Vikwazo vipya dhidi ya Iran
26 Oktoba 2007Matangazo
Vikwazo vilivyotangazwa na Waziri wa Nje wa Marekani,Condoleezza Rice na Waziri wa Fedha Henry Paulson mjini Washington,vinalenga benki tatu za Iran,makampuni tisa yanayohusika na petroli,ujenzi na usafiri yanayodhibitiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi-IRGC.
Condoleezza Rice amesema,vikwazo hivyo humaanisha hakuna raia au shirika binafsi la Kimarekani litakaloruhusiwa kuwa na shughuli za kibiashara pamoja na hao waliotajwa.Na mali yao iliyo chini ya mamlaka ya Marekani,itazuiliwa moja kwa moja.
Kwa upande mwingine,Rais wa Urusi,Vladimir Putin amesema,vikwazo vipya vya kimataifa dhidi ya Iran vitazidi kuchafua hali ya sasa.Iran,mara kwa mara imesisitiza kuwa mradi wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani tu.