‘Ukimbizi ni madhila lakini si mwisho wa maisha’: Watumiaji wa DW Facebook wauelezea ukimbizi | Masuala ya Jamii | DW | 22.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

‘Ukimbizi ni madhila lakini si mwisho wa maisha’: Watumiaji wa DW Facebook wauelezea ukimbizi

Tuliwaomba wasomaji wetu wa Facebook wachangiane nasi hadithi zao juu ya dhana ya ukimbizi kwa kuwauliza ikiwa wamewahi kuishi maisha ya ukimbizi na kile walichopoteza au kujifunza.

Kambi ya wakimbizi ya Gashora inayowahifadhi wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda.

Kambi ya wakimbizi ya Gashora inayowahifadhi wakimbizi wa Burundi nchini Rwanda.

Majibu yao yalikuwa yanasimulia maana halisi ya ukimbizi sio tu kwa mkimbizi ambaye analazimika kuhama kwao kwa sababu mbalimbali, bali pia kwa wale ambao bado hawajawahi kuwa wakimbizi.

Kwa ujumla, wasomaji wetu walikuwa wanataka kutuambia kuwa mkimbizi kunamaanisha sio tu kupoteza nchi yako na mali yako, bali pia heshima, familia na baadhi ya wakati hata moyo wa kusonga mbele kama jamii ya kibinaadamu.

Kwa mfano ni Chrinda Mzee Christophe wa Butaganzwa Ruyigi nchini Burundi, ambaye anasema aliwahi kuwa mkimbizi kwa muda wa miaka 14 nchini Tanzania. “Maisha ya ukimbizini ni magumu sana na kuhuzunisha, kukatisha tamaa na hasara nyingi mno, ikiwemo kukosa heshima, huduma za msingi, uraia, haki....“

Kwa hali hiyo, mkimbizi huyu wa zamani anasema kamwe asingependa kuishi uhamishoni tena na wala asingemtakia binadamu yeyote aishi “maisha ya kuitwa mkimbizi, maana inauma sana, inachoma moyo.“

Christophe haishii kwenye dua tu, bali pia ana onyo kwa wale anaowaita waandaaji vita, akiwataka “…wafikirie madhara ya baadaye kisha wafanye maamuzi sahihi ili wasiturudishe tulikotoka.“

‘Jina la mkimbizi ni mkosi‘

Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania.

Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania.

Uzoefu wa kuwa mkimbizi ulitajwa pia na Faliala Msembengi Yanick kutoka Mbarara, Uganda. Anasema kwake hii imekuwa sehemu ya maisha yake. Anasimulia kuwa mwaka 1996 alijikuta akilazimika kuwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Lugufu, katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania. “Maisha mabaya sana! Mara unaitwa muhuni, huna uhuru, njaa, umaskini, magonjwa, mara ukosefu wa maji.“

Kwa Yanick, mkimbizi si yule anayehama nchi yake tu, kwani anasema hata ndani ya Uganda alikozaliwa na kukulia, alishawahi kuwa mkimbizi wa ndani. “...ndio hatari sasa mkimbizi hana haki ya shule! Jina mkimbizi ni mkosi na balaa!“

Ya kuwa mkimbizi wa ndani, yalimkumba pia Kiroba Mzee, ambaye anasimulia kuwa kisa cha yote ni pale alipoangusha mlingoti wa chama tawala kwenye nyumba ya balozi wa kijiji chake. “Acha mgambo wanisakame, dadi nikaamua kukimbia kijiji changu nikaenda kuishi ukimbizini huko mbali. Maisha yalikuwa ya shida sana. Nilokutana nayo huko ni mengi na ya kuhuzunisha.“

Na ndani yake, Mzee akapata funzo kubwa la maisha, nalo ni kuwa “usimdharau mtu yeyote katika hii dunia, maana hujui nani atakayekusaidia.“

Yusuf Ndihokubwayo wa mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, ambako kwa takribani mwaka sasa kumeshuhudiwa machafuko yaliyoanza kuzalisha wakimbizi wa ndani na wa kuvuuka mipaka ya taifa hilo la Afrika ya Kati, anasema naye aliwahi mkimbizi kwa zaidi ya miaka 18, akiishi kambi tofauti tafauti kwenye nchi tatu tafauti za Afrika Mashariki - Muyovozi nchini Tanzania, Kakuma nchini Kenya na kisha kwenye mji mkuu Nairobi na baadaye mji mkuu wa Uganda, Kampala.

‘Ukimbizi ulifungua macho‘

Hata hivyo, Ndihokubwayo anauangalia ukimbizi kuwa si laana ya moja kwa moja kama anavyodhani Yanick. “Kiukweli, kuwa mkimbizi si tusi, ila kuna haki nyengine huzipati, ukiwemo uhuru wa kutembea unavyotaka na kulazimishwa kufika katika makaazi yako mapema muda wa saa 12:00 jioni.“

Lakini kuna upande mgumu pia anauona pia. “Upande wa masomo huwa kusoma chuo kikuu si rahisi. Upande wa chakula ni mara chache utapata kile unachokitamani maana unakula ulichopokea kutoka kwa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa. Upande wa kuishi na wenyeji huwa si rahisi, maana baadhi yao wanawadharau, wengine wanawaelewa.”

Vikosi vya serikali vikiwakabili waandamanaji mjini Bujumbura.

Vikosi vya serikali vikiwakabili waandamanaji mjini Bujumbura.

Kwake yeye, licha ya maumivu yaliyomo kwenye ukimbizi, anaamini kuna jambo alilofaidika nalo. “…kujuwa namna ya kuishi na watu kutoka nyanja tofauti na kujua hali halisi ya maisha kwa hii dunia jinsi yanavyokwenda. Nilifaidi pia kuwa mvumilivu kwa hali ngumu, maana kuna siku unalala na njaa, kuna siku unapata. Na la mwisho, nilifunguka macho.”

Hata kwa wale ambao wameyaishi maisha yao hadi sasa wakiwa hawajalazimika kuyakimbia makaazi yao, bado kwao ukimbizi una maana. Wameona, wamesikia, wamehusika kwa njia moja ama nyengine kwenye kile kinachowasibu wenzao. Isayo Sambo wa Dodoma, Tanzania, anasema yeye binafsi hajawahi kuwa mkimbizi, bali "huwa nauvaa uhusika na kuona wengi wao wanapoteza mawasiliano na ndugu zao, wanakumbana na maisha mapya yenye changamoto nyingi ikiwemo kukosa uhuru binafsi.”

Andrea John wa Mhololo, mkoani Chato, Tanzania, ana fahari ya amani na utulivu nchini mwake, lakini anayasikia maumivu ya ukimbizi. “Sijawahi kuishi maisha ya ukimbizi, kwa kuwa nchi yetu i tulivu na ina amani, ila inasemekana ni mateso makubwa sana kuishi maisha hayo ya ukimbizi, mara mnaitwa wahamiaji haramu.”

Katika wakati huu, ambapo wakimbizi na wahamiaji haramu yamekuwa moja ya masuala makubwa ya siasa za kimataifa, kando na yale ya ugaidi na athari za mabadiliko ya tabia nchi, wasomaji wetu wanatufunza kwamba janga hili linalosababishwa kwa kiasi kikubwa na wanaadamu wenyewe linaweza kuepukika.

"Taifa lolote likiwa na amani ndio sehemu ya maisha ya watu wake na sehemu ya uchumi wake,” anasema Gidion Leonard Lubuye wa Ilemela, Mwanza, huku mwenzake, Jarbond Bwisengo, akiiomba DW "muwe munaizungumuzia hii mada kila wiki, labda itasaidiya wakimbizi waweze kueleweka ulimwenguni, maana hali yao ya maisha ni ngumu sana na hali ya kukata tamaa."

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW Kiswahili Facebook
Mhariri: Saumu Yussuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com