarajiwa kuzungumzia hatua zitakazofuata katika kutekeleza harakati za amani zilizokubaliwa wakati wa mkutano mjini Berlin hapo jana.Kabla ya mkutano huo, Umoja wa Ulaya uliahidi kufanya kila liwezekanalo kutekeleza makubaliano yoyote yalioafikiwa katika meza ya mazungumzo hasa kuhusiana na hatua ya kusitishwa kwa mapigano na marufuku ya silaha ya Umoja wa Mataifa kwa Libya.

Hii huenda ikajumuisha kutuma ujumbe wa Muungano wa Ulaya katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika kulingana na mkuu wa sera za kimatifa wa Muungano huo Josep Borell.Ugiriki na Italia tayari imeonyesha kujitolea kwake kupeleka vikosi vya kijeshi huku Ujerumani ikisema inakadiria iwapo itashiriki katika hatua hiyo.