Usalama wa Ujerumani chini ya sera ya milango wazi | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Usalama wa Ujerumani chini ya sera ya milango wazi

Mwaka mmoja uliopita Ujerumani ilijipambanua kama nchi ya msaada. Maswala ya usalama wakati huo hayakuwa na umuhimu. Lakini hii leo imedhihirika kwamba njia za wakimbizi zilitumiwa vibaya na wafuasi wa itikali kali.

1608-19-DW-Wir-schaffen-das-Teaser-DEU.png

Wakati akiruhusu mipaka ya Ujerumani ifunguliwe kwa wakimbizi, Kansela Angela Merkel alisema: Wir Schaffen das (tunaweza kumudu hilo). Je, alikuwa sahihi?

Kuwasili kwa maelfu ya wakimbizi katika majira ya mapukutiko mwaka 2015 hakuna uhusiano wowote na mashambulizi ya Wuerzburg na Ansbach mwezi Julai mwaka huu. Washambuliaji wote walikuwa tayari wapo Bayern kabla ya hapo.

Lakini ukweli tu kwamba washambuliaji hao walipokelewa Ujerumani, na baadae kuwageukia watu waliowasadia kwa kuwashambulia na shoka na mabomu, umemulika upande unaotatiza wa uhamiaji. Leo hii wengi wanajiuliza, ni watu gani wanapenda bado kujichanganya na wakimbizi? Nini kitatokea tena?

Mwaka uliopita majibu ya maswali hayo kutoka kwa vyombo vya usalama na wawakilishi wa serikali yalikuwa ni uhakikisho: kwamba kwa magaidi haileti maana kujichanganya na wakimbizi kuja Ujerumani. Waliamini njia ya Balkan ilikuwa ndefu sana kwa magaidi kuweza kupoteza muda wao kuitumia.

Deutschland Saudi Arabien verspricht Unterstützung nach Anschlag in Ansbach

Mashambulio kama la mjini Ansbach yamezusha maswali kuhusu iwapo Ujerumani ilikuwa sahihi kupokea maelf ya wakimbizi.

Mbali na uhalisia

Lakini leo hii tunajua kuwa uhakikisho huu haukuwa sahihi. Katika ripoti ya usalama wa taifa, mkuu wa shirika la usalama wa ndani Hans-George Maassen, alielezea ushahidi wa kuwepo na karibu magaidi 17 walioingia barani Ulaya kupitia njia ya Balkan. Zaidi ya hayo, kulingana na ofisi ya shirikisho ya kupambana na ugaidi, zaidi ya taarifa 400 zimetolewa kwa idara za usalama kwamba miongoni mwa wakimbizi wapo wapiganaji, wasaidizi na wafausi wa makundi ya kigaidi. Mwanzoni mwa mwezi Agosti, kulikuwepo na visa 62 vinavyochunguzwa.

Guido Steinberg kutoka taasisi ya uchumi na siasa ya Ujerumani aliiambia DW katika mahojiano kuwa, kabla ya majira ya mapukutiko ya mwaka 2015, haikuwa rahisi kuingia barani Ulaya. Bila shaka magaidi walikuwa wanaweza kutumia pass bandia ambazo ni ghali mno na mara nyingi pasi hizo hugundulika mipakani.

Lakini mwaka 2015, watu wenye uwezekano wa kuwa magaidi walikuwa na kazi moja ya kuvuka mpya na kuingia Ugiriki. Baada ya hapo mipaka ilikuwa wazi karibu bila ukaguzi wa vitambulisho, na kujua maisha yao ya nyuma. Mwanya huo ulitumiwa na kundi la kigaidi la Dola la Kiislamu, anasema mtaalamu wa ugaidi Steinberg.

Kwa vyovyote vile, njia hiyo inayojulikana kama Balkan iligunduliwa na Waislamu wenye itikadi kali na kutumiwa ipasavyo. Ukweli huu unadhihirika katika kisa cha Bilal C. ambaye mwendesha mashitaka mkuu wa serikali alimfungulia mashitaka mwezi Juni.

Wachunguzi wanaamini kwamba Mualgeria huyo alikuwa na mawasiliano na Abdelhamid Abaaoud, mmoja wa washukiwa wakuu wa mashambulizi ya Paris Novemba 13, 2015. Wanaamini Abaaoud alimpa kazi Bilal C. kuchunguza njia ya Balkan katika mukhtadha wa ukaguzi mipakani, na fursa za magendo. Kulingana na ushahidi uliopo, wawili kati ya washambuliaji wa Paris walipitia Ujerumani.

Deutschland Merkel und Seehofer

Merkel amekuwa akikwaruzana na mshirika wake wa Karibu, waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer (kulia), kutokana na suala la wakimbizi.

Wengine ambao hawakuendelea na safari yao na kuamua kubakia nchini Ujerumani ni Wasyria wawili Saleh A. na Hamza C. ambao waliingia nchini majira ya kiangazi mwaka 2015 kupitia Uturuki na Ugiriki. Wakiwa nchini Ujerumani wawili hao walishirikiana na Wasyria wengine wawili kupanga njama ya shambulio kubwa katika mji wa zamani wa Düsseldorf. Mmoja wa washukiwa hao wa kundi la Dola la Kiislamu alikamatwa wakati alipokwenda kuchukuwa fedha zake za msaada wa kiserikali katika eneo lake alikosajiliwa kama mkimbizi la Brandenburg.

Europol yaonya juu ya wakimbizi kujasiliwa na wapiganaji

Picha za operesheni za polisi na makaazi ya wakimbizi yaliyozingirwa zinajitokeza pia katika maeneo yanayoizunguka miji ya Wuerzburg na Ansbach. Kwa wakimbizi walio wengi, ni jambo la kuogofya kwamba wachokozi waliotaka kuwatoroka huenda walijichanganya miongoni mwao.

Lakini shirika la polisi ya Ulaya Europol, linaonya pia kwamba wakimbizi mmoja mmoja pia wanaweza kuvutika kirahisi na mawazo ya itikadi kali. Shirika hilo linasema kuna hatari kubwa kwamba huenda wakimbizi wa Syria wakageuka shabaha ya uandikishaji wa makundi ya itikadi kali.

Hata idara ya ujasusi wa ndani inaona hatari hiyo. Rais wake Maassen anaonya dhidi ya kile alichokiita "Misikiti ya uani." Shirika hilo la ujasusi linaeleza kuwa makundi ya kisalafi yamekuwa yakielekeza ujumbe wao kwa wakimbizi.

Shirika hilo linadai kuwa makundi hayo ya Kisalafi yanajaribu kuwavutia wakimbizi katika itikadi yao kwa kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku. Hata Thomas Muecke kutoka mtandao wa kuzuwia vurugu VPN, alionya juu ya kampeni ya makundi ya wafuasi wa msimamo mkali kuwavutia wakimbizi.

Symbolbild Deutschland Flüchtlinge Bildung

Wakimbizi wakishiriki mafunzo ya ujumuishwaji katika jamii mjini Berlin.

Muecke anasema kwa wakimbizi hasa wenye umri mdogo inahitajika kazi kubwa kuwaweka sawa na kufanya kila liwezekanalo kuwashirkisha katika jamii. "Tunahitaji kuwabadilisha vijana hao, maana tusipofanya hivyo makundi ya itikadi kali yatawabadili. Na kisha vijana hao watawekwa katika mazingira ambapo hawawezi kufikiwa tena kutoka nje," alisisitiza Muecke. Ikiwa hilo halitofanyika, hatari ya kujazwa itikadi kali itakuwa kubwa pale vijana hao watakapokatishwa tamaa na maisha.

Wakimbizi wanaweza kulinda Ujerumani

Wakati hatari za kiuslama zimekuwa zikielezwa kutoka kila upande, hivi karibuni wamejitokeza wataalamu ambao katika sera ya wakimbizi, wanaiona fursa ya kuwepo na usalama zaidi nchini Ujerumani. Mwandishi wa vitabu wa Kiingereza Robert Verkaik, alieandika kitabu cha "Jihad John", anaaamini kwa kuwapokea mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Kiarabu, Ujerumani imejiwekea kinga ya muda mrefu dhidi ya mashambulizi ya kigaidi.

Vervaik aliandika katika gazeti la Independent la nchini Uingereza, kwamba serikali ya Kansela Angela Merkel na raia wa Ujerumani wameonyesha kupitia mshikamano wao na wakimbizi, kwamba Ujerumani haipigi vita Uislamu. Waislamu nchini humo hivyo wanaweza kushirikiana kama hatua ya shukrani, na vyombo vya usalama kuwaondoa miongoni mwa watu wenye itikadi kali.

Thomas de Maiziere PK Bombenexplosion Ansbach

Waziri wa Mambo ya ndani Thomas de Maiziere anataka kuwashikirisha wakimbizi kubaini wahalifu miongoni mwao.

Mtazamo kama huo pia anao mshauri wa zamani wa usalama wa ndani katika utawala wa rais George W. Bush nchini Marekani (2004 - 2007) Frences Townsend. Townsen ambaye kwa sasa ni mkurugenzi wa mradi wa kupambana na itikadi kali, anaamini kuwa Wasyria waliotoroka vita wanaweza kuwa chanzo cha upashaji habari kwa idara ya ujasusi.

Matamashi ya "Wakimbizi wachache, Uwezekano mdogo wa ugaidi" bado yanakosa usahihi kwa sababu nyingine. Katika kambi za wakimbizi ndani na nje ya Syria kitisho cha itikadi kali ni kikubwa zaidi kuliko ilivyo barani Ulaya. Hivyo kuchukuliwa kwa wakimbizi barani Ulaya kutalipokonya kundi la IS uwanja mpana wa kusajili wapiganaji.

Hata waziri wa mambo ya ndani amedokeza kuhusu uwezekano wa kushirikiana na wakimbizi wakati akiwasilisha mipango yake ya hivi karibuni. Katika mapambano dhidi ya itikadi kali na ugaidi, waziri Thomas de Maiziere amejumlisha miongoni mwa mambo mengine, ushirikiano na wakimbizi. Kupitia ushirikiano huo, wakimbizi walio na taarifa juu ya washukiwa na uhalifu miongoni mwao, wanaweza kuziwasilisha kwa mamlaka za usalama.

Mwandishi: Fabian von der Mark

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com