1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine yataka Urusi iwekewe vikwazo zaidi

22 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr zelenskiy ametoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo zaidi wakati ambapo mapigano bado ni makali katika eneo la Donbas.

https://p.dw.com/p/4D3NX
Der ukrainische Präsident Selenskyj besucht Mykolajiw
Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Wito huu wa Zelenskiy unakuja wakati ambapo Urusi Jumatano itafanya maadhimisho ya Vita vya Pili vya Dunia huku Rais Putin akitarajiwa kuweka shada la maua katika makaburi ya waliouwawa kwenye vita hivyo.

Katika ujumbe wake wa kila siku anaoutoa kwa njia ya video, Rais Zelenskiy alisema vikwazo zaidi vitakavyowekewa Urusi vitaifanya nchi hiyo ipate shinikizo la kiuchumi kutokana na gharama ya kuingia vitani na kusema kuwa washirika wa Ukraine wanastahili kuisaidia nchi hiyo na silaha kwa haraka kwa kuwa maisha ya maelfu ya watu yanategemea msaada huo.

"Ulipuaji wa kikatili wa mabomu hautowapa chochote wanapakalia kimabavu eneo hilo, jeshi la Urusi linajitia halielewi hali ilivyo. Linaendelea kuharibu na kuuwa. Eneo la kusini tunaendelea kuyatetea maeneo ya Mykolaiv na Zaporizhzhia na ukombozi wa Kherson unaendelea kwa haraka pia," alisema Zelenskiy.

Ukraine yalemewa katika mapigano ya mashariki

Iwapo Umoja wa Ulaya utaweka vikwazo hivyo, basi huu utakuwa ni mzunguko wa saba wa vikwazo ambavyo urusi imewekewa.

Katika wiki chache zilizopita, Urusi imeizidi nguvu Ukraine katika mapigano ya mashariki mwa nchi hiyo kutokana na zana nzito ilizo nazo. Majeshi ya Urusi yameendelea kuelekea eneo la Lysychansk ambalo ndilo eneo mojawapo ya machache yaliyosalia ambayo bado yako chini ya udhibiti wa majeshi ya Ukraine huko Donbas.

Der ukrainische Präsident Selenskyj besucht Mykolajiw
Zelenskiy akizungumza na gavana wa Mykolaiv Vitaly Kim (wa pili kulia)Picha: UKRAINIAN PRESIDENTIAL PRESS SERVICE/REUTERS

Jumatano serikali ya Ukraine ilisema mji wa viwanda ulioko mashariki wa Severodonetsk ni kama "jehanam" wakati ambapo majeshi ya Urusi yanazingira miji miwili mikuu huko Donbas ambako ndiko ilikoelekeza juhudi zake zote za kijeshi.

Gavana wa jimbo la Lugansk Sergiy Gaiday katika taarifa amesema watau wanaokolewa taratibu kutoka eneo la Lysychansk ingawa mamia ya wanaotafuta hifadhi katika kiwanda cha kemikali cha Azot huko Severodonetsk, hawakuweza kuondoka kutokana na mapigano makali yanayoendelea.

Haya yanafanyika wakati ambapo waziri wa ulinzi wa Ukraine OleksiiReznikov amesema awamu ya kwanza ya zana zilizoahidiwa Ukraine kutoka Ujerumani zimewasili nchini humo. Silaha hizo zimewasili baada ya Ukraine kuomba mara kadha msaada wa silaha.

Mwandishi kumiminiwa risasi kumi na nne kaskazini mwa Kyiev

Kwengineko shirika la Maripota wasio na Mipaka RSF lilisema Jumatano kwamba mpiga picha mmoja raia wa Ukraine na mwanajeshi aliyekuwa anaandamana naye wameuwawa kikatili walipokuwa eneo la msituni wakiitafuta ndege isiyo na rubani ya mwandishi huyo aliyokuwa anaitumia katika kazi yake ya kupiga picha.

Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Italia wawasili Kyiv

RSF ilisema imefanya uchunguzi wa vifo vya mwandishi huyo Maks Levin na mwanajeshi Oleksiy Chernyshov baada ya kurudi katika eneo ilikopatikana miili yao mnamo Aprili mosi. Shirika hilo lilisema lilihesabu tundu 14 za risasi katika gari walilokuwa wakitumia ambalo bado liko huko msituni kaskazini mwa mji mkuu Kyiev.

Hayo yakairifiwa Rais wa Urusi Vladimir Putin Jumatano anatarajiwa kuweka shada la maua kama kumbukumbu ya waliouwawa katika Vita vya Pili vya Dunia ambapo Ujerumani iliuvamia Umoja wa Sovieti mwaka 1941.