UNGA: Afrika yataka kiti UNSC, yaiunga mkono Palestina
24 Septemba 2025
Mwaka huu, viongozi wa Afrika wanaohudhuria Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA-80) wameingia New York na ajenda iliyo wazi: kupata sauti yenye nguvu zaidi katika uongozi wa dunia, kuendeleza amani na usalama, na kuhamasisha rasilimali kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Chini ya kaulimbiu "Tukiwa Pamoja: Miaka 80 na zaidi kwa ajili ya amani, maendeleo na haki za binadamu,” viongozi wa Afrika wanatarajiwa kusukuma mbele mpangilio wa dunia usio wa upendeleo, unaoakisi umuhimu wa kisiasa na kijiografia wa bara hili na kushughulikia historia ya kutengwa kwake.
Mkutano wa UNGA-80 umeanza Jumanne kwa hotuba za viongozi mashuhuri, akiwemo Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil na Rais wa Marekani Donald Trump. Hata hivyo, macho mengi yalielekezwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliyefungua mjadala akisisitiza umuhimu wa suluhu ya Gaza. Guterres alisema hali "ni ya kutovumilika na inazidi kuzorota kila saa,” akiongeza kuwa "utaifa wa Wapalestina ni haki, si zawadi. Bila mataifa mawili, hakutakuwa na amani Mashariki ya Kati, na misimamo mikali itasambaa kote duniani.”
Kauli hiyo imepokelewa kwa nguvu barani Afrika, ambako mataifa mengi tayari yametambua Palestina kwa muda mrefu. Wengi wanasema mapambano ya Wapalestina yanalingana na historia ya bara hili ya ukoloni na ukandamizaji.
Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele katika msimamo huu, ikisisitiza kuwa haitaweza kukaa kimya mbele ya machafuko ya Gaza. Rais Cyril Ramaphosa ametoa wito mara kadhaa kwa suluhu ya mataifa mawili na kuonya kwamba kuendelea kwa vita kunadhoofisha amani ya kimataifa.
Mageuzi ya Baraza la Usalama
Zaidi ya msimamo wa Gaza, viongozi wa Afrika pia wanataka marekebisho ya Baraza la Usalama la UN. Wanasema kwamba bara hili linatoa mchango mkubwa katika operesheni za ulinzi wa amani na maendeleo, lakini halina kiti cha kudumu kwenye chombo hicho muhimu cha maamuzi.
Kwa miaka mingi, hoja ya Afrika imekuwa kwamba mamlaka ya kura ya turufu inayotumiwa na Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China yamepoteza uhalali. Viongozi wanasema mfumo huo unakwamisha hatua za haraka za kimataifa hata pale sheria za kimataifa zinapovunjwa.
Miongoni mwa wachambuzi wanaochunguza suala hili ni Michael Kwadwo Nketiah, mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa. Alisema kuwa kuongeza viti vya kudumu si jambo rahisi, kwani "hata ili kuongeza kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN, lazima kuwe na marekebisho ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, na marekebisho hayo yanahitaji uungwaji mkono wa theluthi mbili ya wanachama.”
Nketiah aliongeza kuwa hata baada ya kupata uungwaji mkono wa wanachama 193, mabadiliko hayo yanahitaji pia kuridhiwa na wanachama watano wa kudumu — ambao mara nyingi hawana nia ya kugawana mamlaka yao na wengine.
Licha ya changamoto hizi, wachambuzi wanasema kuwa sauti ya Afrika inazidi kupata nguvu kutokana na ongezeko la ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi, pamoja na mchango wake mkubwa katika kulinda amani duniani.
Changamoto na fursa kwa bara la Afrika
Katika mijadala ya UNGA, viongozi wa Afrika pia waligusia changamoto za bara lao, ikiwemo mizozo ya Sahel, mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na changamoto za maendeleo endelevu. Hata hivyo, masuala haya hayapati nafasi kubwa sawa na migogoro ya Gaza au Ukraine.
Pamoja na changamoto hizo, viongozi wa Afrika wanatumia fursa ya mikutano ya pembeni ya UNGA kujadili biashara, uwekezaji, nishati na rasilimali adimu. Rais Félix Tshisekedi wa DRC, kwa mfano, aliendesha kongamano la "Invest in DR Congo” kutangaza madini ya kimkakati ya nchi yake.
Kwa ujumla, msimamo wa Afrika katika UNGA-80 umejikita kwenye hoja mbili kuu: kuhalalisha taifa la Palestina na kudai mageuzi ya Baraza la Usalama. Kwa bara lililoathiriwa kwa muda mrefu na historia ya kutengwa, huu ni wakati wa kuhakikisha kwamba sauti za Kusini zina nafasi sawa katika uongozi wa dunia.