Ujerumani yaongoza kundi C
10 Oktoba 2016Mabingwa wa dunia Ujerumani yaongoza kundi lake la C baada ya kupata ushindi katika michezo yake miwili ya mwanzo ya kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi. Kesho Jumanne(11.10.2016) itapambana na Ireland ya kaskazini.
Ujerumani iko katika njia salama kuelekea kuutetea ubingwa wake wa kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi baada ya kuiangusha jamhuri ya Czech kwa mabao 3-0 siku ya Jumamosi mjini Hamburg. Kikosi hicho cha kocha Joachim Loew kilionesha tangu mwanzo kuwa nani ni mwenye nyumba mjini Hamburg na mashabiki walijionea kandanda safi kutoka kwa kikosi hicho. Kocha wa Ujerumani Joachim Loew anathibitisha hayo kwa kusema.
"Nilikuwa na furaha tele, kwa sababu kikosi changu tangu mwanzo kilikuwa na udhibiti kamili wa mchezo huo. Ulikuwa ni mchezo mzuri sana wachezaji wakionesha mchezo wa hali ya juu na kupata mabao matatu, ambayo waliyapata kwa ushirikiano mzuri sana, ndio , nilifurahi sana."
Mkurugenzi wa Die Mannschaft Oliver Bierhoff alionesha furaha kwa kusema kikosi cha timu yake kimeweza kuudhibiti mchezo na kupata mabao ya uhakika.
"Ilikuwa hali ya kuonesha nguvu tuliyonayo, na ilikuwa hali nzuri. Na nafikiri, kwamba timu ilifanya vizuri tangu mwanzo hadi mwisho. Waliweza kucheza kwa ushirikiano na kujisikia raha uwanjani , na kuudhibiti mchezo mzima. Na hii inajionesha katika viwango. Ilikuwa muhimu , kwamba baada ya michuano iliyopita ya kufuzu, ambayo haikuwa mizuri kwetu, sasa tunawapa burudani mashabiki wetu."
Mapambano zaidi ya Ulaya
Kesho Jumanne (11.10.2016)Ujerumani itajitupa tena uwanjani mjini Hannover kupambana na Ireland ya kaskazini timu ambayo mara kadhaa huipa kibarua Die Mannschaft, lakini mara hii kocha Joachim Loew amesema kikosi chake kiko imara kuwaweka mahali wanapostahili Ireland ya kaskazini. Katika kundi C pia Norway iliyobugia mabao 3-0 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa kwanza mwezi uliopita, itajitupa uwanjani kuwania pointi tatu dhidi ya San Marino, wakati Jamhuri ya Czch inapambana na Azebarjain.
Leo Jumatatu(10.11.2016) kuna mapambano mengine barani Ulaya kuwania kufuzu kucheza katika fainali hizo, ambapo Ureno iko nyumbani kwa visiwa vya Faror, Uswisi inapambana na Andora, Ubelgiji iko Gibraltar , Bulgaria inapambana na Sweden na Ufaransa ina kibarua kigumu dhidi ya Uholanzi. Mlinda mlango wa Ufaransa Hugo Iloris amesema huo utakuwa mchezo mgumu sana kwa Ufaransa leo.
"Waholanzi wana wachezaji wengi ambao wanaweza kubadilisha mabo, hususan katika eneo la kati, mchezaji mmojawapo ninayemfikiria na ambaye ni muhimu sana katika timu hiyo ni Kevin Strootman , ambaye alikuwa majeruhi na sasa amerejea uwanjani , lakini pia washambuliaji wako na kasi sana na wanaweza kusababisha madhara katika mapambano ya mtu na mtu, lakini kwa jumla, timu ya Uholanzi ina penda kumiliki mpira na watafanya hivyo, ni timu ambayo ina wachezaji wengi wenye vipaji na kwa hiyo tunapaswa kuwa waangalifu sana kesho."
Ufaransa na Uholanzi zinaingia katika mchezo huo mjini Amsterdam wakiwa na rekodi zinazofanana katika kundi A.Kila timu ina pointi 4 baada ya michezo miwili , kila timu ilishinda mabao 4-1 na wako sawa kwa pointi na tofauti ya magoli.
Kocha Didier Deschamps , ambaye ikosi chake kilifikia fainali ya kombe la Ulaya mwaka 2016, alizungumza na vyombo vya habari na kusema.
"Huu ni utamaduni wa kandanda la Uholanzi , kikosi chao ni cha wachezaji chipukizi , lakini wenye vipaji, wanapenda kuumiliki mpira na kushambulia, wana wachezaji wenye uwezo wa kubadilisha mfumo wa mchezo na hususan washambuliaji. Kwa hiyo utakuwa mchezo tofauti kabisa kuliko siku ya Ijumaa kwa Ufaransa na Uholanzi."
Uturuki ilizamishwa jana na Iceland kwa kuchapwa mabao 2-0 mjini Reykjavic , wakati Iceland ikiimarisha sifa yake ya kuwa moja kati ya timu ngumu katika bara la Ulaya kuvunja ujasiri wao.
Katika mchezo wake wa kwanza Iceland ambayo ilifikia robo fainali ya kombe la Ulaya nchini Ufaransa mwaka huu , iliiangusha Finland kwa mabao 3-2.
Waingereza waongoza
Uingereza inaongoza kundi lake F baada ya kushinda michezo yake yote miwili ikiwa na pointi 6, licha ya kumbadilisha kocha wake na kuongozwa na Gareth Southgate baada ya kocha wao Sami Alerdice kuachia ngazi. Mlinda mlango Joe Hart hata hivyo amesema anatarajia kwamba Slovenia watawaiweka Uingereza katika mbinyo mkali wakati timu hizo zitakapopambana mjini Ljubljana kesho Jumanne.
Ushindi dhidi ya Slovakia na Malta umeiweka Uingereza juu ya msimamo wa kundi hilo F.
Mlinzi wa Uhispania Gerard Pique amepata uungwaji mkono kutoka kwa kocha wa kikosi hicho Julen Lopetegui pamoja na shirikisho la kandanda la Uhispania baada ya kutangaza nia yake ya kuachana na timu ya taifa baada ya kombe la dunia mwaka 2018.
Pique atangaza kuiacha timu ya taifa
Mlinzi huyo wa timu ya Barcelona , ambaye ameichezea timu ya taifa ya Uhispania mara 86 na kushinda kombe la dunia na ubingwa wa mataifa ya Ulaya na timu hiyo, alisema ukosoaji kila mara kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari , umeua furaha ya kuichezea Uhispania, baada ya ushindi wa mabao 2-0 jana Jumapili dhidi ya Albania.
Pique ambaye alizomewa na mashabiki wa Uhispania mwaka jana, alisababisha mijadala katika mitandao ya kijamii kwa kuvaa jezi yake dhidi ya Albania ambapo mikono ya jezi yake ilikatwa, na kuonekana kwamba aliondoa beji inayoonesha nembo ya mistari miekundu na njano rangi za Uhispania.
Kocha wa Uhispania Lopetegui amesema anahisi kumuunga mkono mlizi huyo.
China bado kidogo
Kutokuwepo kwa China kwa muda mrefu katika eneo la juu katika soka la kimataifa kunaonekana kutaendelea kwa takriban miaka mingine sita ijayo isipokuwa pale tu Gao Hongbo atakapoleta mabadiliko makubwa katika majaaliwa ya nchi hiyo baada ya mwanzo mbaya kabisa katika duru ya mwisho ya kufuzu kucheza katika kombe la dunia.
Wakati hatua zinazopewa hamasa na rais Xi Jinping kuibadili nchi hiyo kuwa moja ya nchi zilizoko katika nafasi za juu katika sekta ya soko la michezo zikishika kasi zaidi, na timu zenye utajiri mkubwa wa fedha zinaendelea kunawiri, hakujakuwa na mabadiliko kwa timu ya taifa.
Matumaini matatu ya Xi kwa soka la Uchina ni kwamba nchi hiyo ifuzu kucheza katika fainali nyingine za kombe la dunia baada ya kujitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 2002, iwe mwenyeji wa fainali za kombe la dunia na hatimaye ishinde kombe hilo.
Baada ya michezo mitatu kati ya 10 katika duru ya mwisho ya mchujo kwa mataifa ya bara la Asia kwa ajili ya fainali za mwaka 2018, hata hivyo, China ina pointi moja tu kutokana na sare ya bila kufungana na Iran.
Kipigo cha bao 3-2 dhidi ya Korea kusini kilitarajiwa lakini haikutarajiwa kupata kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Syria siku ya Alhamis, na ina maana mpambano wa kesho Jumanne dhidi ya Uzbekistan ni lazima China ishinde iwapo itataka kulazimisha kuwa moja kati ya timu zinazoweza kushika nafasi za juu katika kundi hilo hali ambayo itawapeleka Urusi kwa fainali hizo.
Barani Afrika , Nigeria kidedea
Kwa upande wa bara la Afrika Nigeria iliiangusha Zambia jana Jumapili kwa mabao 2-1 , katika kundi B. Nigeria imeanza juhudi hizo na mapema katika kundi lao gumu ambapo Algeria na Cameroon zilitosheka na sare ya bao 1-1 mjini Blida. Congo ilikubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Misri , wakati Tunisia iliishinda Guinea kwa mabao 2-0 nyumbani jana Jumapili.
Duru nyingine ya mchujo katika bara la Afrika itafanyika mwezi ujao lakini duru nne za mwisho zitafanyika kati ya Agosti na Novemba mwakani. Mshindi wa kila kundi kati ya makundi matano atashiriki katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi.
Wakati huo huo Libya imemfuta kazi kocha wake mkuu Javier Clemente baada ya kipigo kikubwa mwishoni mwa juma. Shirikisho la soka la nchi hiyo limetoa taarifa hiyo , bila ya kutoa maelezo, siku moja baada ya Libya kukandamizwa mabao 4-0 na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo katika kundi A mjini Kinshasa siku ya Jumamosi.
Na katika riadha:
Abel Kirui wa Kenya alichanja mbuga na kumpita bingwa Dickson Chumba katika kilometa za mwisho na kushinda mbio za Chicago Marathon jana Jumapili. Florence Kiplagat wa Kenya pia alishinda nae mbio zake za pili za Chicago Marathon mfululizo kwa wanawake. Kirui mwenye umri wa miaka 34 alimaliza mbio hizo za maili 26.2 katika muda ambao si rasmi wa saa 2 dakika 11 na sekunde 23.
Mpiganaji ngumi maarufu Aaron Pryor , akikumbukwa kwa mapambano yake makali na Alexis Arguello wa Nicaragua, alifariki jana akiwa na umri wa miaka 60 baada ya kuugua muda mrefu ugonjwa wa moyo.
"Tunasikitika sana na tuna majonzi kutangaza kwamba mpendwa wetu Aaron amefariki nyumbani ikiwa na familia yake, " Frankie Pryor , mjane wake, alisema katika taarifa nyumbani kwa familia yake karibu na Cincinati , Ohio.
Kwa taarifa hiyo ndio tunakamilisha habari hizi za michezo jioni ya leo. Hadi mara nyingine mimi ni Sekione Kitojo , Kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape / rtre / dpae
Mhariri: Mohammed Khelef