1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa walaani mashambulizi ya Yemen

22 Januari 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika gereza moja nchini Yemen ambalo limewaua takribani watu 70.

https://p.dw.com/p/45wQf
UN-Generalsekretär António Guterres
Picha: AFP/UN/M. Garten

Guterres amesema shambulizi hilo limevuruga huduma za mawasiliano ya intaneti kwenye nchi hiyo iliyoharibiwa na vita. Pia amelaani shambulizi la Jumatatu lililofanywa na waasi wa Houthi mjini Abu Dhabi na kuwaua watu watatu.

Shirika la misaada la Save the Children limesema mashambulizi hayo yametokea Ijumaa kwenye eneo la Saada linalodhibitiwa na waasi wa Houthi pamoja na shambulizi kwenye kituo cha mawasiliano katika bandari ya Hodeida na kuwaua watoto wapatao watatu.

Sheria za kimataifa zizingatiwe

 ''Imeelezwa kuwa watoto walikuwa wakicheza kwenye uwanja wa mpira wa miguu uliokuwa karibu na kituo hicho wakati shambulizi lililopotokea,'' lilieleza shirika la Save the Children.

Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Guterres amezikumbusha pande zote kwamba sheria za kimataifa za kibinaadamu zinapiga marufuku mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia.

''Amezikumbusha pande hizo wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinaadamu kuhakikisha kwamba raia wanalindwa dhidi ya hatari zinazotokana na operesheni za kijeshi, kwa kuzingatia kanuni za uwiano, tofauti na tahadhari,'' ilifafanua taarifa hiyo.

Jemen Saada Zerstörung Gefängnis durch Luftangriff
Gereza lililoshambuliwa Saada, YemenPicha: Ansarullah media center/AFP

Mashirika manane ya kutoa misaada yanayoendesha shughuli zake nchini Yemen yamesema katika taarifa ya pamoja kwamba yameshtushwa na taarifa za mauaji ya watu hao, wakiwemo wahamiaji, wanawake na watoto na kuyapuuza waziwazi maisha ya raia. Wamesema gereza hilo la Saada lilikuwa likitumika kama kituo cha kuwahifadhi wahamiaji, ambao ndiyo wengi waliouawa.

Ahmed Mahat, mkuu wa shirika la madaktari wasio na mipaka nchini Yemen, amesema kuna miili mingi bado iko kwenye eneo la tukio la mashambulizi ya anga na watu wengi hawajulikani waliko. Mahat anasema sio rahisi kubaini idadi ya watu waliouawa kwa sasa.

Guterres: Mashambulizi yasitishwe

Akizungumza na waandishi habari mjini New York, baada ya hotuba yake ya mwaka mpya kuhusu hali ya kimataifa kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Guterres ameliita shambulizi la waasi wa Houthi katika Umoja wa Falme za Kiarabu kama la kusitikisha na kwamba ni kosa kubwa. Amesema kuendelea kwa hali ya mashambulizi inabidi isitishwe mara moja.

Soma zaidi: Watu 11 wauawa kwenye mashambulizi Yemen

Amewakosoa waasi wa Houthi kwa kukataa kukutana na afisa wa Umoja wa Mataifa aliyekuwa akijaribu kufanya mazungumzo ya kusitisha ghasia hizo. ''Ni kosa kubwa sana kwa Houthi kukataa kumpokea mjumbe wetu maalum,'' alifafanua Guterres.

Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema wamekuwa wakiwasiliana kwa karibu na nchi mbalimbali ambazo zina uhusiano na waasi wa Houthi kujaribu kuelezea kwamba ni kwa maslahi yao na kwa ajili ya amani, mjumbe wao maalum ameweza kwenda Sanaa. Guterres amesema ana matumaini kwamba mkutano huo utafanyika hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken ametoa wito wa kupunguzwa kwa mashambulizi nchini Yemen baada ya zaidi ya watu 100 kuuawa katika siku za hivi karibuni, wakiwemo watu 70 waliouawa kwenye gereza la Saada.

USA Washington | Antony Blinken emäfgt den Saudi-Arabischen Ausßenminister Prinz Faisal Bin Farhan Al Saud
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia, Faisal bin Farhan na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony BlinkenPicha: Jonathan Ernst/AP Photo/picture alliance

Blinken amesema kuongezeka kwa mzozo huo kunaleta wasiwasi mkubwa kwa Marekani na amewatolea wito wote wanaohusika na mzozo wa Yemen kujizuia, kuzingatia na kuheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinaadamu na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Siku ya Ijumaa Blinken alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan na kumuhakikishia nia ya Marekani kuwasaidia washirika wake wa nchi za Ghuba kuimarisha ulinzi wao na amesisitiza umuhimu wa kupunguza madhara kwa raia.

Baraza la Usalama lasema hayo ni mashambulizi mabaya

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limelaani mashambulizi ya Abu Dhabi yaliyofanywa na waasi wa Houthi siku ya Jumatatu, likisema kuwa hayo ni mashambulizi mabaya ya kigaidi na limetaka wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Lakini katika taarifa yake kabla ya mkutano wa Ijumaa, rais wa baraza hilo Balozi wa Norway kwenye Umoja wa Mataifa, Mona Juul amelaani vikali mashambulizi mapya ya Yemen ambayo yamesababisha vifo kadhaa. Juul amesema wana wasiwasi sana na kwamba shambulizi hilo halikubaliki na ametoa wito wa pande zinazohusika kujizuia na mashambulizi.

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanasisitiza haja ya kuwawajibisha wahalifu, waandaaji na wafadhili wa vitendo hivyo vya kigaidi vinavyopaswa kulaumiwa na kuwafikisha mbele ya sheria.

(AFP, Reuters)