1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikwazo vikali dhidi ya Iran

Miraji Othman10 Juni 2010

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuiwekea Iran vikwazo vilivyo vikali zaidi.

https://p.dw.com/p/NmpN
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapiga kura kuiwekea vikwazo IranPicha: AP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuiwekea Iran vikwazo vilivyo vikali zaidi. Kama hatua hiyo itautanzua mzozo wa kinyukliya baina ya nchi hiyo na nchi za Magharibi ni jambo la ati ati, na pia kama litausaidia upinzani katika nchi hiyo. Usikilize uhariri ulioandikwa na Daniel Scheschkewitz, unaosomwa studioni na Othman Miraji...

Naam, tena vikwazo vingine. Kutokana na uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika siku za mbele itakuwa marufuku kwa Iran kununua kutoka nchi za nje vifaru, helikopta za kijeshi, manuwari na mifumo ya maroketi. Pia inapangwa kuwekwa vizuizi vya kusafiri maafisa wa nchi hiyo, kuzizuwia akaunti za benki za nchi hiyo pamoja pia na kuweka vikwazo vya kibiashara kwa zaidi ya makampuni na taasisi 40 zinazoshiriki katika mipango ya kinyukliya au ya maroketi ya huko Iran. Vikwazo hivyo kwanza vimeelekezwa kwa walinzi wa jeshi la mapinduzi, nguzo muhimu ya utawala wa Iran.

Kinachofaa kukaribishwa ni kwamba jamii ya kimataifa imedhihirisha inaweza kuchukuwa hatua kuelekea programu ya kinyukliya ya Iran, lakini kuna wasiwasi juu ya kufanikiwa vikwazo hivyo.

Katika mabishano kuhusu programu ya kinyukliya ya Iran, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu hapo, tena kwa mara kadhaa, limewahi kuweka vikwazo dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu, lakini bila ya kuweza kuufanya utawala wa Tehran ubadilishe msimamo wake. Si vikwazo vya kiuchumi ambavyo kichinichini pia vilikuwa ni kitisho cha kutaka kuubadilisha utawala wa Tehran- siasa iliofuatwa na mtangulizi wa Rais Obama- yaani George Bush- wala mbinyo hafifu katika mashauriano uliokuwa unawekwa na nchi za Ulaya umeweza hadi sasa kuifanya Iran ibadilishe siasa yake. Bado Rais Ahmedinedschad anashikilia kutaka kusafisha madini ya Uranium ndani nchini mwake na anawakataza wakaguzi wa Shirika la Nishati ya Kinyukliya la Umoja wa Mataifa, IAEA, kuingia wanakotaka katika vinu vya kinyukliya vya Iran.

Sasa skurubu inakazwa zaidi kwa kutumiwa hivyo vinavoitwa vikwazo vya busara, ambavyo havitawatia kabari wananchi, lakini vitawagusa hasa wawakilishi wa utawala wa Tehran na wale wanaofaidika nao. Ukweli ni kwamba huko Iran, licha ya mashehe, wale walio muhimu madarakani ni wafanya biashara walio mabwanyenye. Kuwawekea vikwazo vya kusafiri watu hao na kuwekwa vizuwizi vya kusafiriasha fedha huku na kule kunaweza kuwa ni tatizo kwa watu hao. Viongozi wa Iran yaonesha wamekasirishwa na maamuzi hayo na wameashirishia kwamba watakomesha kufanya mashauriano juu ya mpango wake wa kinyukliya na pia wataachana kushirikiana kwa aina yeyote na wakala wa kimataifa juu ya nisahti ya kinyukliya, IAEA.

Vikwazo, lakini, vina nafasi tu ya kufanikiwa ikiwa havitakuwa ni lengo la mwisho, bali viwe ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu. Kwa sasa mkakati huo hauonekani. Ni kawaida kwa tawala za kiimla kutoipigia magoti mibinyo ya kisiasa, hata kama mibinyo hiyo itapelekea hali ya uchumi iwe mbaya katika nchi. Pia huko Tehran watu wanajuwa fika kwamba Russia na China hazina hamu ya kutia mafuta zaidi juu ya moto juu ya mzozo huo. Na pia Rais Barack Obama, kinyume na mtangulizi wake- George Bush- havutiwi na fikra ya kufuatiliza mbinyo wake wa kidiplomasia na harakati za kijeshi. Na kutokana na kutokuweko masikilizano hivi sasa katika uhusiano baina ya Israel na Marekani, haitazamiwi kwamba Marekani itatoa kibali kwa Israel ivishambulie vinu vya kinyuliya vya Iran.

Rais Ahmedinedschad hivi sasa ana matatizo makubwa zaidi kuliko hivyo vikwazo vilivoamuliwa dhidi ya nchi yake. Ikiwa ni siku chache kabla ya kukumbukwa mwaka mmoja tangu kukandamizwa kikatili vuguvugu la upinzani la Iran, kuna kimya cha kama shetani anapita katika nchi hiyo. Utawala wa nchi hiyo umeamua kabisa mnamo siku za mbele kuyazima maandamano yeyote na kuwafumba midomo wapinzani. Vikwazo kwa kweli havitawasaidia zaidi watu wanaopigania demokrasia huko Iran, hasa kwa vile katika azimio liliopitshwa jana kumekosekana kabisa kutajwa kwa vyovyote hali ya haki za wananchi katika nchi hiyo.

Mwandishi: Scheschkewitz, Daniel /ZPR/Miraji Othman

Mhariri: Mohammed Abdulrahman