Urusi na Ukraine zashindwa kukubaliana | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi na Ukraine zashindwa kukubaliana

Mazungumzo kati ya rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzako Petro Poroshenko wa Ukraine yamemalizika bila ya kuonyesha kuwa na suluhu ya mgogoro unaoendelea Ukraine. Viongozi hao walikutana Belarus.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa marais wa Ukraine na Urusi kukutana uso kwa uso tangu mwezi Juni. Walikuwa mjini Minsk wakihudhuria mkutano wa kikanda. Mada muhimu iliyozungumziwa ulikuwa mgogoro unaoendelea Ukraine ya mashariki. Rais Petro Poroshenko alisema kuwa mkutano ulikuwa na maana kubwa sana: "Leo, bila shaka hatma ya Ulaya na ulimwengu kwa ujumla itaamuliwa Minsk. Lazima tutafute suluhu sahihi itakayoleta amani katika bara letu," alisema Poroshenko.

Putin alikutana na Poroshenko katika kasri la uhuru, jengo la kifahari kabisa mjini Minsk. Wanasiasa hao walipeana mikono kwa kifupi, lakini bila ya kukaribiana. Marais wa Belarus, Kazakhstan na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya nao walishiriki kwenye kikao hicho. Walikaa kwenye meza ya duara, Putin na Poroshenko wakitazamana.

Mapigano yaendelea Ukraine Mashariki

Mwanajeshi wa Ukraine akipambana na waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine

Mwanajeshi wa Ukraine akipambana na waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine

Punde kikao kilipoanza ilikuwa wazi kwamba yapo maeneo mengi ambayo Urusi ina mtazamo tofauti na Ukraine. Rais Poroshenko alisisitiza kwamba ni lazima Urusi iache kupeleka silaha kwa waasi walioko Ukraine Mashariki ili vita vikome katika eneo hilo. "Nina uhakika kwamba hakuna anayetaka vita wala anayetaka raia wa Ukraine wazidi kuuwawa," alisema Poroshenko. "Angalieni mlichotufanyia: Magaidi wanadungua ndege zenye raia wasio na hatia kutoka nchi tofauti. Nimekuja Minsk kufanya kila linalowezekana ili umwagikaji damu ukome na ili tupate suluhu ya kisiasa."

Putin kwa upande wake alizungumzia zaidi masuala ya kiuchumi. Alielezea wasiwasi wake juu ya mapatano kati ya Umoja wa Ulaya na Ukraine. Ni mapatano yanayoruhusu biashara huru, jambo litakaloilazimisha Ukraine ifuate viwango vya ubora vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya. Putin alisema kuwa makubaliano hayo yataiathiri nchi yake. "Tunawaelewa washirika wetu wa Ulaya. Wameshaingia kwenye sehemu ya soko la Ukraine na sasa wanataka kusambaa nchi nzima. Na wanataka kuwafukuza wapinzani wote. Nadhani bidhaa zisizo na ubora zitaishia kuuzwa Urusi," alisema Putin.

Poroshenko alimhakikishia Putin kwamba biashara huru kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya hautakuwa na athari mbaya kwa Urusi. Badala yake itaimarisha biashara kati ya Ukraine na Urusi. Lakini wakati viongozi hao wakijaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia, nchini Ukraine mapigano bado yanaendelea.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/wdr

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com