1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yawazuia wahamiaji kuvuka bahari ya Aegean

Bruce Amani
7 Machi 2020

Rais Recep Tayyip Erdogan amewaamuru walinzi wa pwani wa Uturuki kuwazuia wahamiaji kuhatarisha maisha yao kwa kuvuka Bahari ya Aegean

https://p.dw.com/p/3Z1ip
Griechenland Flüchtlingsboot an der Küste von Lesbos
Picha: Reuters/A. Konstantinidis

Maelfu ya wahamiaji wamekusanyika katika mpaka wa ardhi kati ya Uturuki na Ugiriki baada ya Rais Erdogan kusema wiki iliyopita kuwa Uturuki haitawazuia wahamiaji kuhamia nchi za Umoja wa Ulaya, na kuzusha machafuko na kuongezeka mgogoro kati ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Walinzi wa pwani wa Uturuki wameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa "kwa maagizo ya rais…ruhusa haitatolewa kwa wahamiaji kuvuka bahari ya Aegean kwa sababu ni hatari.”

Hata hivyo wamesema sera ya Uturuki ya kuwaruhusu wahamiaji na wakimbizi kuhamia nchi nyingine haijaguswa, na kuwa maelekezo ya rais yalihusu tu safari za baharini.

Rauchbomben und Tränengas an griechisch-türkischer Grenze
Makabiliano yalizuka kati ya wahamiaji na vikosi vya usalama kwenye mpaka wa Uturuki na UgirikiPicha: Reuters/H. Aldemir

Uturuki na Umoja wa Ulaya zinatupiana lawawa, huku Ankara ikiiambia Brussels kuutekeleza mpango wa uhamiaji wa mwaka wa 2016, na umoja huo ukidai kuwa Ankara inawatumia wahamiaji kwa madhumuni yao ya kisiasa.

Wakati wa vuta nikuvute ya Jumamosi iliyodumu kwa masaa kadhaa, polisi wa Ugiriki walitumia gesi ya kutoa machozi na mizinga ya maji ya kuwasha dhidi ya wahamiaji waliojaribu kuvunja uzio kwenye mpaka wa mkoa wa Edirne, kwa mujibu wa wanahabari wa AFP. Wahamiaji walijibu kwa kuwarushia mawe wakisema kwa sauti kubwa "Fungueni malango”. Vikosi vya usalama vya Uturuki pia vilijibu kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi.     

Wakati huo huo Rais Erdogan anapanga kuwa Brussles Jumatatu ijayo kwa ajili ya ziara ya siku moja ya kikazi. Taarifa kutoka ofisi ya Erdogan imesema atakwenda Brussels Machi 9. Taarifa hiyo haikufafanua atakakokwenda wakati wa ziara yake ya siku moja au aina ya kazi inayompeleka katika mji huo mkuu wa Ubelgiji, lakini Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya yako mjini Brussels.

Tangazo hilo limekuja saa chache tu baada ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja wa Ulaya wanaokutana nchini Croatia kuikosoa Uturuki Ijumaa, wakisema inawatumia wahamiaji waliokata tamaa kwa ajili ya manufaa yao ya kisiasa.