Viongozi ASEAN watakiwa kushirikiana kukabili vitisho, migogo | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.09.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi ASEAN watakiwa kushirikiana kukabili vitisho, migogo

Viongozi wakuu wa mataifa ya Kusini-Masahriki mwa Asia ASEAN,wametakiwa kushirikiana zaidi kukabiliana na vitisho vya ugaidi, mabadiliko ya tabianchi na masuala yanayowagawa kama vile mgogoro wa bahari ya China Kusini.

Akiufungua rasmi mkutano huo, rais wa Laos Bounnhang Vorachit, amesema kuna haja kwa wao kushirkiana kwa karibu kufuatilia matukio na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa mataifa ya jumuiya hiyo ya ASEAN na pia kushirikiana na jumuiya ya kimataifa. Viongozi wa mataifa yanaounda jumuiya ya mataifa ya kusini-Mshariki mwa Asia ASEAN, walikuwa wanakutana mjini Vientiane kwa Mkutano wao wa kilele wa kila mwaka, ambao umehudhuriwa pia na Rais wa Marekani Barack Obama kwa mara mwisho.

"Changamoto mbalimbali za kiusalama zimetokea katika sehemu nyingi za dunia katika muundo wa ugaidi na itikadi kali, majanga ya asili, mabadiliko ya tabianchi, mgogoro wa wakimbizi, usafirishaji binaadamu kimagendo, migogoro ya maeneo na migogoro ya kivita. Wakati huo huo, ingawa uchumi wa dunia umefufuka taratibu, kasi ya ukuaji imeendelea kuwa ndogo na tete, Kwa kuzingatia hayo yote, kuna haja kwetu kufuatilia matukio hayo kwa karibu na kuendelea kuimarisha ushirikiana kati ya mataifa waanachama wa ASEAN," alisema rais Vochit.

Rais wa Ufilipino akiungana na wenzake kwa ajili ya picha ya kumbukumbu mjini Varientiane, Laos.

Rais wa Ufilipino akiungana na wenzake kwa ajili ya picha ya kumbukumbu mjini Varientiane, Laos.

Wasiwasi kuhusu China

Kulingana na muswada wa taarifa ambayo itatolewa bmwishoni mwa mkutano, viongozi hao walitarajiwa kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusiana na hatua za China kufukia sehemu ya bahari ya China Kusini kwa ajili ya matumizi yake mengine. Lakini katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya kidiplomasia kwa China, viongozi hao hawakutarajiwa kuitaja rasmi hukumu iliyotolewa mwezi Julai na mahakama ya kimataifa ya utatuzi wa migogoro, kwamba China haikuwa na haki ya kisheria kudai umiliki wa sehemu kubwa ya eneo hilo la bahari. China iliipinga huku hiyo na kuitaja kuw ani batili.

Kabla ya mkutano huo, Ufilipino iliona kuwa huenda China inajipanga kuanza ujenzi mwingine katika bahari ya China Kusini, baada ya meli 10, zikiwemo nne zinazoonekana kama mashua kubwa, zilizoonekana karibu na kisiwa cha Huangyan. "Hili ni jambo la kutia wasiwasi kwa sababu ni kisiwa chetu", waziri wa ulinzi Lorenzana aliwambia waandishi wa habari mjini Vientinane, na kuongeza kuwa ikiwa China itafanikiwa kujenga majengo kisiwani hapo watakuwa hawawezi tena kukirejesha.

Obama kuwarai viongozi ASEAN

Rais Obama alitarajiwa kuibua shuala hilo na viongozi wa ASEAN na kujadili haja ya kutatua mgogoro wa kieneeo chini cha sheria ya kimataifa kulinga na taarifa iliyotolewa na ikulu ya White House. Pia alitarajiwa kuwahakikishia viongozi wa kanda ya Kusini-Mashairki mwa Asia juu ya dhamira ya Marekani kwa kanda hiyo wakati wa ziara yake nchini Laos, ya kwanza kwa rais wa Marekania alieko madarakani.

Rais wa Marekani Barack Obama akiongozwa na mwenyeji wake rais wa Laos Bounnhang Vorachit baada ya kuwasili Laos.

Rais wa Marekani Barack Obama akiongozwa na mwenyeji wake rais wa Laos Bounnhang Vorachit baada ya kuwasili Laos.

Jumuiya ya ASEAN yenye nchi wanachama 10 inazijumlisha nchi za Brunei,Cambodia, Indonesia, Laos, Malaysia, Myanmar, Ufilipino, Singapore, Thailand na Vietnam. Mkutano wa leo utafuatiwa na mikutano kadhaa mingine kesho Jumatano, na mkutano wa kile siku ya Alhamisi kati ya viongozi kutoka ASEAN an mataifa mengine yakiwemo Marekani, China, Urusi, India, Korea Kusini, Japan, Australia na New Zealand.

Mmwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com