1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitishia Marekani kuhusu biashara

Saumu Mwasimba
9 Machi 2018

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamtaka Trump aziepushe nchi zao na mpango wake wa viwango vya ushuru la sivyo watalipiza kisasi na kutanua uwanja wa vita vya kibiashara

https://p.dw.com/p/2u3Yu
USA Trump besiegelt Strafzölle auf Stahl und Aluminium
Picha: picture-alliance/abaca/O. Douliery

Umoja wa Ulaya unamatumaini ya kupata fursa ya kuepuka viwango vya ushuru katika mpango wa Marekani kuhusiana na biashara ya  bidhaa za chuma na bati.Matarajio ya Umoja wa Ulaya yametangazwa na maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja huo wakati ambapo naibu rais wa halmashauri ya Umoja huo Jryki Katainen akimshutumu rais Donald Trump wa Marekani kwamba anaendeleza hatua ya ubinafsi wa kibiashara.

Rais Trump alitia saini hapo jana mpango maalum wa kuweka viwango vya ushuru vya asilimia 25 dhidi ya biashara ya chuma na asilimia 10 katika bidhaa za bati akitumia sheria ya Marekani ambayo ni nadra kutumiwa  ili kumpa mamlaka kama rais kuchukua hatua dhidi ya biashara inayoingizwa Marekani ambayo inahujumu usalama wa taifa. Umoja wa Ulaya umeapa kulipiza kisasi ikiwa nchi za Umoja huo zitaguswa na mpango huo hali ambali inaongeza uwanja wa vita vya kibiashara. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel baada ya kukutana na viongozi wa kiviwanda  katika nchi hiyo kubwa kiviwanda katika Umoja wa Ulaya amesema kwamba pamoja na Marekani kuchukua hatua hiyo Umoja wa Ulaya lazima utoa kwanza nafasi ya kufanyika mazungumzo ingawa amesisitiza itakuwa busara ikiwa Marekani itaziepusha katika mpango huo nchi za Umoja wa Ulaya.

Symbolbild Handelskrieg USA und EU
Picha: Imago/Ralph Peters

Marekani yatangaza vita vya biashara Ulaya?

Mpango wa kuweka viwango vya ushuru katika biashara za kutoka nje nchini Marekani ambao umezusha wimbi la kauli za kuilaani nchi hiyo ni suala linalotarajiwa kuugubika mkutano uliopangwa muda mrefu utakaofanyika siku ya Jumamosi kati ya kamishna wa masuala ya biashara wa Umoja wa Ulaya Cecilia Malmstrom,mwakilishi wa masuala ya kibiashara wa Marekani Robert Lighthizer na mwenzao kutoka Japan Hiroshige Seko. Katika mkutano huo Umoja wa Ulaya utataka kupata maelezo zaidi kuhusiana na mpango huo kwa mujibu wa Malmstrom ambaye amesema kwamba bado suala hilo halijaeleweka vizuri ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu kile kilichoamuliwa na rais Donald Trump. 

Mpango huo wa Marekani kimsingi unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika kipindi cha wiki mbili zijazo na Umoja huo wa Ulaya umesema kupitia kamishna wake kwamba unatarajia kutojumuishwa kwenye mpango huo mpya wa viwango vya ushuru wa Marekani. Kamishna wa Umoja wa Ulaya ambao ni mshirika wa Marekani amesema kwamba Umoja wa Ulaya hauwezi kuwa ni kitisho kwa usalama wa taifa wa Marekani na kwahivyo haustahili kuwa miongoni mwa wanaoguswa katika mpango huo.

Juu ya hilo naibu rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Katainen amesema kwa mtazamo wake hotuba ya rais Trump alipozungumzia kuhusu usalama wa kiuchumi Marekani kilichodhihirika ni kwamba rais huyo amelenga zaidi katika kuiweka Marekani mbali na ushindani wa kibiashara:Kutokana na hilo kamishna wa masuala ya biashara wa Umoja huo anasema ikiwa Ulaya itaguswa na mpango huo wa viwango vipya vya ushuru katika bidhaa zake zinazoingizwa Marekani basi hapana shaka Umoja huo utakuwa tayari kupiza kisasi katika kipindi cha siku 90 kwa mujibu wa kanuni za shirika la biashara duniani WTO: Mpaka sasa tayari nchi wanachama 28 wa Umoja wa Ulaya zimeshatishia uwezekano wa kuchukua hatua za kuujibu mpango wa Marekani.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman