1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi kuridhia taarifa ya pamoja mkutano wa G20 ukimalizika

John Juma APE, DPAE, RTRE
15 Novemba 2022

Washiriki wakuu katika mkutano huo wakiwemo wawakilishi wa Urusi, wamekubaliana kuwa baada ya mkutano huo watakuwa na maafikiano ya pamoja. Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Ulaya Charles Michel amethibitisha hayo Jumanne.

https://p.dw.com/p/4JXEq
Indonesien Bali | G20-Gipfel | Themenbild | Justin Trudeau, Kanada
Picha: Willy Kurniawan/REUTERS

Mkutano wa kilele wa G20, kundi la nchi tajiri zaidi ulimwenguni na zinazoinukia kiviwanda umeanza rasmi Jumanne katika kisiwa cha Bali nchini Indonesia. Rasimu inayojadiliwa, inaangazia zaid msimamo wa Umoja wa Mataifa wa kuilaani Urusi kufuatia vita vyake nchini Ukraine, lakini pia inatambua mitizamo tofauti miongoni mwa wanachama.

Viongozi wa mataifa hayo 20 tajiri na yanayoinukia kiuchumi ulimwenguni, wangali wamegawika kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, lakini wanaonekana kuwa tayari kutuma ujumbe mkali kulaani vita hivyo ambavyo vimedumu kwa miezi tisa sasa na ambavyo vimeiathiri Ukraine na kusababisha bei ya vyakula na nishati kupanda juu zaidi ilimwenguni kote.

Rasimu hiyo ambayo shirika la habari la Associated Press limepata nakala yake, imetumia maneno makali  kuhusu uchokozi wa Urusi, na inaitaka nchi hiyo kuwaondoa wanajeshi wake kikamilifu nchini Ukraine bila masharti. Inasisitiza msimamo sawa na uliochukuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Machi 2.

Rasimu inayojadiliwa kwenye mkutano wa G20 inalenga msimamo wa Umoja wa Mataifa kulaani vita vya Urusi nchini Ukraine.
Rasimu inayojadiliwa kwenye mkutano wa G20 inalenga msimamo wa Umoja wa Mataifa kulaani vita vya Urusi nchini Ukraine.Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Kulingana na taarifa ya shirika la habari la kijerumani DPA, licha ya Urusi hapo awali kupinga kuwa sehemu ya taarifa ya pamoja, mataifa ya Magharibi yalifanikiwa kupitisha kipengee cha kulaani vita dhidi ya Ukraine kwenye rasimu hiyo.

Hatua ya Urusi kuidhinisha rasimu hiyo inaonekana kama ishara kwamba huenda imepoteza uungwaji mkono hata kutoka kwa mshirika wake China kuhusu vita vyake kraine.

Viongozi wa G20 wawasili Bali kwa mkutano wa kilele

Awali, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anayemwakilisha Rais Vladimir Putin kwenye mkutano huo alisema, wataikubali taarifa ya pamoja baada ya mkutano huo kumalizika.

Mikutano ya pembezoni

Mikutano mingine kadhaa pia imefanyika pembezoni mwa mkutano wa kilele ukiwemo mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mapema Jumanne.

Msemaji wa wizara hiyo ya Urusi Maria Zakharova alichapisha picha ya viongozi hao wakiwa wameketi pamoja, lakini bila ya kutoa taarifa zaidi.

Biden na Xi washinikiza ushirikiano katika mkutano wao Bali

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenzake wa China Xi Jinping pwamekubaliana kwamba kuna haja ya dharura ya kumaliza machafuko nchini Ukraine. Kulingana na ikulu ya rais nchini Ufaransa, viongozi hao wamesisitiza misimamo yao ya awali ya kuzuia matumizi ya zana za nyuklia kwenye machafuko hayo. Wamesema hayo walipokutana pembezoni mwa mkutano wa kilele unaofanyika  Bali nchini Indonesia.

Xi na Macron wamesisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wa Ukraine. Kulingana na taarifa kutoka ikulu ya Macron, viongozi hao wamekubaliana kwamba ipo haja ya dharura kusitishwa machafuko nchini Ukraine.

Xi alisema China na Ufaransa zinapaswa kuimarisha ushirikiano na zikuze maendeleo lakini pia ziheshimu masilahi binafsi ya kila upande.

Awali rais wa China Xi Jinping alikutana na rais wa Marekani Joe Bidenna wakaahidi kuacha malumbano na wafanye kazi kwa ushirikiano kupunguza tofauti kati ya nchi hizo mbili.

Volodymyr Zelensky ataka Urusi ikomeshwe

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Ukraine Presidency/IMAGO

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliungana na rais wa Marekani Joe Biden katika kujaribu kuwashawishi viongozi wa G20 kuitenga Urusi zaidi kidiplomasia na kiuchumi, licha ya mgogoro wa kifedha unaozidi kuongezeka ulimwenguni.

"Ninataka vita hivi vya uchokozi kutoka Urusi kumalizika kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa na kulingana na sheria ya kimataifa. Hatutairuhusu Urusi kusubiri na kuimarisha vikosi vyake na kuanza safu mpya ya ugaidi, uharibifu na kuvuruga utulivu wa ulimwengu. Ninaamini huu ndio wakati ambapo vita vya uharibifu vya Urusi vinaweza kukomeshwa,” alisema Volodymyr Zelensky.

Kando na Umoja wa Ulaya, mkutano huo wa siku mbili unazijumuisha Marekani, Ujerumani, Argentina, China, Ufaransa, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Saudi Arabia, Korea Kusini naAfrika Kusini