1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yataka eneo salama la kibinaadamu kuundwa Gaza

26 Oktoba 2023

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajadiliana kuhusu vita kati ya Hamas na Israel na pia kuanzishwa eneo salama la kupitisha misaada ya kiutu. Umoja huo pia unajadili hatua za kuchukua katika mgogoro mwengine wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Y4Ys
Jengo la makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels
Jengo la makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels Picha: Virginia Mayo/AP/dpa/picture alliance

Umoja wa Ulaya unajaribu kuwa na Umoja na ushawishi katika masuala ya migogoro iliyotokea katika eneo la Mashariki ya kati tangu Hamas, ilipoishambulia Israel Oktoba 7. Ukubwa wa umwagikaji wa damu huko, umesababisha Ulaya kuuangazia kwa undani zaidi mzozo huo wakati ambapo mashaka yanaongezeka juu ya uwezo wa mataifa ya Magharibi kuendelea kuiunga mkono Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi.

Baada ya siku kadhaa za majadiliano, rasimu ya taarifa ya hivi punde ya mkutano huo iliyoonekana na shirika la habari la AFP imetoa wito wa kuundwa kwa eneo salama la kupitishia misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza. Taarifa ya Umoja huo ambayo huenda ikabadilishwa wakati viongozi wake wanapokutana mjini Brussels, imekosa kushughulikia matakwa ya Umoja wa Mataifa ya kutaka usitishwaji wa mapigano.

Miito ya usitishwaji mapigano Gaza yatolewa

Ujerumani ambayo haitaki kutamka wazi kuhusu kusitishwa kwa mapigano, ikiona hilo ni kama kuifunga mikono Israel, ilitaka miito inayotolewa iwe ya kukubali maeneo hayo salama ya kibinaadamu.

Hata hivyo wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya wamepaza sauti zao na kusema iwapo ulaya itachelewa kutoa maneno sahihi juu ya mgogoro huu wakati idadi ya vifo ikiendelea kupanda, inaathiri hadhi ya umoja huo duniani na kuiacha ikidorora kimaendeleo.

Slovakia yasema haitatoa tena msaadawa kijeshi kwa Ukraine

Slowakei | Robert Fico
Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico Picha: Darko Bandic/AP Photo/picture alliance

Kingine kilichojitokeza ni hatua ya Waziri Mkuu mpya wa Slovakia Robert Fico, kusema serikali yake inasitisha msaada wa kijeshi nchini Ukraine, huu ukiwa ni msimamo wa kwanza kutoka Magharibi kuelekea Ukraine.

Fico aliwaambia wabunge kwamba nchi yake haitotoa misaada hiyo tena, akisema hilo ni moja ya ahadi zake katika kampeni yake, lakini akasema Slovakia itaendelea kutoa msaada wa kibinaadamu wa jirani yake huyo.

Zelenskiy atoa wito wa silaha zaidi kwa Ukraine

Baada ya tangazo hilo Urusi ilisema uamuzi wa Slovakia hautakua na athari yoyote kwa mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miezi 20. Msemaji wa serikali wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov aliwaambia waandishi habari kuwa Slovakia haikuwa inapeleka silaha nyingi nchini Ukraine.

Hata hivyo Fico amesema watu wa Slovakia wanamatatizo yao chungu nzima ya kuyashughulikia kuliko kuufuatilia mgogoro wa Ukraine. Ametoa wito wa mazungumzo ya amani akisema hilo ni bora kuliko kuendelea na mauaji jambo ambalo halitamfaidisha mtu yeyote.

Chanzo: afp