Ujerumani yataka kiti katika baraza la usalama la UN
28 Aprili 2026
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Johann Wadephul anatarajiwa hivi leo, kuimarisha kampeini ya nchi yake ya kutaka kupatiwa kiti kisicho cha kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kabla ya mchakato wa kura kwenye baraza kuu la Umoja huo Juni 3.
Wadephul atakutana na mabalozi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini New York kuipigia debe nchi yake kupata kiti hicho kwa mwaka 2027 hadi 2028.
Katika juhudi zake hizo,waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani pia atawasilisha nia ya Ujerumani kwa wajumbe kutoka mataifa 54 ya bara la Afrika , kundi ambalo ni muhimu katika kura hiyo.
Somalia,Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Liberia zinashikilia kwa sasa viti visivyo vya kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
Ujerumani imekuwa ikiunga mkono wito wa mataifa ya Afrika wa kudai mageuzi kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na bara hilo kutaka alau viti viwili vya kudumu na kura ya turufu.